#WekaKazi: Kobe Bryant; Kuamka saa tisa kila siku kulivyompa mafanikio makubwa.
Kobe Bean Bryant (Kuzaliwa Agosti 23, 1978, kufariki Januari 26, 2020) alikuwa mchezaji mpira wa kikapu wa nchini Marekani aliyepata mafanikio makubwa sana.
Kwa miaka 20 aliyokuwa mchezaji, alichezea timu ya Los Angeles Lakers kwenye ligi kuu ya kikapu nchini Marekani (NBA).
Kwenye kipindi ambacho alikuwa mchezaji, alipata mafanikio makubwa sana, ikiwepo;
1. Kushinda mataji matano ya ligi kuu.
2. Kuwa mchezaji bora mara 18.
3. Kuchaguliwa mara 16 kwenue timu bora ya ligi.
4. Kuchaguliwa mara 12 kwenye timu ya walinzi.
5. Kuwa mchezaji aliyelipwa zaidi mwaka 2008
6. Kufika fainali za wachezaji wanaolipwa zaidi mara mbili.
7. Kuwa mfungaji bora mara mbili.
8. Kushika nafasi ya nne ya wafungaji wa nyakati zote.
9. Kupata tuzo ya heshima ya Naismith Memorial Basketball Hall of Fame mwaka 2020.
10. Kutajwa kwenye timu ya kumbukizi ya 75 ya ligi ya NBA mwaka 2021.
Unaweza kujiuliza mtu mmoja anaweza kupataje mafanikio yote hayo ndani ya miaka 20 tangu kuingia kwenye mpira wa kikapu mpaka kustaafu?
Hakuna siri, kwani Kobe alikuwa akieleza wazi kwamba alikuwa AKIWEKA KAZI kuliko wachezaji wengine wote ambao wamewahi kutokea.
Kobe alifanya mazoezi kila siku bila kuacha, akianza mapema na kuchelewa kumaliza.
Hakuwa na kitu kingine chochote alichokuwa anafikiria zaidi ya mpira wa kikapu.
Na kuweka kwake kazi hakujamtupa, bali kumempa mafanikio ambayo hakuna wachezaji wengine ambao wameweza kuyapata yote kwa pamoja.

Kuna mengi ambayo Kobe anatufundisha kuhusu mafanikio na kazi, baadhi ni kama ifuatavyo;
1. Usikubali mtu yeyote akuzidi kwenye kazi.
Mchezaji Jay Williams timu yake ilikuwa inaenda kushindana na timu ya Kobe. Kwa kujua ufanyaji mazoezi wa Kobe, aliamua kwamba atawahi kufanya mazoezi kuliko wachezaji wengine wote.
Alipofika uwanjani, alimkuta Kobe tayari yupo na ameshalowa jasho.
Alionekana kuwa pale kwa zaidi ya saa nzima. Jay alifanya mazoezi kwa nusu saa na kuondoka, akimwacha Kobe anaendelea.
Timu ya Kobe ilishinda mchezo siku hiyo na Kobe alipata alama 40 yeye peke yake.
Mchezo ulipoisha, Jay alimfuata Kobe na kumwuliza kwa nini anafanya mazoezi kwa juhudi sana?
Kobe akamjibu; “Kwa sababu nilikuona ukija na nikataka kukuonyesha kwamba haijalishi unafanya kazi kwa juhudi kiasi gani, nipo tayari kufanya kazi zaidi yako.”
Unaweza kuona hapo ni kwa kiasi gani Kobe alikuwa amejitoa kweli kweli kuhakikisha hakuna mtu yeyote anayemshinda kwenye kazi.
2. Mara zote alikuwa wa kwanza kufika kwenye mazoezi na wa mwisho kuondoka.
Wakati ratiba ya kufanya mazoezi ilikuwa inaanza saa moja asubuhi, Kobe alifika uwanjani saa kumi na moja alfajiri.
Na hata baada ya muda wa mazoezi kuisha, Kobe alibaki uwanjani akiendelea na mazoezi peke yake.
Wakati mwingine alifanya mazoezi kwenye giza, akijifunza kulenga kikapu bila hata ya kukiona.
Wakati wa mashindano ya Olympics ya mwaka 2008, Chris Bosh na Dwayne Wade wanaelezea kitu cha ajabu walichokiona kwa Kobe ambacho hawajawahi kukiona kwa wachezaji wengine.
Bosh anaeleza; “Tulikuwa Las Vegas na tulikuwa tunaenda kupata kifungua kinywa na timu, tunamwona Kobe anakuja akiwa anatokwa jasho na akiwa na barafu kwenye magoti. Nikajiuliza, ni saa mbili asubuhi, anatoka wapi muda huu?”
Wade akaendelea; “Kila mtu ndiyo alikuwa ameamka, wote tulikuwa tunapiga miayo, lakini Kobe tayari alikuwa ameshafanya mazoezi kwa masaa matatu.”
Kuwa tayari kuwahi kwenye mazoezi kabla ya wengine kulipa fursa ya kuwa mbele ya wengine kwenye upande wa mazoezi.
3. Alifanya mazoezi mara 4 kwa siku, wakati wengine walifanya mara mbili.
Kobe alipangilia siku yake kwa namna ambayo alipata muda mwingi wa kufanya mazoezi kuliko wachezaji wengine wote.
Hapa anaelezea jinsi anavyoipangilia siku yake;
“Kama kazi yako ni kuwa mchezaji bora kabisa duniani, ni lazima ufanye mazoezi. Kama utaamka saa 4 asubuhi na kufanya mazoezi kwa masaa mawili, yaani saa 6 mpaka saa 8 mchana, unahitaji muda wa kupumzika ili mwili upoe. Utaweza tena kufanya mazoezi saa 12 jioni mpaka saa 2 usiku. Hapo unakuwa umefanya mazoezi mara mbili kwa siku. Sasa fikiria ukiamka saa 9 usiku na kufanya mazoezi saa 10 mpaka saa 12 asubuhi, ukaenda kupumzika, ukarudi tena saa 3 mpaka saa 5 asubuhi, halafu tena saa 8 mpaka saa 10 jioni, kisha kumalizia saa 1 mpaka saa 3 usiku. Hapo unakuwa umefanya mazoezi mara 4 kwa siku. Kama utafanya hivyo kila siku kwa miaka mingi bila kuacha, utawaacha wengine nyuma sana. Unapokuwa umefika mwaka wa 5 au wa 6 kwa utaratibu huo, hakuna mwingine atakayeweza kukufikia na utakuwa bora kabisa duniani. Huwa naianza siku yangu mapema kwa sababu nataka kufanya kazi zaidi.
Anaongeza kusema; “Naweza kufanya mazoezi kwa masaa mengi, na najua wengine hawawezi kufanya hivyo, kwa sababu najua ratiba zao. Hii ndiyo sababu naweza kustaafu na kuwa na amani kwa sababu najua nimefanya kila nilichopaswa kufanya ili kuwa mchezaji bora kabisa.”
Juhudi kubwa kwenye kazi na muda wa kutosha kwenye kazi ni vitu ambavyo havikwepeki kama unataka kupata mafanikio makubwa.
4. Kuridhika kwake kulitokana na kujisukuma zaidi kila siku ili kufikia uwezo wake kamili.
Akiongea wakati wa sherehe yake ya kustaafu, akieleza nini kinamsukuma kuwa bora, alisema; “Ni kwenye zile siku ambazo umeamka mapema na kufanya kazi kwa juhudi, siku ambazo umechelewa kulala na kufanya kazi. Nyakati ambazo hujisisikii kufanya kazi, umechoka sana, hutaki kujisukuma, lakini inabidi tu ufanye. Hiyo ndiyo ndoto yenyewe.”
Ndoto kubwa ya Kobe ilikuwa ni safari yake ya kuwa bora na kufanya kazi kwa juhudi ndiyo gharama aliyochagua kulipa ili kufikia lengo.
Kwa kumalizia kuna kisa cha Kocha mmoja ambaye anaelezea siku aliyofanya kazi na Kobe na kushangazwa sana na ufanyaji wake wa kazi kwa kujituma.
Kocha huyo aliyeitwa Rob, aliungana na timu ya Kobe wakati wanaelekea kwenye mashindano.
Siku moja kabla ya kuanza mazoezi makali, aliongea na Kobe na kumpa namba yake, akimwambia kama atahitaji msaada wakati wa mazoezi anaweza kumpigia.
Kocha huyo aliachana na Kobe, ilikuwa ni usiku na akaenda chumbani kwake. Aliangalia tatmthilia mpaka saa tisa usiku ndiyo akaamua alale. Kabla hajapata usingizi, simu ikaita, kuangalia ni Kobe, ilikuwa saa 10 na robo alfajiri. Alipokea simu na maongezi yakawa hivi;
Kobe; “Hey Rob, natumaini sitakuwa nakusumbua muda huu.”
Rob; “Hapana, kuna shida yoyote?”
Kobe; “Nilikuwa najiuliza kama unaweza kunisaidia baadhi ya mazoezi, ni hilo tu.”
Rob; “Sawa, nakuja muda siyo mrefu.”
Rob anasema ilimchukua dakika 20 kufika uwanjani na kumkuta Kobe aliwa peke yake na amelowa jasho kama mtu aliyetoka kuogelea, na hapo ilikuwa haijafika hata saa 11 alfajiri.
Rob alimsaidia Kobe baadhi ya mazoezi kwa muda wa saa moja na robo, kisha kwenda kwenye mazoezi mengine kwa dakika 45. Baada ya hapo Rob aliondoka na kumwacha Kobe uwanjani akimalizia mazoezi.
Rob alirudi chumbani kwake akiwa amechoka kwa usingizi na kulala usingizi mzito. Alitakiwa kurudi tena kwenye mazoezi saa tano asubuhi, hivyo alipoamka muda huo alikuwa bado ana uchovu na usingizi mkali.
Alifika kwenye uwanja wa mazoezi na kumkuta Kobe akifanya mazoezi ya kurusha mpira peke yake, wakati wachezaji wengine bado wanajipanga.
Rob alimfuata Kobe na kumgusa mgongoni na kumwambia;
Rob; “Hongera kwa kazi nzuri ya mazoezi asubuhi ya leo.”
Kobe; “Asante sana, nathamini mchango wako.”
Rob; “Kwa hiyo umemaliza saa ngapi?”
Kobe; “Kumaliza nini?”
Rob; “Kumaliza mazoezi na kuondoka uwanjani.”
Kobe; “Sijaondoka tangu umeniacha, nilipanga kurusha mpira mara 800 ndiyo nimemaliza sasa.”
Rob hakuamini alichokisikia, alishangazwa na jinsi Kobe alivyojitoa kwenye kazi na alijionea mwenyewe kwa nini alikuwa na mafanikio makubwa kuliko wachezaji wengine wote.
Rob anamalizia kwa kusema alikuwa akisikia nukuu ya Kobe anasema; “Sitaki kuwa Michael Jordan, bali nataka kuwa Kobe Bryant.”
Na kweli aliyoyokuwa anayafanya yalikuwa ya kipekee kabisa kwake, hakuna mchezaji mwingine aliyeweza kuyafanya.
Rafiki yangu mpendwa, tumejionea wenyewe hapo, mafanikio makubwa hayaji kama bahati au ajali, yanatengenezwa na yanatengenezwa kwa gharama kubwa sana.
Kuwa tayari kulipa gharama kubwa kwenye Kuweka Kazi ili uweze kupata mafanikio yoyote makubwa unayoyataka.
Rafiki yangu mpendwa,
Kama umeipenda na kujifunza kupitia makala hii, nina habari njema sana kwako.
Kitabu cha UNA NGUVU YA KUTENDA MIUJIZA kinakuonyesha jinsi ambavyo ndani yako tayari una nguvu ya kufanya makubwa zaidi ya unavyofanya sasa.
Kama ambavyo umemuona Kobe akiweza kufanya makubwa, hata wewe pia unaweza.
Ni kujitambua nguvu zako zilipo na kuweza kuzitumia vizuri.
Pata leo na usome kitabu hiki ili ujifunze na uweze kuchukua hatua kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi.
Kupata nakala yako ya kitabu wasiliana na namba 0752 977 170 sasa.
Usikubali kubaki hapo ulipo sasa, pata kitabu, soma na chukua hatua ili uyaboreshe maisha yako zaidi.
Rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Muuza Matumaini,
Bilionea Mafunzoni,
Mwanafalsafa ya Ustoa,
Mkuu wa Chuo Cha Mauzo,
Kocha Dr. Makirita Amani
amakirita@gmail.com
http://www.amkamtanzania.com / http://www.t.me/amkamtanzania
http://www.utajiri.tz / http://www.t.me/utajiritz
http://www.mauzo.tz / http://www.t.me/chuochamauzo
Tru kocha
LikeLiked by 1 person
Karibu na weka kazi.
LikeLike