3103; Msimamo pekee hautoshi.

Rafiki yangu mpendwa,
Tunajua umuhimu wa msimamo kwenye safari yetu ya mafanikio.
Hakuna kitu tunaweza kufanya mara moja au mara chache na kikatupa mafanikio makubwa.
Mafanikio makubwa yanatokana na kufanya kwa msimamo kwa muda mrefu bila kuacha.

Lakini msimamo peke yake hautoshi.
Kuwa na msimamo kwenye kitu ambacho siyo sahihi kunakupoteza zaidi.
Lakini pia kuwa na msimamo kwa kufanya kwa kiwango kile kile kunaendelea kukupa matokeo yale yale ambayo tayari unayapata.

Kwa matokeo yoyote unayoyapata, unapaswa kuzidisha juhudi unazoweka.
Pale unapoona siku zako zinafanana na matokeo unayoyapata ni yale yale, jua msimamo pekee hautoshi kukupa matokeo ya tofauti, hivyo unaanza kuwa kuongeza juhudi zako mara mbili zaidi.

Kuongeza juhudi unazoweka kunakusukuma kwenda kwenye kiwango kipya cha ufanyaji na kuwa kwenye nafasi ya kupata matokeo ya tofauti na uliyozoea kupata.

Sisi binadamu ni viumbe wa tabia, huwa tunapenda sana mazoea.
Ni muhimu sana kwenda kinyume na tabia na mazoea hayo ili kupata matokeo makubwa na ya tofauti.

Kupata matokeo ya aina moja kwa muda mrefu, hata kama ni makubwa ni jambo linalopaswa kukupa wasiwasi.
Usihadaike na ukubwa wa matokeo unayoyapata, kama matokeo hayo hayabadikiki na kuendelea kukua zaidi, upo kwenye hatari.

Haijalishi upo juu kiasi gani, matokeo unayoyapata yanatakiwa kuendelea kubadilika na kuwa makubwa zaidi kadiri muda unavyokwenda.
Hivyo unawajibika kila mara kujikagua juhudi unazoweka na matokeo unayoyapata.

Huwa kuna tofauti kati ya juhudi na matokeo, mara nyingi matokeo yanakuja baadaye sana baada ya hatua kuchukuliwa.
Kwenye hali kama hiyo, mara ngingi huwa ni vigumu kupima ufanisi wa hatua unazoweka.
Hapo ndipo unapohitaji kuwa na njia za kukuhakikishia juhudi unazoweka ni sahihi.

Kabla hujawa na msimamo wenye mwendelezo wa ukuaji kwenye eneo lolote lile la maisha yako, hakikisha kwanza ni eneo sahihi na juhudi zinazowekwa ndiyo sahihi kabisa.
Yaani unapaswa kuhakikisha unachofanya ndiyo sahihi kabla hujafikiria kuhusu kukiboresha zaidi kupitia kuongeza juhudi.

Mambo yote tuliyojadili hapa, yatawezekana kama tu unapima namba zako vizuri.
Bila ya kupima kwa namba za uhakika, ni rahisi mtu kuona mambo yanaenda vizuri, maana kuna matokeo yanayokuwa yakipatikana.
Lakini unapopima kwa namba, unaona wazi matokeo kwa uhalisia wake, na hapo ndipo unapojua mahali sahihi pa kuongeza juhudi.

Kwa yote unayoyafanya kwenye maisha yako, mara kwa mara ongeza zaidi juhudi unazoweka.
Ni kwenye juhudi ndipo penye nafasi kubwa ya kubadili matokeo unayokuwa unayapata.

Kila mara jikague kama juhudi unazoweka ni sahihi, kisha kuza zaidi juhudi hizi na matokeo unayoyapata yatabadilika.

Mafanikio yako yanategemea sana uwezo na uharaka wa kupima matokeo na juhudi zinazowekwa.
Unahitaji kuyapima matokeo yako kila mara ili uweze kuboresha juhudi unazoweka na kupata mafanikio makubwa zaidi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe