3077; Kwa nini umekubali?

Rafiki yangu mpendwa,
Sisi binadamu tuna uwezo mkubwa sana wa kufanya chochote kile tunachotaka kufanya.
Tunachohitaji tu ni sababu kubwa ya kwa nini tufanye kitu hicho.
Tunapokuwa na sababu kubwa huwa tunaitimiza.

Unapokuwa na msukumo mkubwa wa kufanya kitu, huwa unahakikisha unakifanya kweli.
Na unapokosa msukumo mkubwa wa kufanya kitu, hukifanyi.

Tumezoea kuangalia upande chanya wa uwezo pekee, lakini huwa hatuangalii upande hasi.
Upande hasi wa uwezo ni nguvu uliyonayo ya kuamua kutokufanya.

Kwa mfano, umepanga kabisa nini unapaswa kufanya ili kupiga hatua kwenye biashara yako.
Lakini inapofika kwenye utekelezaji, unaamua kutokufanya yale uliyopanga kufanya.

Wengi wanaposhindwa kufanya walichopanga kufanya, huwa wanajiuliza kwa nini hawajafanya.
Lakini hilo ni swali ambalo huwa halina majibu na hata likiwa nayo huwa hayana msaada.

Swali sahihi kujiuliza ni kwa nini umekubali kutokufanya?
Ni wewe mwenyewe umekaa chini na kupanga nini ufanye ili kupata matokeo mazuri.
Sasa iweje wakati wa kufanya unapofika ukubali kutokufanya?
Hilo ndiyo swali ambalo ukijipa majibu yatakuwa na tija kubwa kwako.

Tumeshaona una uwezo mkubwa wa kufanya chochote unachotaka.
Na hata pale unapopanga na ukashindwa kufanya, bado pia ni sehemu ya uwezo huo, kwa upande hasi. Yaani unakuwa umetumia uwezo wako mkubwa kuamua kutokufanya kile ulichopanga kufanya.

Tunajua kuwa sisi binadamu huwa hatuchukui hatua kama hakuna maumivu tunayokuwa tunapitia.
Hiyo ikiwa na maana kwamba ili tuchukue hatua, lazima maumivu ya pale tulipo yawe makubwa kuliko maumivu ya kuchukua hatua.

Hiyo ina maana kwamba kama umepanga kufanya kitu na hujakifanya, maumivu ya kutokukifanya siyo makubwa kama ya kukifanya.
Hivyo inakuwa rahisi kwako kutokufanya kuliko kufanya.

Unakubali kutokufanya pale maumivu ya kutokufanya yanavyokuwa madogo.
Kama kubaki kwenye mazoea hakukuumizi, basi utaendelea na mazoea.
Lakini kama mazoea yanakuumiza, utafanya kila kitu ili kutoka kwenye mazoea hayo.

Kama unaweza kupanga kitu unachopaswa kufanya lakini ukaamua kutokukifanya, ni dhahiri kwamba unaweza kuamua kukifanya pia.
Unachohitaji ni kuwa na sababu kubwa sana ya kufanya, ambayo inavuka sababu zote za kutokufanya.

Kwa sehemu kubwa, adui wa mafanikio yetu makubwa ni mazoea anbayo tayari tunayo.
Tusipoweza kuyavunja mazoea hayo na kujiweka kwenye mazingira yenye maumivu wakati wote kama hatutachukua hatua, tutaendelea kubaki kwenye mazoea hayo.

Hebu jiulize hapo ulipo sasa, ni mazoea gani yanayokukwamisha usifanye makubwa unayopaswa kufanya ili kupata mafanikio makubwa unayotaka?
Kwa sababu popote ulipo sasa kuna namna unajikwamisha kufanya makubwa zaidi unayojua unapaswa kuyafanya.
Ni mazoea gani yanayokuzuia kwa sasa?
Yajue hayo mazoea na uyavunje ili upate hasira za kufanya makubwa zaidi ya unavyofanya sasa.

Swali la msingi sana kujiuliza na kujijibu kila wakati ni mazoea gani yanakuzuia usijitoe mazima kwenye kile unachotaka kufanya?
Kwa sababu ukiweza kuyavuka mazoea hayo na kujitoa mazima mazima kwenye kile unachotaka, hakuna namna utashindwa kukipata.
Vunja mazoea, amua kisha jitoe mzima mzima kwenye kufanya.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe