3097; Usiwaambie, waonyeshe.

Rafiki yangu mpendwa,
Moja ya mahitaji muhimu kwenye safari yetu ya mafanikio ni kuwa na timu bora kabisa.

Safari ya mafanikio ni kama maisha ya mwituni, simba hata awe mkali kiasi gani, anahitaji kuwa ndani ya kundi la simba wengine.
Simba akiwa peke yake, japo anaweza kuonekana shujaa, huwa hawezi kudumu kwa muda mrefu.
Kwani akikutana hata na kundi la fisi wenye ushirikiano mzuri, wanatosha kumsumbua sana.

Kadhalika, kwenye safari yako ya mafanikio, ukiwa peke yako unaweza kuonekana ukienda kwa kasi kubwa. Lakini hautaweza kufikia mafanikio makubwa na hata mafanikio yoyote utakayoyapata hutaweza kudumu nayo kwa muda mrefu.

Unahitaji timu nzuri na imara ili kujenga mafanikio makubwa na pia kuyalinda ili ubaki nayo kwa muda mrefu.

Wengi wanapofikiria kuhusu timu, huwa wanakwamishwa na tabia tofauti tofauti za watu.
Huwa wanachoka pale wanapoona wanahitajika kuwabadili watu tabia ambazo wanazo ili waendane na utamaduni wanaoujenga.
Watu wakifikiria ugumu wa watu kubadilika, huona haina haja ya kujisumbua na watu, bora wafanye mambo yao peke yao.

Ni kweli kabisa ya kwamba watu siyo rahisi kubadilika, lakini hilo halipaswi kukukwamisha kwenye kujenga timu.
Badala yake unapaswa kujenga timu, kwa kuzingatia msingi mzuri wa kuwashawishi watu kubadilika.

Msingi huo siyo kuwaambia watu kile wanachopaswa kufanya, bali kuwaonyesha kwa mfano.
Unapaswa kuwa mabadiliko unayotaka kuyaona kwa wengine, ongoza kwa mfano, ongoza ukiwa mbele ya wengine.
Chochote unachotaka watu wakifanye, anza kukifanya wewe mweyewe kwa msimamo mkubwa.
Usifanye tu kwa muda, bali fanya kwa msimamo kila mara.

Baada ya kufanya, kinachofuata ni kutumia zawadi na adhabu kwenye timu yako.
Unawapa zawadi wale wanafanya vizuri na kuwaadhibu wale wasiofanya.
Hilo pia unalifanya kwa msimamo bila kuacha.

Haitachukua muda utaona mabadiliko makubwa sana kwenye timu yako.
Wale wanaotaka kubaki kwenye timu watajisukuma kubadilika wao wenyewe ili waendane na timu.
Huku wale ambao hawawezi kubadilika wakikimbia wenyewe kwa sababu ya adhabu wanazokuwa wanapata mara kwa mara.

Kwa kutumia njia hii ya kuonyesha kwa mfano kisha kutoa zawadi na kuadhibu, utaweza kujenga utamaduni bora kabisa kwenye biashara yako bila ya kutumia nguvu kubwa.
Unakuwa umetumia nguvu mbili kubwa za mabadiliko kwa wakati mmoja.
Unatumia nguvu ya kuiga, kwa sababu binadamu tuna tabia ya kufuata mkumbo.
Lakini pia unakuwa umetumia nguvu ya zawadi na adhabu, huwa tunafanya tunayozawadiwa na kuepuka tunayoadhibiwa.

Kwa wewe kuanza kufanya kwa mfano, kisha wengine kuiga, wengine wengi zaidi watashawishika kuiga, kwa sababu hicho ndiyo kinaonekana kuwa kitu sahihi, wengi wape.
Wachache ambao hawatasukumwa na kuiga, wakipata adhabu watashtuka na kuiga au watakimbia kwa kuona hawapo sehemu sahihi.
Kwa vyovyote vile, utakuwa umeibuka na ushindi, kwa kuweza kujenga utamaduni sahihi kwenye biashara yako.

Kama unataka timu yako iwahi kwenye kazi, kuwa wa kwanza kufika kabla ya wote, wataanza kuiga. Wazawadie wanaowahi, hata kama ni kwa kuwasifia na waadhibu wanaochelewa, hata kama ni kwa kuwasema. Nenda hivyo kwa msimamo na utajikuta ukiwa na timu ya watu wanaowahi.

Kama unataka timu yako ifanye mauzo makubwa, anza kwa kuuza kwa ukubwa wewe mwenyewe. Kisha wape zawadi wale wanaofanya mauzo makubwa na wape adhabu wanaofanya mauzo madogo. Fanya hivyo kwa msimamo na utaweza kujenga timu inayofanya mauzo makubwa.

Tumia mfumo huu rahisi kujenga tabia na utamaduni wowote unaoutaka kwenye timu yako.
Fanya kwa mfano, wazawadie wanaofanya na waadhibu wasiofanya.
Fanya hayo kwa msimamo bila kuacha na matokeo yatazaliwa mazuri.

Neno kuhusu msimamo, ni muhimu sana unapofanya hayo ufanye kwa mwendelezo na msimamo bila kuacha.
Hiyo ni kwa sababu watu huwa wanajua kupima nguvu ya soda.
Wakiona kuna mabadiliko unayoleta, wanajua hayatadumu kwa muda mrefu.
Hivyo wataweza kuigiza kwa muda mfupi wakisubiria uchoke na kuacha na wao pia wanaacha.
Ukifanya kwa msimamo na mwendelezo bila kuacha, watu watachoka kuigiza, hivyo wataamua kufanya kweli au kukimbia.

Waonyeshe, wazawadie na waadhibu, mfumo rahisi wa kujenga tabia na utamaduni bora kwenye timu yako.
Msimamo na mwendelezo ni muhimu ili tabia na utamaduni unaojenga uweze kuwa imara na kudumu.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe