Sisi binadamu asili yetu ni viumbe vya kijamii. Maisha yetu yamejengwa katika misingi ya mahusiano. Kila mtu yuko hapa duniani kwa sababu tayari kuna watu ambao anahusiana nao.

Hatuwezi kuishi kwa kujitegemea wenyewe kwa kila kitu. Tunawahitaji wengine ili maisha yetu yaende. Ni kama vile viungo vya mwili vilivyokuwa na ushirikiano.

Na njia bora ya kuimarisha mahusiano na ushirikiano ni kuangalia tabia nzuri zilizopo ndani ya wengine badala ya kuangalia mabaya tu.

Falsafa ya Ustoa inatufundisha jinsi ya kutengeneza mahusiano bora na wale wanaotuzunguka kwa kuimarisha mahusiano yetu  na ushirikiano kwenye mambo mbalimbali.

Aliyekuwa Mtawala wa Roma na Mwanafalsafa wa Ustoa, Mwanafalsafa Marcus Aurelius alikuwa na maneno mazuri ya kutuambia kuhusu mahusiano;

Say to yourself first thing in the morning: I shall meet with people who are meddling, ungrateful, violent, treacherous, envious, and unsociable. They are subject to these faults because of their ignorance of what is good and bad. But I have recognised the nature of the good and seen that it is the right, and the nature of the bad and seen that it is the wrong, and the nature of the wrongdoer himself, and seen that he is related to me, not because he has the same blood or seed, but because he shares in the same mind and portion of divinity. So I cannot be harmed by any of them, as no one will involve me in what is wrong. Nor can I be angry with my relative or hate him. We were born for cooperation, like feet, like hands, like eyelids, like the rows of upper and lower teeth. So to work against each other is contrary to nature; and resentment and rejection count as working against someone. – Marcus Aurelius, Meditations.

Jiambie hili kitu cha kwanza asubuhi: Leo nakwenda kukutana na watu ambao ni waovu, wasio na shukrani, wenye fujo, wasaliti, wenye wivu na wasiojali.
Watu hao wako hivyo kwa sababu hawajui kipi kizuri na kipi kibaya. Lakini mimi natambua asili ya uzuri na nimeona kipi sahihi na asili ya ubaya na kuona kipi kisicho sahihi na asili ya wanaofanya ubaya na kuona wana uhusiano na mimi, kwa sababu wana damu sawa na yangu na tunashirikiana mawazo yetu. Siwezi kuumizwa na yeyote kwa sababu hakuna anayeweza kunihusisha kwenye ubaya wake. Pia siwezi kuwa na hasira au kumchukia ndugu yangu. Sote tumezaliwa kwa ushirikiano, kama miguu, mikono, kope za macho, meno ya juu na ya chini.
Hivyo kufanya kazi kwa kupingana ni kinyume na asili na chuki na kukataana ni kufanya kazi kinyume na wengine.

Kabla hujaanza siku yako, kila siku asubuhi jiambie tu kauli hiyo kwa sababu usipojiandaa kiakili basi utavurugwa sana.
Watu wengi siku hizi wamevurugwa na maisha yao. Wana matatizo yao ambayo wanatafuta mtu wa kumuuzia na wewe ukikubali tu kununua umeisha.

Kununua matatizo ya watu ni pale unapotaka kuwarekebisha kwa yale waliyofanya.

Siku moja nilikuwa niko kwenye gari la umma, mama mmoja aliingia kwenye gari na kutaka kukaa, kwenye siti kulikuwa na dada mmoja, na kulikuwa na nafasi ila alikuwa amekaa vibaya. Yule mama aliyeingia ndani akamuomba naomba usogee ili na mimi nikae, yule dada alimwangalia usoni yule mama bila kumwambia neno, baadaye anamwambia si ukae, kwani siti huoni? Watu wengine sijui wakoje? Alimtukana yule mama, na yule mama alijisikia vibaya kibinadamu, yule dada aliongea mengi, alikuwa na kisirani chake, hivyo kisirani chake na matatizo yake akaamua kumpelekea yule mama.

Ikitokea mtu anakukanyaga, anakusukuma njiani, anakutukana, amekuibia, amekudhulumu, ana wivu, na mengine mengi yanayofanana na hayo wala hata usimjibu, Bali jiambie kauli ya kifalsafa ambayo tumejifunza kutoka kwa mstoa mwenzetu, jiambie tu nilijua tu nitakutana na watu kama hawa, kisha endelea na maisha yako.

Sina uhakika kama itakufaa lakini ukitaka kupambana na mtu ambaye tayari ana matatizo yake lazima atakuuzia, na lengo lako wewe kwenye siku ni kuuza na siyo kununua matatizo ya watu. Usikubali kuingia kwenye mitego.

Fokasi na orodha yako ya mambo uliyopanga kwa siku na haya mengine usikubali kuyaruhusu yakuvurugie utulivu wa akili hata siku moja.

Kitu kimoja zaidi, ikitokea mtu amekutendea ndivyo sivyo, usihangaike naye na jua anafanya hivyo kwa sababu ya matatizo yake binafsi.

Jiambie tena,
Siwezi kuumizwa na yeyote kwa sababu hakuna anayeweza kunihusisha kwenye ubaya wake.
Pia siwezi kuwa na hasira au kumchukia ndugu yangu. Sote tumezaliwa kwa ushirikiano, kama miguu, mikono, kope za macho, meno ya juu na ya chini.

Kutoka kwa Mstoa mwenzako,
Mwl Deogratius Kessy