3092; Kamari yenye ushindi wa uhakika.

Rafiki yangu mpendwa,
Kila mtu anataka ushindi kwenye maisha yake.
Ni hitaji hilo la ushindi ndiyo limekuwa linawasukuma watu wengi kufanya mambo hata yasiyokuwa na tija, ili tu kuona wameshinda.

Tunaona watu wengi wakiwa na ushabiki mkubwa wa michezo mbalimbali. Yote hiyo ni kutaka ushindi.
Na kwenye hiyo michezo, kumeongezeka kitu kingine ambacho kimezidi kuwateka watu kwenye hitaji lao la ushindi.
Kitu hicho ni kamari au kaka wanavyoita kwa lugha ya kuhadaa, michezo ya kubahatisha.

Watu wengi wamekuwa na uraibu na kamari hizo, huku wakipoteza fedha nyingi, lakini hawaachi kwa sababu ya matumaini ya kupata ushindi.
Lakini huo unakuwa ushindi ambao siyo wa uhakika.
Pamoja na kukosekana huko kwa uhakika wa ushindi, bado watu wanaendelea na kamari hizo kwa sababu ya matumaini wanayokuwa nayo, hasa kwa ushindi mdogo waliowahi kupata au kwa kuona ushindi wa wengine.

Leo nataka nikushirikishe aina ya kamari ambayo ushindi ni wa uhakika.
Kamari hiyo unapewa kete mbili uzirushe kwa pamoja, zote zikionyesha namba sita juu, unapata fedha.
Kama zitaonyesha namba nyingine tofauti, hutapata fedha, lakini pia hutapoteza chochote.
Lakini pia unapata nafasi ya kuendelea kurusha hizo kete.

Swali ni je utafanya nini ili uweze kupata fedha nyingi zaidi?
Jibu ni moja, kurusha kete hizo mara nyingi uwezavyo.
Kwa sababu ukipatia unapata fedha, na ukikosea hupotezi chochote, hivyo ukirusha mara nyingi, unajiweka kwenye nafasi ya kupatia zaidi na kuingiza fedha nyingi zaidi.

Sasa fikiria kamari hiyo hiyo, lakini kwa sasa siyo kete, bali wateja unaowafikia ili kuwauzia.
Hiyo ni kamari, lakini yenye uhakika.
Ukimfikia mteja, iwe ni kwa kumtembelea au kwa simu na kumshawishi kununua, kama atanunua utakuwa umeingiza fedha.
Na kama atakataa kununua huingizi fedha, lakini pia unakuwa hujapoteza fedha yoyote ile.

Hivyo swali linakuja tena, unatakiwa kufanya nini ili kuingiza fedha nyingi zaidi kwenye mauzo?
Na jibu ni moja tu, wafikie wateja wengi zaidi.

Mauzo ni kamari yenye uhakika wa ushindi.
Kwa kuwafikia wateja na kuwashawishi kununua, wakikubali unaingiza fedha.
Na wakikataa, hakuna unachokuwa umepoteza.
Hivyo ili kupata ushindi kwa uhakika, unapaswa kuwafikia wateja wengi zaidi.

Kwa nini watu hawachezi kamari hii ya uhakika wa ushindi na isiyo na kupoteza?
Kwa sababu inahusisha kufanya kazi.
Na watu huwa hawapendi kazi,
Badala yake wanataka njia za mkato za kupata fedha.
Na njia hizo za mkato zinaishia kuwakata hata fedha kidogo wanazokuwa nazo.
Wewe epuka njia za mkato na kuwa tayari kuweka kazi, ushindi utakuwa wa uhakika kwako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe