Barua ya VI; Kushirikishana Maarifa.

Rafiki yangu Mstoa,
Tunaishi kwenye zama za maarifa na taarifa, ambapo nguvu kubwa ipo kwa wale wenye maarifa na taarifa sahihi na kufanyia kazi.

Pamoja na maarifa na taarifa kupatikana kwa wingi kwenye zama hizi, bado wengi sana wameshindwa kuzipata na kufanyia kazi, kitu ambacho kimepelekea wanaki nyuma.

Ili kuweza kufanikiwa kwenye zama hizi, tunahitaji kuwa na watu sahihi ambao tunashirikishana nao maarifa na taarifa muhimu.

Hilo aliliona Mwanafalsafa Seneca miaka zaidi ya elfu mbili iliyopita, kabla hata zama hizi za maarifa hazijaanza.
Kwenye barua yake ya sita kwa rafiki yake Lucilius, Seneca anaeleza umuhimu wa marafiki kushirikishana maarifa sahihi ili kuwa bora na kupiga hatua.

Kwa kuwa sisi ni marafiki kupitia falsafa hii ya Ustoa, napenda kuchukua nafasi hii kukushirikisha maarifa bora kutoka kwenye barua hiyo ili uweze kujifunza na kuchukua hatua sahihi. Karibu sana ujifunze.

1. Kujiboresha hakuna mwisho.

Huwa kuna kauli mbiu kwamba elimu haina mwisho. Lakini wengi wanapotumia kauli hiyo, huwa wanadhani ni kwa elimu ya darasani. Kwa kuwa kuna ngazi za juu zaidi za elimu kwa watu wanaotaka kujiendeleza zaidi.
Lakini uhalisia wa kauli hiyo ni kujiboresha binafsi hakuna mwisho. Kila wakati kuna kitu kipya unachoweza kujifunza na kukitumia kuwa bora zaidi ya ulivyokuwa.
Tena kwa hakika, pale unapojiambia umeshajua kila kitu na huna tena cha kujiboresha, ndiyo unakuwa umeanza kuanguka vibaya.

Hatua ya kuchukua;
Kila siku kuwa tayari kujifunza na kuchukua hatua ili kuboresha maisha yako. Usifike hatua yoyote na kuona tayari umeshajua kila kitu, kwani hapo ndipo anguko litakapoanzia.

Nukuu;
“I do not yet, however, assure myself, or indulge the hope, that there are no elements left in me which need to be changed. Of course there are many that should be made more compact, or made thinner, or be brought into greater prominence.” – Seneca

“Sijiaminishi au kujipa matumaini kwamba sina tena kitu cha kubadili ndani yangu. Bado kuna maeneo mengi yanayoweza kuboreshwa zaidi.” – Seneca.

2. Wengi wanakosa urafiki na siyo marafiki.

Marafiki ni muhimu sana kwenye maisha yetu. Kwa sababu hao ni watu tunaowachagua kulingana na mambo ambayo tunafanana.
Lakini kilicho muhimu siyo tu kuwa na marafiki, bali pia kuwa na urafiki.
Na Seneca anaeleza kwamba wanachokosa wengi siyo marafiki, bali urafiki.
Anaelezea urafiki kama hofu na matumaini yanayowaleta watu pamoja na kuvuka maslahi binafsi. Maslahi binafsi hayana nafasi kwenye urafiki na urafiki wa kweli ni ule unaokwenda mpaka kifo.
Urafiki unaletwa pamoja kwa matamanio sawa, ambayo hayawezi kuisha kwa mtu kwa maisha yake yote.
Kwa kuwa matamanio ya mtu huwa hayaishi kwa kipindi chote cha maisha yake, hivyo pia ndivyo urafiki wa kweli unavyodumu mpaka kifo cha mtu.

Hatua ya kuchukua;
Usiangalie tu marafiki ulionao, bali angalia urafiki uliojenga nao. Je urafiki wenu umejengwa kwenye nini? Kama unataka kujenga urafiki wa kudumu, angalia matamanio makubwa uliyonayo kisha ambatana na wenye matamanio ya aina hiyo. Kwa kuwa na ndoto kubwa unazozipambania na kuungana na wale wenye ndoto kubwa kama hizi, mtasafiri pamoja kwa miaka yenu yote.

Nukuu;
“I can show you many who have lacked, not a friend, but a friendship; this, however, cannot possibly happen when souls are drawn together by identical inclinations into an alliance of honourable desires.” – Seneca

“Naweza kukuonyesha wengi ambao walichokosa siyo marafiki, bali urafiki; lakini hilo haliwezi kutokea pale roho zinapoletwa pamoja kwa matamanio yanayofanana.” – Seneca

3. Kizuri mshirikishe rafiki.

Njia pekee ya kufurahia kitu kizuri unachokuwa nacho ni kuweza kumshirikisha rafiki yako.
Haijalishi kitu ni kizuri kiasi gani, kama utabaki nacho wewe mwenyewe, kinakosa maana.
Seneca anaeleza raha ya kujifunza ni kuwafundisha wengine na kama atapewa kitu kwa sharti la kubaki na kitu hicho peke yake, hatakikubali.
Hili la kushirikisha vitu vizuri kwa marafiki zetu ni muhimu sana hasa kwa zama hizi ambapo watu wengi huwa wana wivu na kukatisha tamaa. Marafiki wa kweli wanafurahia mafanikio yako, kwani nao pia wanataka kufanikiwa.
Hivyo chochote kizuri unachokipata, washirikishe marafiki zako.

Hatua ya kuchukua;
Unapopata kitu chochote kizuri usikae nacho peke yako, badala yake washirikishe marafiki zako. Kufanya hivyo kutaleta maana kubwa kwa kile ulichopata.

Nukuu;
“No good thing is pleasant to possess, without friends to share it.” – Seneca

“Hakuna kitu kizuri ambacho utakifurahia kama huna marafiki wa kuwashirikisha.” – Seneca

4. Usiwape tu vitabu, waonyeshe na pa kusoma.

Seneca anasema haitoshi tu kuwapa marafiki zako vitabu vya kusoma, bali pia unapaswa kuwaonyesha wapi pa kusoma.
Hiyo ni kwa sababu vitabu ni vingi na virefu, mtu hawezi kumaliza kusoma vyote. Hivyo kwa kumwonyesha maeneo muhimu ya kusoma yatakayompa maarifa sahihi kwake, unakuwa umemsaidia sana rafiki yako.
Kilicho muhimu zaidi ni kuwashirikisha marafiki zako vitabu ambavyo vimekuwa na manufaa kwako na kuhakikisha na wao wanayapata manufaa hayo kwa kuwaelekeza wapi wasome.

Hatua ya kuchukua;
Washirikishe marafiki zako vitabu ambavyo vimekuwa na manufaa kwako na wawekee kabisa alama maeneo gani ya kusoma ili wapate kile unachotaka wapate.

Nukuu;
“I shall therefore send to you the actual books; and in order that you may not waste time in searching here and there for profitable topics, I shall mark certain passages, so that you can turn at once to those which I approve and admire.” – Seneca

“Nitakutumia vitabu halisi na ili kukusaidia usipoteze muda kutafuta wapi pa kusoma, nitaweka alama kwenye kurasa zenye manufaa ili uweze kwenda moja kwa moja kwenye hizo.” – Seneca

5. Kusoma pekee haitoshi, lazima uende kwenye eneo la tukio.

Tunaweza kujifunza mambo mengi kwa kusoma, lakini tutajifunza kwa uhakika zaidi pale tunapokwenda kwenye eneo la tukio.
Pale tunaposhiriki moja kwa moja kwenye kuchukua hatua za kujifunza, tunaelewa na kuwa bora zaidi.
Utatumia muda mfupi kujifunza na utaelewa kwa kina zaidi kama utashiriki moja kwa moja kwenye zoezi la kujifunza, badala tu ya kusoma au kusikiliza.
Shiriki mafunzo muhimu kwa kuchukua hatua ili uweze kuwa bora.
Seneca anasema kujifunza kwa kufuata maagizo kunachukua muda mrefu na kueleweka kunakuwa kudogo, lakini kujifunza kwa kuiga mfano kunachukua muda mfupi na kueleweka kwa haraka.
Kwa kuwa karibu na wale unaojifunza kwao, utajifunza kwa urahisi na uhakika zaidi.
Hivyo basi, chochote unachotaka kujifunza, tafuta mtu aliyefanikiwa kwenye kitu hicho kisha jifunze kwake.

Hatua ya kuchukua;
Tafuta fursa za kujifunza kwa kufanya ili uweze kujifunza haraka na kwa uhakika. Usiishie tu kufuata maagizo, bali fuata mifano. Usiishie tu kusoma au kusikiliza, bali fanya pia.

Nukuu;
“Of course, however, the living voice and the intimacy of a common life will help you more than the written word. You must go to the scene of action, first, because men put more faith in their eyes than in their ears, and second, because the way is long if one follows precepts, but short and helpful, if one follows patterns.” – Seneca

“Kusikia sauti iliyo hai kutakusaidia kuliko tu kusoma maandishi. Unapaswa kwenda kwenye eneo la tukio, moja kwa sababu watu wanaamini zaidi wanachoona kuliko wanachosikia na mbili, kwa sababu njia ni ndefu kama mtu atafuata maaguzo lakini fupi na yenye msaada kama mtu ataiga mfano.” – Seneca

6. Ili kuwa rafiki mzuri kwa wengine, anza kuwa rafiki kwako mwenyewe.

Seneca anaeleza kwamba hatua kubwa ambayo mtu anaweza kupiga kwenye maendeleo yake binafsi ni kuwa rafiki yake yeye mwenyewe.
Anasema unapoanza kuwa rafiki yako mwenyewe, kuna manufaa makubwa mawili; moja, kamwe huwezi kuwa mpweke, kwa sababu tayari wewe ni rafiki yako mwenyewe na pili, unaweza kuwa rafiki bora kwa wengine wengi.
Huwa tunajifunza huwezi kuwapa wengine kile ambacho huna na pia kuwataka wengine wakupe ambacho umeshindwa kujipa  mwenyewe ni ubinafsi.
Anza kwa kuwa rafiki yako wewe mwenyewe, jipe urafiki wa kweli ili pia uweze kuwapa wengine urafiki na wao pia waweze kukupa urafiki.

Hatua ya kuchukua;
Kila siku kuwa rafiki bora kwako mwenyewe. Zijue ndoto kubwa na matamanio uliyonayo, jipende, jiamini na jikubali sana. Hilo litafanya usiwe na upweke hata kama uko peke yako. Lakini zaidi itafanya uwavutie marafiki sahihi kuja kwako.

Nukuu;
“What progress, you ask, have I made? I have begun to be a friend to myself.” That was indeed a great benefit; such a person can never be alone. You may be sure that such a man is a friend to all mankind.” – Seneca

“Unauliza ni hatua gani nimepiga? Nimeanza kuwa rafiki yangu mwenyewe. Hilo lina manufaa makubwa kwa sababu mtu wa aina hiyo kamwe hawezi kuwa mpweke. Unaweza kuwa na uhakika mtu wa aina hii atakuwa rafiki kwa watu wote.” – Seneca

Rafiki yangu Mstoa, wanasema kizuri kula na rafiki zako. Inapokuja kwenye maarifa mazuri unayoyapata na yakawa na manufaa kwako, usiyafanye kuwa siri kwako, bali washirikishe marafiki zako.
Na ili uweze kupata marafiki wazuri, anza kwa kuwa rafiki mzuri kwako mwenyewe.
Kilicho muhimu siyo marafiki ulionao, bali urafiki unaokuwa nao, kwa sababu huo ndiyo wenye nguvu ya kuwaweka pamoja kwa kipindi chote cha maisha yenu.

Kutoka kwa Mstoa mwenzako,
Kocha Dr Makirita Amani.