Barua ya IX; Kuhusu Falsafa Na Urafiki.

Rafiki yangu Mstoa,
Urafiki ni dhana ambayo imekuwepo tangu enzi na enzi, lakini ambayo imekuwa ngumu sana kuelezewa na kueleweka na watu.

Hata kwenye zama tunazoishi sasa, bado ni vigumu sana kwa watu kujua nani ni marafiki wa kweli na urafiki una mchango gani kwenye maisha.

Malalamiko ya watu yamekuwa ni mengi kwenye eneo la urafiki, hasa ile hali ya kusalitiana.
Watu wamekuwa hawaaminiki kama ambavyo mtu angependa kuwaamini.

Kushindwa kujua mchango na wajibu wa urafiki kwenye maisha, imekuwa chanzo cha watu kushindwa kujua jinsi ya kuwa na marafiki wazuri na hata kunufaika na urafiki.

Kwenye barua yake ya 9 aliyoandika kwa rafiki yake Lucilius, Seneca alifafanua kwa kina dhana ya urafiki kwa kutumia falsafa mbalimbali, ikiwepo ya Ustoa na falsafa ya Epicurus.

Mambo ya msingi ambayo Seneca anatutaka tuyajue kuhusu urafiki ili tuweze kuutumia kwa tija ni kama ifuatavyo.

1. Kila mtu anahitaji kuwa na marafiki.

Seneca anaanza kwa kufafanua falsafa ambayo imekuwa inanukuliwa vibaya kwamba mtu mwenye hekima anajitosheleza mwenyewe na hahiyaji watu wengine.
Anasema ni kweli mtu mwenye hekima anaweza kujitegemea, lakini hilo haliondoi hitaji la yeye kuwa na marafiki.

Seneca anafafanua kwamba mtu mwenye hekima anahitaji marafiki siyo kwa ajili ya kuwategemea, bali kama sehemu ya maisha yake.
Na kama ambavyo mtu huyo anahitaji macho, masikio, mikono na viungo vingine, ndivyo pia anavyohitaji marafiki.
Lakini pia, kama mtu mwenye hekima atapoteza jicho lake au mkono wake, hataona maisha yake yamekosa maana, badala yake ataendelea kutumia viungo alivyobaki navyo.
Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye urafiki, mtu mwenye hekima anawahitaji marafiki, lakini hata akiwakosa haiathiri maisha yake.

Hatua ya kuchukua;
Tambua kwamba unahitaji marafiki kwenye maisha yako, lakini siyo kwa ajili ya kuwategemea. Kama wasipokuwepo maisha yako yasivurugike. Weza kujitegemea kwa kila ulichonacho lakini tumia vya nje kama sehemu ya maisha.

Nukuu;
“In this sense the wise man is self-sufficient, that he can do without friends, not that he desires to do without them.” – Seneca
“Kwa maana hiyo, mtu mwenye hekima anajitosheleza mwenyewe, kwamba anaweza kwenda bila marafiki, lakini siyo anataka kutokuwa nao.” – Seneca

2. Njia ya haraka ya kupata marafiki.

Kama mtu anahitaji marafiki, lakini pia hapaswi kuwategemea, anawezaje kuwapata marafiki, hasa pale anapokuwa amepoteza wale aliokuwa nao?
Watu wengi huwa wanasema ni rahisi kujenga urafiki utotoni na ujanani, ila ni vigumu ukishakuwa mtu mzima.

Seneca anatupa njia rahisi na ya haraka ya kujenga urafiki.
Njia hiyo ni kuwapa watu kile unachotaka wakupe. Kama unataka watu wakupende, anza kwa kuwapenda. Kama unataka watu wakujali, anza kwa kuwajali.
Urafiki unakuwa mgumu kujenga pale mtu anapoangalia nini anapata badala ya kuangalia nini anatoa.

Hatua ya kuchukua;
Ili kujenga urafiki kwa haraka, wape watu kile ambacho unataka wakupe.
Anza kutoa kabla ya kupokea na hilo litawafanya watu wapende kuwa karibu na wewe.

Nukuu;
“If you ask how one can make oneself a friend quickly, I will tell you, Hecato, says: ‘If you would be loved, love.'” – Seneca.
“Kama unauliza mtu anawezaje kujenga urafiki kwa haraka, nitakuambia, Hecato anasema: ‘Kama unataka kupendwa, penda.'” – Seneca

3. Mazoea huwa yanaua urafiki.

Kitu kinachowakatisha tamaa wengi kwenye urafiki ni pale unapokufa baada ya watu kuwa wameweka juhudi kubwa na muda mrefu kwenye kuujenga.
Seneca anaeleza urafiki mwingi huwa unakufa kutokana na mazoea.
Seneca anaeleza kwamba watu huwa wanakipa kitu umakini mkubwa wakati wa kukitengeneza, lakini kikishakamilika hawakipi tena umakini mkubwa.
Anatoa mfano wa mkulima wakati wa kupanda na kupalilia anavyoweka umakini mkubwa kwenye mazao kuliko akiwa ameshayavuna.
Kadhalika mchoraji anaweka umakini kwenye kazi anayochora, akishaikamilisha anaiweka pembeni.
Na hata kwa wazazi, kumbukumbu nzuri za watoto wao ni wakati walipokuwa wadogo na kuhitaji umakini wao mkubwa, siyo baada ya kuwa wakubwa na kujitegemea.

Hatua ya kuchukua;
Ili urafiki uweze kudumu kwa muda mrefu, kila wakati upe umakini na kuendelea kuujenga. Usichukulie urafiki kama kazi ambayo imeshakamilika, kwani utaleta mazoea na mazoea yataua urafiki huo.
Na hii ni kwenye mahusiano yako yote kwenye maisha, endelea kuyawekea juhudi na epuka kuruhusu mazoea.

Nukuu;
“When one is busy and absorbed in one’s work, the very absorption affords great delight; but when one has withdrawn one’s hand from the completed masterpiece, the pleasure is not so keen.” – Seneca
“Mtu anapokuwa ametingwa na kazi, huwa inampa raha, lakini akishaikamilisha na kuiweka pembeni, haimpi tena raha.”

4. Urafiki siyo nipe nikupe.

Tumeona kwenye namba 2 hapo juu kwamba njia rahisi ya kujenga urafiki ni kuwapa watu kile ambacho unataka wakupe.
Seneca anatupa tahadhari kubwa hapa, kama tutajenga urafiki kwa sababu ya vitu ambavyo tunategemea kuvipata kwa hao marafiki, urafiki huo hautaweza kudumu.
Pale unapojenga urafiki na mtu ambaye unategemea akupe kitu fulani, urafiki huo utaisha pale atakaposhindwa kukupa ulichotegemea kwake.
Kadhalika wale wanaojenga urafiki na wewe ili kupata vitu fulani, wakivikosa urafiki unaishia hapo.
Wakati mwingine hata watu wakipata kile walichotaka kwenye urafiki, bado urafiki huo utavunjika, pale mtu atakapokuwa hana uhitaji tena.

Seneca anauita urafiki wa aina hiyo urafiki wa majira mazuri, kwani baada ya majira hayo kupita urafiki huo hufa.
Anaeleza pia ndiyo sababu kwa nini watu waliofanikiwa wana marafiki wengi, wakati walioshindwa wako na upweke.
Ni kwa sababu wengi kwenye urafiki wanaangalia wanapata nini, na huo siyo urafiki wa kweli ambao utadumu.

Hatua ya kuchukua;
Usiingie kwenye urafiki kwa kuangalia unakwenda kupata nini, kwani hicho ndiyo kitakachoua urafiki, iwe umekipata au hujakipata.
Lakini pia jitahadhari na wale wanaojenga urafiki na wewe kwa maslahi yao binafsi, hakuna namna utaweza kukaa nao kwenye urafiki kwa muda mrefu.

Nukuu;
“He who begins to be your friend because it pays will also cease because it pays.” – Seneca
“Yule anayeanza kuwa rafiki yako kwa sababu ya maslahi yake binafsi, ataacha pia kuwa rafiki yako kwa sababu ya maslahi yake binafsi.” – Seneca

5. Mahitaji ya msingi na matakwa ya anasa.

Katika kuelezea jinsi ambavyo watu wenye hekima wanaweza kujitosheleza na kutokutegemea wengine, Seneca anagusia eneo la mahitaji ya msingi (needs) na matakwa ya anasa (wants).
Anaeleza mtu mwenye hekima ana mahitaji mengi ya msingi, lakini hana matakwa yoyote ya anasa.
Na kwa upande wa pili, mpumbavu hana mahitaji ya msingi, kwa sababu hajui jinsi ya kuyatumia, ila ana matakwa mengi ya anasa.

Hapa kuna ujumbe mkubwa sana ambao tukiuelewa utatupa uhuru mkubwa.
Ukikazana na mahitaji ya msingi kwenye maisha yako, ambayo huwa siyo mengi, unakuwa na utulivu na pia utaweza kujenga marafiki sahihi na kudumu nao kwa muda mrefu.
Lakini kama utaendeshwa na matakwa ya anasa, hayo huwa hayana ukomo, hivyo kila wakati utakuwa unataka zaidi, utatafuta watu wa kutimiza matakwa yako na hilo litaathiri mahusiano yako.

Hatua ya kuchukua;
Yajue mahitaji ya msingi kwako na uyape hayo uzito, ili uweze kujenga maisha tulivu na ya kujitosheleza.
Achana na matakwa ya anasa kwani hayo yatakufanya uwe tegemezi kwa watu wengine na kushindwa kuwa na utulivu na kujitosheleza.

Nukuu;
“The wise man is in want of nothing, and yet needs many things. On the other hand, nothing is needed by the fool, for he does not understand how to use anything, but he is in want of everything.” – Seneca
“Mtu mwenye hekima hana matakwa yoyote ya anasa, ila ana mahitaji ya msingi mengi. Kwa upande mwingine, mpumbavu hana mahitaji yoyote ya msingi, kwa sababu hajui jinsi ya kuyatumia, ila ana matakwa ya anasa mengi.” – Seneca

Rafiki yangu katika Falsafa hii ya maisha ya Ustoa, tumejifunza hapa mambo ya msingi sana kuhusu kujenga urafiki kifalsafa.
Na ujumbe mkuu kabisa ni tuwe watu wenye hekima, tujitosheleze na kujitegemea kwa kuwa na mahitaji ya msingi na kuepuka matakwa ya anasa.
Ni kupitia utulivu huo ndiyo tutaweza kujenga urafiki mzuri na utakaodumu kwa muda mrefu na kuwa na manufaa kwa wote.

Kutoka kwa Mstoa mwenzako,
Kocha Dr Makirita Amani.