Barua ya VII; Epuka makundi.

Rafiki yangu Mstoa,
Kwa asili sisi binadamu ni viumbe wa kijamii na huwa tunapenda kuwa ndani ya kundi fulani.
Huwa tunajiona tukiwa salama zaidi ndani ya kundi kwa kuamini watu wengi hawawezi kukosea.

Lakini hilo siyo sahihi, watu huwa wanakosea zaidi kwenye kundi kuliko wakiwa peke yao.
Hivyo kama unataka kufikiri kwa usahihi na kufanya maamuzi sahihi, unapaswa kuepuka kushawishiwa na kusukumwa na kundi.

Huo ni ushauri ambao Mwanafalsafa Seneca aliutoa kwa rafiki yake Lucilius kwenye barua ya saba aliyomwandikia.
Karibu tujifunze kuhusu kuepuka makundi kwenye barua hii ili tuweze kufanya maamuzi bora.

1. Makundi yanakuvuruga.

Seneca anasema tunapaswa sana kuepuka makundi kwa sababu huwa hayatuachi na utulivu tuliokuwa nao.
Mara zote tunapojihusisha na makundi, huwa yanatuvuruga.
Anasisitiza huwezi kuyaamini makundi kwa usalama wako.
Kuwa ndani ya makundi kunaibua udhaifu ulio ndani yako.

Hatua ya kuchukua;
Kwa utulivu wako wa nafsi na akili, epuka kuwa ndani ya makundi.
Makundi yanakuchochea kufuata mkumbo kwa mambo yasiyokuwa sahihi kwako.

Nukuu;
“To consort with the crowd is harmful; there is no person who does not make some vice attractive to us, or stamp it upon us, or taint us unconsciously therewith. Certainly, the greater the mob with which we mingle, the greater the danger.” – Seneca
“Kufuata kundi ni hatari; hakuna mtu anaweza kuwa ndani ya kundi na akatoka hajaambukizwa maovu. Kadiri kundi linavyokuwa kubwa, ndivyo pia hatari inakuwa kubwa.” – Seneca

2. Michezo inachochea zaidi makundi.

Hakuna eneo linalochochea kufuata makundi na kufuata mkumbo kama ushabiki wa michezo mbalimbali.
Watu wanapokuwa wanashabikia michezo, huwa wanachukuliwa na hisia za kundi na kuacha kufikiri kwa akili zao.
Seneca anaeleza jinsi ambavyo kwenye ushabiki wa michezo, watu wanaweza hata kushangilia pale mwingine anapokuwa anauliwa.
Kwa mfano kwenye michezo ya mieleka, mchezaji mmoja anakuwa anampiga mwingine na watu wanashabikia mpaka hata anaweza kumuua.
Kama tunataka kuweka fikra zetu sawa wakati wote, tunapaswa kuepuka sana ushabiki wa michezo mbalimbali, hasa ile yenye madhara kwa wengine.

Hatua ya kuchukua;
Epuka kuwa shabiki wa michezo yenye madhara kwa watu wengine. Maana kwa kushabikia kwako unakua umechangia kudhuriwa kwa mtu mwingine.

Nukuu;
“But nothing is so damaging to good character as the habit of lounging at the games; for then it is that vice steals subtly upon one through the avenue of pleasure.” – Seneca
“Hakuna kitu kinachoharibu tabia njema kama ushabiki wa michezo; kwa sababu ni rahisi uovu kumwingia mtu kupitia starehe.” – Seneca

3. Makundi yana ushawishi mkubwa, hata kwa wanaojielewa.

Kuna watu huwa wanadhani wanaweza kuwa kwenye makundi na yasiwe na athari kwao.
Wanajiona wanaweza kujihusisha na makundi hayo kwenye mambo yenye manufaa, na kuepuka yale yasiyo na manufaa, yaani maovu.
Lakini huko ni kujidanganya tu.
Kundi lina ushawishi mkubwa kwa mtu yeyote yule, hata wenye uelewa mkubwa.
Seneca anaeleza hata wanafalsafa waliokuwa na uelewa sana kama Socrates, bado waliweza kuathiriwa na kundi.

Hatua ya kuchukua;
Acha kujidanganya kwamba utaweza kuzuia kundi lisikuathiri, ukishakuwa ndani ya kundi, utaathiriwa na kundi hilo na hakuna namna unaweza kujizuia.
Njia pekee ya kuepuka madhara ya kundi ni kutokuwa ndani yake.

Nukuu;
“The young character, which cannot hold fast to righteousness, must be rescued from the mob; it is too easy to side with the majority. Even Socrates, Cato, and Laelius might have been shaken in their moral strength by a crowd that was unlike them; so true it is that none of us, no matter how much he cultivates his abilities, can withstand the shock of faults that approach, as it were, with so great a retinue.” – Seneca
“Vijana wadogo ambao bado hawajawa na msingi wa yaliyo sahihi wanapaswa kuokolewa kutoka kwenye kundi; kwa sababu ni rahisi kwao kufuata mkumbo. Hata Socrates, Cato, na Laelius wangeweza kutikiswa kwenye maadili yao kwa kuwa ndani ya kundi ambalo ni tofauti na wao; hivyo pia ndivyo ilivyo kwetu sote, haijalishi tumejijengea uwezo kiasi gani, hatuwezi kuhimili mtikisiko wa kuwa ndani ya kundi.” – Seneca

4. Usiige wala kudharau.

Inapokuja kwenye kukabiliana na makundi, watu huchukua upande mmoja kati ya hizi mbili; kuiga kundi au kudharau kundi.
Seneca anatuambia hatupaswi kuchukua njia yoyote kati ya hizo mbili, usiige kundi kwa sababu lina watu wengi na wala usilidharau kwa sababu linatofautiana na wewe.
Badala yake jitenge na makundi kadiri uwezavyo, na ujihusishe na wale wanaokusukuma kuwa bora zaidi.

Hatua ya kuchukua;
Usiingie kwenye makundi kwa sababu ya wingi wa watu na wala usiyashambulie kwa kuona wewe uko sahihi zaidi yao. Badala yake epuka makundi na ungana na wale wanaokufanya kuwa bora zaidi.

Nukuu;
“Withdraw into yourself, as far as you can. Associate with those who will make a better man of you. Welcome those whom you yourself can improve. The process is mutual; for men learn while they teach.” – Seneca
“Jitenge na makundi kadiri uwezavyo. Jihusishe na wale wanaokufanya kuwa bora. Wakaribishe wale unaoweza kuwafanya kuwa bora. Ni mchakato wenye manufaa kwa wote, kwa sababu watu wanajifunza vizuri pale wanapofundisha.” – Seneca

5. Epuka kutafuta umaarufu kwa kujisifia.

Watu wengi huwa wanapenda kuwa ndani ya makundi ili kupata umaarufu kupitia kujisifia kwa mambo mbalimbali wanayokuwa nayo.
Hilo huwa halina manufaa yoyote zaidi ya kukaribisha changamoto kutoka kwenye makundi hayo, ambayo yatataka kujinufaisha zaidi na kile unachojisifia nacho.
Seneca anasema kwa sehemu kubwa makundi hayawezi kukuelewa kwa kile unachojisifia nacho, hivyo hata kama ulikuwa unalenga kupata watu sahihi, unaishia kutokuwapata.

Hatua ya kuchukua;
Unaweza kudhani kuwa ndani ya kundi ni kupata watu sahihi kwako, lakini kwa bahati mbaya sana wengi wanaokuwa kwenye makundi huwa wanakuwa siyo sahihi kwako.
Hivyo acha kutafuta umaarufu ndani ya makundi, haitakunufaisha.

Nukuu;
“There is no reason why pride in advertising your abilities should lure you into publicity, so that you should desire to recite or harangue before the general public…. as it is, there is not a man of them who can understand you.” – Seneca
“Hakuna sababu ya kutafuta umaarufu kwa kujisifia ndani ya kundi, …. kwa sababu hakuna atakayekuelewa.” – Seneca

6. Kauli tatu za kufungia.

Seneca anamaliza barua hii kwa kumshirikisha rafiki yake Lucilius nukuu tatu alizojifunza kwa wengine na anazoona zina somo kubwa kwake.

Ya kwanza ni ya Democritus ambaye alisema: “One man means as much to me as a multitude, and a multitude only as much as one man.”
Akimaanisha; “Mtu mmoja ana maana kwangu kama watu wengi, na watu wengi wana maana kwangu kama mtu mmoja.”

Ya pili ni iliyosemwa na mtu mwingine aliyeulizwa nini faida ya kujifunza mambo mengi yanayowafikia wachache, akajibu: “I am content with few, content with one, content with none at all.”
Akimaanisha; “Nimeridhika na wachache, nimeridhika na mmoja na nimeridhika ba pasipo yeyote.”

Ya tatu ni kutoka kwa Epicurus, ambaye alimwandikia mmoja wa washirika wake kwenye kujifunza: “I write this not for the many, but for you; each of us is enough of an audience for the other.”
Akimaanisha; “Naandika haya siyo kwa ajili ya wengi, bali kwa ajili yako; kila mmoja wetu anatosha kuwa hadhira ya mwenzake.”

Kwa kauli hizo tatu, tunajifunza kwamba kilicho muhimu siyo kuwa na watu wengi au watu wachache, bali kilicho muhimu ni kuwa na watu sahihi.
Hivyo tukazane sana kujenga mahusiano bora na watu sahihi, ili tuweze kuwa bora na kuwafanya wao kuwa bora pia.

Tumejifunza mengi hapa kuhusu madhara ya kuwa kwenye makundi mabaya.
Tuyaepuke makundi kwa sababu ya ushawishi mkubwa kwetu na tujihusishe na watu ambao wanatufanya kuwa bora na sisi tunawafanya wawe bora pia.

Kutoka kwa Mstoa mwenzako,
Kocha Dr Makirita Amani.