3091; Tumwombee akue.

Rafiki yangu mpendwa,
Mtoto anapozaliwa, huwa hatuwi na wasiwasi kama atakua au la.
Tunachojua ni kadiri muda utakavyokuwa unaenda, kuna mabadiliko ya ukuaji ambayo tutayaona kwake.
Hatuhitaji kuwa na wasiwasi wala kumwombea mtoto ndiyo akue.
Ukuaji tayari upo ndani yake, kinachohitajika ni muda na mazingira sahihi ili ukuaji huo uweze kupatikana.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye biashara tunazofanya.
Ukuaji wa biashara hizo haujitaji tufanye maombi au kuwa na wasiwasi wa aina yoyote.
Tunachohitaji ni kuendesha biashara hizo kwa misingi sahihi na kujipa muda wa kutosha na biashara itakua tu.
Kama muda unakwenda na biashara haikui, kunakuwa na shida kwenye misingi ya uendeshaji wa biashara hiyo.
Hivyo mtu huhitaji wasiwasi wala maombi, unachohitaji ni kuendesha biashara kwa misingi sahihi na kujipa muda na matokeo yatakuja.

Kadhalika, kwa mantiki hiyo hiyo, hatuhitaji kuwa na wasiwasi wowote juu ya lengo kubwa ambalo kila mmoja wetu analo, lengo na kufikia ubilionea.
Hatuhitaji maombi ili kufika huko, tunachohitaji ni kufuata misingi na kujipa muda wa kutosha.
Misingi tayari tunayo, ambayo ni kujenga biashara na kufanya uwekezaji. Tukitekeleza hayo kwa ukubwa na usahihi, tukajipa muda wa kutosha, lazima tutafikia lengo.
Hatuhitaji kuwa na wasiwasi juu ya ukubwa wa lengo au urefu wa muda.
Ukipanda mchicha na mbuyu siku moja, ukuaji wake hautakuwa sawa. Yote ni mimea na hata kama utaipa mazingira sawa, itatofautiana kwenye muda wa ukuaji.

Lengo la ukurasa huu ni tuache kuhangaika na mambo yasiyokuwa na tija, hasa wasiwasi kwenye safari ambayo tupo.
Tunachohitaji ni kukaa kwenye mchakato sahihi, kuchukua hatua zinazopaswa kuchukuliwa na kujipa muda wa kutosha.
Pia tunapaswa kujipima na kujitathmini kadiri muda unavyokwenda ili kuona kama tupo kwenye uelekeo sahihi au kama tunahitaji kufanya maboresho zaidi.
Hizo ndizo hatua tunazopaswa kuchukua ili kuweza kujenga biashara kubwa na kufikia lengo la ubilionea.

Hupaswi kupoteza muda wako kuwa na wasiwasi kama utafikia lengo la kujenga biashara yenye mafanikio.
Huhitaji hata kufanya maombi ili biashara iweze kukua.
Kila biashara tayari ina ukuaji ndani yake.
Unachohitaji ni kukaa kwenye mchakato sahihi na kujipa muda wa kutosha.
Hakuna lengo utakaloshindwa kulifikia kama utakaa kwenye mchakato sahihi na kujipa muda wa kutosha.
Hayo ndiyo maeneo makubwa mawili kwa upande wako kufanyia kazi ili kufika popote unapotaka kufika.

Mchakato sahihi kwenye lengo lolote ni ule ambao tayari umeshawawezesha wengine kufikia lengo hilo hilo.
Kwa kufanya kile ambacho tayari wengine wameshafanya na kupata matokeo, ni rahisi kwetu kupata matokeo pia.
Haya mambo hayahitaji kubahatisha.
Yanafuata kanuni sahihi na za uhakika.
Wajibu wako ni kufanyia kazi kanuni hizo, kujipa muda na kujitathmini kadiri unavyokwenda.
Hakuna chochote kinachoshindikana kwa kufanya yale yaliyo sahihi.
Tuyafanye hayo na tuache kuwa na wasiwasi au kuhangaika na mengi yasiyokuwa na tija.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe