3086; Uhakika wa ushindi.

Rafiki yangu mpendwa,
Maisha ni mchezo mkubwa ambapo kila mtu anapambana kupata ushindi ambao ni mafanikio.

Pamoja na kila mtu kuwa kwenye mapambano hayo, ni wachache sana ambao wanapata ushindi mkubwa wanaokuwa wanautaka.

Wengine wengi sana hawaupati ushindi huo, licha ya kukazana sana kuiga yale ambayo wachache wanaoshinda wamekuwa wanayafanya.

Kwenye mchezo wa aina yoyote ile, kushinda au kushindwa huwa hakuanzii uwanjani, bali kunaanzia kwenye mtazamo wa mchezaji mwenyewe.

Mambo ambayo watu wanafanya kwa nje yanatofautiana sana, lakini wote wanaopata ushindi, huwa na mtazamo ambao unaendana.

Kama unataka kuwa na uhakika wa ushindi kwenye safari yako ya maisha, kuna mambo makubwa matatu unayopaswa kuyajenga kwenye mtazamo wako.

Moja ni kuchukua hatua kubwa sana.
Hakuna ushindi unaopatikana bila kuchukua hatua ambazo ni kubwa.
Unatakiwa kuchukua hatua kubwa sana kwenye kila unachotanya kwenye maisha yako ili kuzalisha matokeo makubwa na ya tofauti.
Kila wakati unapaswa kufanya tofauti na ulivyozoea kufanya, ili uweze kupata matokeo ya tofauti pia.
Mara zote kaa kwenye upande wa kuchukua hatua kubwa.

Mbili ni kuendelea kusonga mbele bila ya kujali mambo unayokabiliana nayo.
Kuchukua hatua kubwa haimaanishi kwamba mambo yatakuwa rahisi kwako.
Mambo yatakuwa magumu, utakutana na kila aina ya changamoto na vikwazo mbalimbali.
Ili kupata ushindi wa uhakika, unapaswa kuendelea mbele bila ya kukwamishwa na chochote.
Wewe unapaswa kuwa na mwendo wa aina moja tu, ambao ni kusonga mbele bila ya kujali umekutana na nini.
Ni ung’ang’anizi huu wa kusonga mbele ndiyo unaokupa ushindi wa uhakika.

Tatu ni kutokujali kuhusu maumivu, kushindwa, kukataliwa, kupoteza, kudharauliwa na kukatishwa tamaa. Unajua nini, hayo ni mambo ambayo lazima utakutana nayo kwenye safari yako ya maisha. Lazima uyapokee na kuendelea na mashindano bila kukwama. Ukijali tu kuhusu mambo hayo, ukianza kuona wewe hustahili kukutana nayo, hapo ndipo unapokuwa umekaribisha kushindwa.
Unapaswa kuendelea na safari yako kama vile mambo hayo hayajakutokea, licha ya kwamba kila wakati yatakuwa yanakutokea.
Ukiweza kuyapuuza hayo, ushindi kwako ni swala la muda tu.

Hutapata ushindi mkubwa kwenye maisha yako kwa kuangalia yale ambayo wanaoshinda wanayafanya.
Unayoona kwa nje hayana nguvu kubwa kama yale yaliyo ndani ya fikra za watu.
Jenga mambo haya matatu uliyojifunza kwenye fikra zako na ushindi utakuwa ni wa uhakika kwako.

Mara zote chukua hatua ambazo ni kubwa sana kuliko ulivyozoea.
Endelea kusonga mbele kwa kasi kubwa bila ya kujali mambo unayokabiliana nayo.
Na futa kabisa yasiyoendana na ushindi unaotaka, unachotaka wewe ni ushindi tu, mengine yote unayapuuza.
Ukiweza kukamilisha hayo, ushindi unakuwa wa uhakika kwako bila ya kujali ni vitu gani unavyofanya kwa nje.
Kaa kwenye njia hii ili upate ushindi wa uhakika kwenye maisha yako.

Itangazie dunia nzima ielewe kwamba upo kwenye haya maisha kwa ajili ya kitu kimoja pekee, ambacho ni ushindi.
Akili yako haipaswi kuwa na msamiati mwingine isipokuwa ushindi pekee.
Unashinda kwa uhakika pale unapokataa kupokea chochote kisichokuwa ushindi.
Anzia hapo na kwa hakika utashinda.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe