Barua ya VIII; Jinsi ya kuishi kifalsafa ili kufanikiwa.
Rafiki yangu Mstoa,
Watu wengi wanaposikia kuhusu kuishi kifalsafa, huwa wanaona hiyo siyo kwa ajili yao.
Huwa wanadhani kuishi kifalsafa ni kwa ajili ya wale waliosomea falsafa au waliopo kwenye dini na imani za aina mbalimbali.
Lakini ukweli ni kwamba, kama unataka kuwa na maisha bora na yenye mafanikio makubwa, njia pekee ya kufikia hilo ni kuishi kifalsafa.
Kuishi kifalsafa haimaanishi kuwa mtu wa tofauti sana, au kuacha yale unayofanya sasa na kwenda kufanya mambo mengine.
Badala yake inamaanisha kufanya kwa ubora yale ambayo tayari tunayafanya ili kuzalisha matokeo bora zaidi.
Falsafa ya Ustoa ni moja ya falsafa zinazoendana vizuri sana na maisha ya mafanikio tunayopambana kuyajenga.
Kwani falsafa hiyo inatupa misingi sahihi ambayo tukiweza kuisimamia, tutaweza kufanya makubwa sana, huku pia tukibaki na utulivu mzuri.
Tunajua mafanikio huwa yanakuja na changamoto zake mbalimbali, ikiwepo kumpa mtu wasiwasi mkubwa kuhusu kupoteza yale ambayo ameshayapata.
Falsafa ya Ustoa inatupa kinga ya wasiwasi huo na kutuweka huru kuyafurahia mafanikio tuliyoyajenga.
Na hata ikitokea tumepoteza yale tuliyokuwa nayo, bado hilo halitutetereshi sana.
Kwenye barua ya nane ambayo Mwanafalsafa Seneca aliiandika kwa rafiki yake Lucilius, alimweleza jinsi anavyoishi kifalsafa.
Baada ya kuitafakari barua hiyo kwa kina, nimeona tunaweza kuigeuza kuwa ndiyo falsafa tunayoishi nayo kwenye hii safari ya mafanikio.
Kwani mambo aliyoyagusia kwenye barua hiyo, tukiyaishi kimafanikio, tutaweza kufanya makubwa, lakini pia kubaki na utulivu mkubwa hata baada ya kuwa tumefanikiwa.
Karibu tujifunze misingi mitano muhimu ya kuishi kifalsafa ili kuweza kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yetu.
1. Peleka muda wako wote kwenye kujenga mafanikio.
Seneca anamwambia rafiki yake Lucilius kwamba huwa anachagua kujitenga na watu na kupeleka muda wake wote kwenye kujifunza na kuandika kuhusu falsafa.
Anasema anaamini kwa kufanya hivyo ataweza kuwasaidia watu wengi zaidi, kuliko akiutawanya muda wake kwenye mambo mengi yasiyokuwa na tija.
Anasisitiza huwa hapotezi muda wowote kwa kutokuwa na cha kufanya. Usiku na mchana ameutoa kwa ajili ya falsafa na analala pale mwili unapokuwa umechoka na siyo vinginevyo.
Seneca anaendelea kueleza hajajitenga tu na watu, bali pia amejitenga na mambo yote ambayo hayana mchango kwake kwenye kujenga falsafa ambayo itakuja kuwa na manufaa kwa watu wengi zaidi.
Kwa kupeleka muda wake wote kwenye kujenga falsafa, anakuwa ameleta manufaa makubwa kwa wengi.
Hatua ya kuchukua;
Peleka muda wako wote kwenye mafanikio unayoyajenga. Usipoteze muda wako kwa watu ambao hawana mchango kwenye mafanikio unayojenga. Na pia epuka mambo yote ambayo ni usumbufu kwenye safari yako ya kujenga mafanikio makubwa.
Muda wako ni mchache, utumie vizuri ili kuweza kujenga mafanikio makubwa unayoyataka.
Nukuu;
“I never spend a day in idleness; I appropriate even a part of the night for study. I do not allow time for sleep but yield to it when I must, and when my eyes are wearied with waking and ready to fall shut, I keep them at their task.” – Seneca
“Huwa sipotezi siku bila ya kuwa na kitu cha kufanya. Natumia muda wangu mpaka wa usiku kujifunza. Huwa sina muda wa kulala, bali nalala pale inapohitajika, pale macho yanapokuwa yamejaa usingizi.” – Seneca
2. Tambua mafanikio makubwa unayojenga siyo kwa ajili yako pekee.
Watu wengi wamekuwa wanakwama na kukata tamaa kwenye safari ya kujenga mafanikio makubwa, hasa pale wanapokutana na vikwazo na changamoto.
Kinachowafanya wakate tamaa na kuacha ni kwa sababu ya ubinafsi.
Wanakuwa wanajenga mafanikio kwa ajili yao wenyewe.
Kwa sababu ya ubinafsi wao, inakuwa rahisi kwao kukata tamaa.
Seneca alimweleza rafiki yake Lucilius kwamba kazi anayoifanya siyo kwa ajili yake mwenyewe bali kwa ajili ya wengine, na siyo kwa ajili ya kizazi chao tu, bali kwa ajili ya vizazi vingi vinavyofuata.
Seneca anasema kazi kubwa aliyokuwa anaifanya kwenye kujifunza na kuandika falsafa ni kuwaelekeza wengine njia sahihi za kufuata kwenye maisha ili kuepuka makosa na changamoto ambazo wengine wamepitia.
Kwa kuifanya kazi yake kuwa kwa ajili ya wengine, ilikuwa rahisi kwake kuipa muda mwingi bila ya kukata tamaa.
Hatua ya kuchukua;
Mafanikio makubwa unayotaka kuyafikia, usijiangalie peke yako tu, bali waangalie wengine wengi watakaonufaika sana na mafanikio hayo.
Angalia wati ambao watanufaika na suluhisho unaloleta.
Angalia watu ambao utawapa fursa za ajira.
Na angalia watu ambao watanufaika na misaada utakayotoa kutokana na mafanikio yako.
Hao wote wanakutegemea sana wewe ufanikiwe.
Hivyo pale unapotaka kukata tamaa na kuiacha safari hiyo, usijiangalie tu peke yako, bali waangalie hao wote.
Hilo litakupa msukumo wa kuendelea licha ya magumu unayokuwa unakutana nayo.
Nukuu;
“I point other men to the right path, which I have found late in life, when wearied with wandering.” – Seneca
“Nawaelekeza watu kwenye njia sahihi ambayo nimeijua kwa kuchelewa kwenye maisha yangu.” – Seneca
3. Uadabishe mwili ili utii akili.
Ni mara ngapi umepanga kuamka mapema ila muda wa kuamka unapofika mwili unakushawishi uendelee kulala?
Ni mara ngapi umepanga kupunguza au kuacha kula vyakula vya aina fulani lakini unajikuta unaendelea kula?
Mara ngapi umepanga kuachana na ulevi wa vitu mbalimbali, lakini unajikuta bado unaendelea?
Kila mmoja wetu kuna namna ambavyo miili yetu imekuwa inakosa adabu kwa akili zetu.
Akili inapanga vizuri kabisa kile kilicho sahihi kwetu kufanya ili kupata mafanikio makubwa, lakini miili inaleta uasi kwa akili na kutuangusha.
Seneca alijua hatari iliyopo kwa miili yetu kuwa kikwazo kama haitaadabishwa.
Ndiyo maana alimshauri rafiki yake Lucilius auadabishe mwili kwa kuupa yale tu ya msingi na siyo ya ziada.
Alimwambia anapaswa kula ili kutuliza njaa, kunywa ili kukata kiu, kuvaa ili kujikinga na baridi na kuwa na nyumba kwa ajili ya kujilinda.
Alimwonya asiruhusu anasa zozote kwenye maeneo hayo ya maisha, kwa sababu yote ni mambo ya kupita.
Tamaa za mwili huwa hazina mwisho, badala ya kutawaliwa na tamaa hizo, tunapaswa kuuadabisha mwili ili utii akili.
Hatua ya kuchukua;
Kile unachopanga kwenye safari yako ya mafanikio, tekeleza kama ulivyopanga, bila kujali mwili unataka au hautaki.
Uzoeshe mwili wako kutii akili yako kwa kutekeleza yote uliyopanga kwa jinsi ulivyopanga.
Amka muda uliopanga kuamka, hata kama mwili haujisikii kuamka.
Kula kile ulichopanga kula na kwa kiwango ulichopanga, usiruhusu ulafi.
Na kama kuna kitu chochote ambacho mwili wako umeshakuwa na ulevi nacho, amua sasa kukiacha mara moja. Na ukishaacha, usirudi tena nyuma.
Uonyeshe mwili wako kwa vitendo kwamba akili ndiyo inayoongoza na hivyo inapaswa kupewa utii.
Nukuu;
“Hold fast, then, to this sound and wholesome rule of life; that you indulge the body only so far as is needful for good health. The body should be treated more rigorously, that it may not be disobedient to the mind.” – Seneca
“Zingatia sheria hii ya maisha; upe mwili kile tu inachohitaji kwa ajili ya afya njema. Unatakiwa kuutesa mwili wako ili uweze kuwa na utii kwa akili yako.” – Seneca
4. Mafanikio ni kuwa mtumwa wa mchakato.
Wanaoyataka mafanikio makubwa ni wengi.
Wanaochukua hatua ili kuyapata mafanikio hayo ni wengi.
Ila wanaoyapata mafanikio hayo kwa uhakika ni wachache sana.
Unajua kwa nini?
Kwa sababu wengi huwa wanakimbizana na kila fursa inayokuja mbele yao, wakijaribu kila kitu kipya wanachokisikia.
Wakati mafanikio makubwa yanataka mtu ufanye kitu kimoja kwa muda mrefu na kwa msimamo bila kuacha.
Watu wengi huwa wanachoka haraka kwenye kufanya kitu kimoja kwa muda mrefu na kujikuta wakikimbilia vitu vipya vinavyokuja.
Hapo ndipo kuwa mtumwa wa mchakato kunapokuwa na faida kubwa kwa mtu.
Kwa kujisalimisha kwenye mchakato, unakuwa huru kukaa kwenye safari ya mafanikio na kuepuka kukimbizana na mambo mapya yanayojitokeza.
Kuchagua kuwa mtumwa wa mchakato unakuwa umechagua kuwa huru kuyajenga mafanikio unayoyataka.
Seneca alimshauri rafiki yake Lucilius kwa kumnukuu Epicurus kwamba ili kufurahia uhuru halisi kwenye maisha, anapaswa kuwa mtumwa wa falsafa.
Hatua ya kuchukua;
Kwa mafanikio makubwa unayotaka kuyafikia, jua mchakato sahihi utakaokufikisha kisha kuwa mtumwa wa mchakato huo. Ufuate mchakato huo bila kukubali kuyumbishwa na kitu chochote. Puuza mengine yote na baki kwenye mchakato huo. Hilo linakupa uhuru mkubwa kwenye maisha yako kwa kukuepusha na wimbi la kukimbizana na fursa mpya zinazojitokeza kila wakati na kuwapoteza wengi.
Nukuu;
“If you would enjoy real freedom, you must be the slave of Philosophy.” – Epicurus
“Kama unataka kufurahia uhuru kamili, unapaswa kuwa mtumwa wa falsafa.” – Epicurus
“The man who submits and surrenders himself to her is not kept waiting; he is emancipated on the spot. For the very service of Philosophy is freedom.” – Seneca
“Mtu anayejitoa na kujisalimisha kwenye falsafa, anapata uhuru wake hapo hapo bila ya kusubiria. Kwa sababu huduma kuu ya falsafa ni uhuru.” – Seneca.
Nyongeza; unapokaa kwenye mchakato ndiyo mafanikio yenyewe, kwa sababu hakuna kinachoweza kukuzuia kufanikiwa kama utakaa kwenye mchakato kwa msimamo bila kuyumba.
5. Kila ulichopewa, kitachukuliwa.
Watu ambao wanapambana maisha yao yote ili kujenga mafanikio makubwa, kwa kudhani watayafurahia maisha baada ya kuwa wamefanikiwa, huwa wanajikuta wakienda maisha yao yote bila ya kuwa na furaha.
Wanapokuwa hawajafanikiwa wanakuwa na wasiwasi kama wataweza kuyapata mafanikio.
Baada ya kufanikiwa wanakuwa na wasiwasi kwamba watayapoteza mafanikio waliyoyapata.
Kwa kuwa na wasiwasi kila wakati, watu wanashindwa kuyafurahia mafanikio waliyoyapata.
Seneca anamkumbusha rafiki yake Lucilius, kupitia maandiko ya wanafalsafa wengine kwamba kitu chochote ambacho mtu umepewa, unaweza kukipoteza.
Na huo ndiyo ukweli, kwa sababu hata maisha tuliyonayo, hatutakuwa nayo milele, yatafikia tamati.
Hivyo hatupaswi kuwa na wasiwasi kuhusu kupoteza mafanikio ambayo tumeyapata, ni sawa na kurudisha kitu ambacho ulikuwa umeazimwa kwa muda.
Hatua ya kuchukua;
Chukulia mafanikio uliyoyapata kama kitu ambacho umeazimwa, inapofika wakati wa kurudisha, usiumie.
Pambana kujenga mafanikio makubwa na kuyalinda, lakini inapotokea umeyapoteza, usiumie na kukosa furaha, jua muda uliopewa wa kuwa nayo umeisha.
Ondoa wasiwasi na hofu zozote unazokuwa nazo juu ya kupoteza mafanikio ambayo umeshayapata, unakua hujayapoteza, bali umeyarudisha yalipotoka.
Nukuu;
“Still alien is whatever you have gained
By coveting.”
“What Chance has made yours is not really yours.”
“The good that could be given, can be removed.”
“Chochote ulichopata kwa tamaa, siyo chako.”
“Ambacho asili imekupa, siyo chako milele.”
“Kizuri unachoweza kupewa, unaweza pia kukipoteza.”
Mafanikio yangekuwa rahisi, kila mtu angekuwa nayo.
Yanakuwa magumu kwa sababu watu wengi wanaoyataka mafanikio hawapo tayari kulipa gharama inayohitajika.
Na gharama hiyo ni kubafili kabisa jinsi ambavyo mtu anayaishi maisha yake.
Kwa kuyaishi maisha yako kifalsafa na kuzingatia misingi mitano tuliyojifunza hapa, utaweza kujenga mafanikio makubwa na kuyafurahia maisha yako wakati wote.
Ni imani yangu wewe rafiki yangu Mstoa utaiishi misingi hii kwa uhakika ili kuwa na maisha bora.
Kutoka kwa Mstoa mwenzako,
Kocha Dr Makirita Amani.
Mafanikio ni kuwa mtumwa wa mchakato.
LikeLike
Hivyo tu, unakuwa umemaliza.
LikeLike
Mchakato no Boss wako wa mafanikio. Mfate kwa utiifu na hakikisha unamsikiliza yeye pekeyake kwa mwendelezo. Ukimwacha anguko litakukuta
LikeLike
Kwa utii mkubwa.
LikeLike
Asantee kocha naandelea kuwa tofauti Kila siku kwa sababu ya mchakato ambao umeuanzisha na tunaufuata hapo ndipo mabadiliko yangu yalipo kwa kuwa nimechagua kufanikiwa sipaswi KWENDA kinyume na huu mchakato ni tafeli tu kuanzia sasA MUDA WANGU NITATUMIA KWA MAMBO MUHIMU TU SITAYUMBISHWA NA MAMBO MENGINE BALI NI YALE NILIYOYAPANGA KUYATEKELEZA.ASANTEEE
LikeLike
Kila la kheri.
LikeLike
Asante sana kwa somo zuri mstoa mwenzangu,uhuru ndio huduma kuu ya ustoa.
LikeLike
Karibu
LikeLike
Kukaa kwenye mchakato ndio mafanikio yenyewe
Asante kocha kwa somo maarifa haya.
LikeLike
Karibu.
LikeLike
Ni kweli ni lazima ukubali kuwa ulichopata kuna siku vitaondoka na wewe ukabaki kama ukivyo jambo la msingi hapo ni kuwa tayari kukubaliana bayo ba kuanza moja na kwa kua una mchakato utapata tena na hata zaidi ya hapo
LikeLike
Kabisa, tuamini kwenye mchakato.
LikeLike
Kuishi kifalsafa ni kufanya kwa ubora Yale ambayo tayari
unayafanya ili kuzalisha matokeo Bora. Pia epuka Mamb
o yote ambayo ni usumbufu kwenye safari yako ya kujen
ga mafanikio makubwa na ni hakika utafanikiwa
Asante Sana kocha.
LikeLike
Karibu
LikeLike
Asante Kocha,
Nilichopata kwa tamaa siyo changu…
Nilichopata kwa kupewa na asili siyo changu milele…
Kizuri ninachoweza kupewa ninaweza pia kukipoteza…
LikeLike
Hakika
LikeLike
Asante sana
LikeLike
Karibu
LikeLike
Ni kweli kabisa mafanikio sio kitu rahisi lazima uwe na dhamira ya dhati kabisa ya kuyapata mafanikio na kujitoa kwelikweli katika kukaa katika mchakato.
LikeLike
Hakika
LikeLike
Asante kocha,Nikufanya kwa msimamo na kukaa kwenye mchakato.
LikeLike
Vizuri
LikeLike
Ukitaka kuwa na maisha bora ishi kifalsafa.
LikeLike
Kabisa
LikeLike
Peleka muda wako wote kwenye kujenga mafanikio.
2.Tambua mafanikio makubwa unayojenga siyo kwa ajili yako pekee.
3.Uadabishe mwili ili utii akili.
4.Mafanikio ni kuwa mtumwa wa mchakato.
5.Kila ulichopewa, kitachukuliwa.
LikeLike
Tukae humo.
LikeLike