3115; Kufanya na matokeo.

Rafiki yangu mpendwa,
Tumejifunza na kuzoea kwamba tunapofanya kitu, tunaona matokeo mara moja.
Hivyo inapotokea tumefanya kitu na hatuoni matokeo, basi tunaona tulichofanya siyo sahihi na hivyo tunaacha kukifanya.

Hayo ni mazoea mabaya ambayo tumejijengea na ambayo ni kikwazo kwetu kupata mafanikio makubwa.

Ukweli muhimu unaopaswa kuujua kuhusu mafanikio ni kwamba yanatokana na kufanya.
Na kila ufanyaji huwa unazalisha matokeo yake, ni vile tu matokeo huwa hayafanani.
Hakuna ufanyaji ambao huwa unaenda bure.

Kufanya ambako kunazalisha matokeo huwa kuna sifa tatu ambazo ni kama ifuatavyo;
Kufanya kwa ukubwa,
Kufanya kwa muda mrefu,
Na kufanya kwa msimamo bila kuacha.

Tofauti kati ya wanaoshinda na wanaoshindwa kwenye maisha huwa inaanzia mahali pamoja tu, ambapo ni ufanyaji.
Wanaoshinda wanazingatia ufanyaji kwa sifa zote tatu.
Wanaoshindwa huwa wanaacha kufanya kitu mapema kama hawaoni matokeo.

Kama huridhishwi na matokeo unayoyapata sasa, mahali pa kuanzia ni kwenye ufanyaji.
Hapo ndipo mkwamo mkubwa unapokuwa umeanzia.
Huenda hujafanya kwa ukubwa ambao unahitajika, kwa muda mrefu inavyohitajika na kwa msimamo bila kuacha.

Hakuna namna unaweza kutenganisha ufanyaji na matokeo, hata ufanye nini.
Watu wamekuwa wanakimbizana na njia za mkato tangu enzi na enzi, lakini haijawahi kupatikana njia ya uhakika ya mafanikio ambayo haihusishi kufanya.

Watu wamekuwa wanatumia muda mrefu kuahirisha kufanya yale wanayojua wanapaswa kuyafanya.
Muda wanaokuwa wameahirisha, hakuna chochote cha maana wanakuwa wanafanya, bali kuupoteza kwa mambo yasiyokuwa na tija.
Halafu wanashangaa kwa nini hawafanikiwi.

Halafu kuna wale ambao muda wote wametingwa.
Wapo ‘bize’ kweli kweli.
Wanamaliza siku zao wakiwa wamechoka sana.
Lakini wakiangalia, hakuna hatua wanazopiga.
Hawa wakisikia unawaambia hakuna kitu wanafanya, wanaona kama unawadhihaki.
Lakini ukweli unabaki pale pale, wanakuwa wameshindwa kufanya kwa usahihi.
Wanakosa vipaumbele, hivyo wanahangaika kufanya vitu ambavyo havina tija kabisa.

Kwa kila mafanikio unayokuwa unayataka, kuna vitu unapaswa kuvifanya ili kuyapata.
Ni muhimu sana ujipime kwenye ufanyaji wa vitu hivyo kama unataka kupata mafanikio makubwa.

Kama hujapata mafanikio unayoyataka, tatizo ni hujafanya kile unachopaswa kufanya ili ufanikiwe.
Na kama umefanya, basi siyo kwa ukubwa, muda na msimamo unaohitajika.
Kitu chochote sahihi unachofanya, ukakifanya kwa ukubwa, kwa muda mrefu na kwa msimamo bila kuacha, lazima kitakupa matokeo makubwa.

Jua kinachopaswa kufanyika na kifanye.
Usitafute njia za mkato.
Usiahirishe kufanya.
Usikate tamaa kwa kuona matokeo hayaji.
Usiridhike kwa matokeo madogo unayopata kwa haraka.
Kaa kwenye ufanyaji sahihi na utaweza kupata matokeo makubwa unayoyataka na yanayokupa mafanikio unayoyataka.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe