3118; Watu wengi wanataka ufanikiwe, mpaka utakapofanikiwa.

Rafiki yangu mpendwa,
Unapokuwa na malengo ya mafanikio makubwa, huwa unapata uungwaji mkono na watu walio wengi kwenye maisha yako.
Unaposhirikisha malengo na mipango mikubwa unayokuwa nayo, wengi wanafurahia kwa sababu unakuwa unawafanya wakumbuke malengo makubwa ambayo walikuwa nayo pia.
Watakutia sana moyo kwamba upambane na majibu mazuri yatakuja.

Unapambana kweli na unafanikiwa kwenye yale uliyopanga kufikia.
Ulitegemea wale waliokuwa wanakusifia wawe ndiyo wa kwanza kwanza kufurahia mafanikio yako.
Lakini kinachotokea kinakuwa ni kinyume kabisa na matarajio yako.
Watu walioonekana kukuunga mkono wakati unaanza, wanageuka na kuwa maadui wako wakubwa baada ya kufanikiwa.

Kuna sababu mbili zinazopelekea mafanikio yako kuwa chanzo cha wale waliokuwa wanakuunga mkono mwanzoni kubadilika na kuwa maadui wako.

Moja ni mafanikio yako yanaonyesha uzembe wao.
Kwa wewe kufanikiwa, kunawafanya wengine waonekane ni wazembe.
Hasa pale unapokuwa umeanzia chini kabisa na kufanikiwa, unawafanya wengine waonekane ni wazembe, wameshindwaje na wao kufanikiwa?
Kwa sababu hakuna anayependa kuonekana ni mzembe, inapelekea uchukiwe na wale wasiofanikiwa.

Mbili ni kukosa udhibiti kwako.
Watu wengi huwa wanapenda kuwa na udhibiti kwa watu wengine, kuwapangia nini cha kufanya, kwa namna gani na wakati gani.
Kadiri unavyofanikiwa ndivyo unavyozidi kuwapuuza watu na kuhangaika zaidi na mambo yako.
Hilo linafanya watu waone una kiburi na dharau, kwa sababu hawana tena udhibiti kwako.

Unachopaswa kufanya ni kuwapuuza wote wenye chuki na wewe.
Unapaswa kuendelea kuyapambania mafanikio makubwa zaidi unayoyataka.
Wale walioshindwa hawapaswi kuwa kikwazo kwako, badala yake wafanye kuwa kichocheo kwako kufanikiwa zaidi.

Wanaokuchukia kwa sababu ya mafanikio yako usiwachukie, bali waonee huruma.
Waonee huruma jinsi maisha yao yalivyo magumu kwa kuendeshwa na chuki.
Fikiria mtu anayeamka asubuhi na matumizi bora ya muda wa siku yake nzima ni kuwa na chuki kwa wengine.
Kwa hakika anakuwa na maisha magumu mno, huku akiwa hana anachovuna.

Wewe endelea kuweka umakini wako wote kwenye kujenga mafanikio makubwa zaidi kwako.
Uzembe uliowazuia wengine kufanikiwa haupaswi hata kupata nafasi kwako.
Mara zote baki ukiwa na udhibiti mkubwa sana kwako binafsi ili uwe huru kufanya kile unachotaka kufanya.
Hulazimiki kufanya yale wengine wanakutaka ufanye ili tu kuwaridhisha.
Nini maana ya wewe kujitesa na kupambana kufanikiwa kama utawaruhusu wakudhibiti vile wanavyotaka wao wenyewe?

Kwenye maisha yako, huwajibiki kukaa chini ya udhibiti wa kundi kubwa la ambao hawajafanikiwa.
Huhitaji hata kuwapa nafasi ya kukusumbua.
Unapaswa kuwapuuza kabisa.
Na hata wakikuambia mafanikio yamekupa kiburi na bila kuwasikiliza wao utaanguka, wacheke kabisa.
Maana kama ushauri wao ungekuwa unafanya kazi vizuri, kwa nini hawajautumia wao wenyewe kupata mafanikio makubwa?

Watu huwa wanapenda kujipa umaarufu na umuhimu wasiokuwa nao.
Wewe ni kuwapuuza tu na kuendelea na safari yako ya mafanikio makubwa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe