3112; Anzia mahali.

Rafiki yangu mpendwa,
Kama utasubiri mpaka taa zote za barabarani ziwake kijani ndiyo utoke, kamwe hutatoka nyumbani.
Unachopaswa kufanya ni kutoka kisha kufuata taa moja moja kadiri inavyoelekeza, iliyo kijani unapita, nyekundu unasubiri iwake kijani.
Lakini hapo unakuwa kwenye mwendo na hivyo inakuwa rahisi kuendelea kuliko ukiwa hujaanza kabisa.

Kwa chochote unachotaka kufanya kwenye maisha yako, anzia mahali popote, kisha nenda ukiboresha kadiri unavyoendelea kufanya.
Ni bora ufanye kwa kukosea kuliko kutokufanya kabisa.
Maana ni rahisi kusahihisha makosa ukiwa tayari unafanya kuliko ukiwa hujaanza kufanya kabisa.
Huwezi kuboresha kitu ambacho hakipo, hivyo bora kuanza kisha kuboresha kadiri unavyokwenda.

Hapaswi kujali watu wengine wanakuchukuliaje kwenye kile ulichoamua kufanya.
Hupaswi kuhofia kwamba watakudharau kwa kuwa umeanzia chini au umekosea.
Jikumbushe hakuna anayejali kuhusu maisha yako zaidi yako mwenyewe.
Hakuna anayeenda kukosa usingizi usiku kwa sababu ya maisha yako.
Hayo ni matatizo yako mwenyewe, ambayo inabidi upambane nayo mwenyewe.
Wale unaofikiria watakuchukuliaje, maisha yako siyo kipaumbele kikubwa kwao kama unavyodhani.
Wananyimwa zaidi usingizi na mambo yao binafsi kuliko mambo yako.

Usitake ukamilifu ndiyo uweze kuanza, hakuna kilichokamilika kwenye maisha.
Kila barabara ina kona na hata kupanda na kushuka.
Ukisubiri mpaka upate njia iliyonyooka moja kwa moja, kamwe hutoanza.
Hupaswi kusubiri mpaka uweze kuona njia nzima mpaka mwisho wa safari.
Unachohitaji ni kuona hatua inayotuata kisha kufanyia kazi hiyo.
Kadiri unavyokwenda, hatua zaidi za kufuata zitajitokeza mbele yako.
Kwa kuanza, kuna mengi mazuri ya kuendelea utakayokutana nayo.

Kadiri unavyohofia kufanya kitu, ndivyo unavyopaswa kujisukuma kukifanya.
Maana pale penye hofu kubwa, ndipo pia penye fursa ya wewe kufanya makubwa zaidi.
Hofu ni kiashiria kizuri cha nini sahihi kwako kufanya.
Kama hupati hofu kwenye kufanya kitu fulani, pata wasiwasi, kitakuwa ni cha kawaida sana, ambacho hakitakupa mafanikio.
Hofu ni kiashiria kwamba unatoka nje ya mazoea yako, kitu ambacho ni kizuri.

Kushindwa pia ni kuzuri, anzia popote na ushindwe, kwani utajifunza mengi sana kupitia kushindwa kuliko unavyojifunza kupitia kufanikiwa.
Kushindwa ni kiashiria kwamba umefanya kitu nje ya mazoea yako, ambayo ni ishara ya ukuaji.
Kushindwa kunakuonyesha ni maeneo gani ambayo bado hujawa vizuri kama unavyopaswa kuwa.
Kama kushindwi, haimaanishi kwamba wewe ni bora sana.
Bali inamaanisha unafanya mambo ya kawaida sana, ambayo pia hayawezi kukupa mafanikio makubwa.
Mafanikio makubwa yanaambatana na kushindwa mara nyingi pia.
Wale waliofanikiwa sana, wanakuwa pia wameshindwa zaidi kuliko wale walioshindwa.

Nimeshakushawishi vya kutosha uanzie popote, pale ulipo sasa na uendelee kuboresha kuliko uendelee kusubiri, au bado?
Kama tayari anza kufanya sasa hivi, siyo kesho, siyo leo, bali sasa hivi.
Anza mara moja na kamwe usiache. Ukishaanza kufanya endelea kufanya kwa kuboresha na kusonga mbele kwa kuboresha zaidi. Kamwe usikubali kusimama au kuacha.

Kama bado sijakushawishi, nina silaha moja ya mwisho kwenye kutetea hoja hii.
Silaha hiyo ni KIFO.
Kumbuka utakufa.
Kila siku inayopita ni siku unayokikaribia kifo chako.
Ni siku ambayo hutakuja kuipata tena kwenye maisha yako.
Kadiri siku zinavyokwenda, ndivyo unavyozidi kupunguza muda wako hapa duniani.
Kama hutaanza kufanya mara moja, hakuna kinachokuwa bora, zaidi ya kuzidi kupunguza muda wako.
Kumbuka pia ukifa, sababu unazojipa sasa utakufa nazo.
Hakuna sababu yoyote unayojipa ambayo itabaki kama alama.
Lakini chochote utakachokuwa umefanya, kitabaki kama alama baada ya kifo chako.
Kifo kikukumbushe kuchukua hatua sasa kuliko kuendelea kusubiri.

Rafiki, anzia popote ulipo, anzia hapo ulipo sasa.
Ni kuanza ndipo kutafungua milango mingi zaidi kwako.
Fanya, fanya, fanya.
Hakuna namna nyingine.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe