3095; Ongeza shinikizo.

Rafiki yangu mpendwa,
Vitu vyote imara kwenye maisha huwa vinatengenezwa kwa shinikizo kubwa.
Madini ya almasi, ambayo ndiyo magumu zaidi na yenye thamani kubwa, ni mkaa ambao umepita kwenye shinikizo kubwa na kwa muda mrefu.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwa watu, watu wanaofanikiwa sana, ambao pia ndiyo huwa watu imara zaidi, huwa wanapitia shinikizo kubwa kwenye maisha yao.

Dan Pena, ambaye ni Kocha wa ufanisi mkubwa, huwa anasema kizazi cha sasa hakiwezi kupata mafanikio kwa sababu ni laini sana na kikipitia shinikizo kinalegea badala ya kuwa imara.

Watu wengi huwa hawapendi kukutana na ugumu au changamoto kwenye maisha yao.
Hivyo huwa wanakazana kutafuta njia rahisi na kukwepa njia ambazo ni ngumu.
Cha kushangaza, kwenye kukwepa ugumu, kunawaacha wakiwa laini na wasioweza kukabiliana na chochote.

Sehemu ya mafanikio makubwa ni uimara wa kukabiliana na wajibu ambao unaambatana na mafanikio hayo.
Wengi kwa kukosa uimara wa kutosha, huwa wanashindwa kuyahimili hata mafanikio madogo wanayopata, hivyo wanayapoteza.

Shinikizo ndiyo nishati inayokusukuma upate mafanikio makubwa.
Shinikizo linakupa njaa na hasira ya kukusukuma kufanya vitu vipya na vikubwa zaidi.
Bila ya shinikizo, watu huwa wanarudi kwenye mazoea na uzembe ambao wamekuwa wanafanya mara nyingi.

Unapaswa kuchukua hatua za hatari zaidi.
Chochote unachohofia kufanya, hicho ndiyo unapaswa kuanza kukifanya mara moja.
Hofu unayokuwa nayo juu ya kitu fulani ni kiashiria kwamba kitu hicho ni kipya na kikubwa kwako.
Ukiacha kufanya kwa sababu ya hofu, unakuwa umekwepa shinikizo na hivyo kujinyima fursa ya ukuaji.

Bila ya kuchukua hatua kubwa na za hatari.
Bila ya kufanya yale unayohofia kufanya.
Bila ya kupita kwenye shinikizo kubwa.
Huwezi kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yako.

Kila wakati wa maisha yako, unapaswa kuwa kwenye shinikizo ambalo unalifanyia kazi.
Adui mkubwa wa mafanikio makubwa ni kuwa kwenye utulivu na kuridhika kwa muda mrefu.
Usikubali kuwa kwenye hali hiyo ya utulivu na kuridhika hata kwa muda mfupi.
Kila wakati tengeneza hali zinazokupa shinikizo ili likusukume kufanikiwa.

Kila unapojiona ukiea kwenye hali ya utulivu na kuridhika, chukua hatua zinazokuweka kwenye hatari na hivyo kusukumwa kuchukua hatua za tofauti.

Kuna hatua nyingi za hatari unazoweza kuchukua ili kujiweka kwenye shinikizo ambalo litakusukuma kufanikiwa.
Unaweza kuchukua mkopo ambao ni mkubwa, ambao utakusukuma ufanye zaidi ili uweze kuuza zaidi na kulipa deni.
Pia unaweza kuwaahidi watu vitu vikubwa na ambavyo havijazoeleka.
Ahadi hiyo inaambatana na adhabu kubwa kama utashindwa kuitekeleza. Hilo litakupa shinikizo kubwa la kuhakikisha unatekeleza.

Kwa kifupi, pale unapojikuta una raha, utulivu na kuridhika, usijisifie kwamba umeshafanikiwa, bali shtuka kwa sababu upo kwenye njia ya upotevu.
Kila wakati unapaswa kuwa chini ya shinikizo fulani.
Kila wakati unapaswa kuwa kwenye hali ya kujisukuma zaidi.
Hiyo ndiyo inayokufanya uwe imara zaidi na ujenge mafanikio makubwa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe