3119; Watu, matatizo, biashara, fedha.

Rafiki yangu mpendwa,
Hii dunia ina watu,
Watu hao wana matatizo mbalimbali.
Biashara zenye mafanikio huwa zinajengwa kwenye msingi wa kutatua matatizo ambayo watu wanayo.
Na fedha nyingi inaweza kutengenezwa kupitia biashara inayotatua matatizo ya watu.

Hayo maelezo hapo juu yamebeba kila kitu ambacho mtu anapaswa kukijua ili kujenga biashara yenye mafanikio makubwa.
Lakini watu huwa wanapenda kufanya mambo kuwa magumu na hilo linapelekea wapoteze muda na nguvu kwenye mambo yasiyokuwa na tija yoyote.

Ukiingia kwenye biashara kwa ajili ya kutatua matatizo ambayo watu wanayo, utaweza kutengeneza fedha kwa ukubwa na wingi.
Lakini ukiingia kwenye biashara kwa ajili ya kupata fedha, utaishia kuwa na matatizo.
Hii ni kanuni ambayo inafanya kazi kwa mafanikio makubwa mara zote.
Kama unataka kujenga biashara yenye mafanikio, anza na matatizo ambayo tayari watu wanayo.

Kila mara iangalie biashara yako kwenye mtiririko huu;
Anza na watu, dunia haitakosa watu.
Nenda kwenye matatizo ambayo tayari wanayo, kadiri matatizo yanavyokuwa makubwa, ndivyo manufaa yanavyokuwa makubwa pia.
Jenga biashara kwenye misingi ya kutatua matatizo ya watu uliyochagua kuyatatua. Asiwepo mwingine anayeweza kutatua matatizo uliyoyalenga kama wewe.
Kuwa na usimamizi mzuri wa mzunguko wa fedha kwenye biashara yako ili kupata mafanikio unayoyataka.

Usizidishe ugumu wa maisha yako kwa kuhangaika na vitu ambavyo huna uhakika navyo.
Rahisisha mchakato wako mzima wa kujenga biashara yenye mafanikio makubwa na fanyia kazi mchakato wako kwa msimamo bila kuacha.

Kama tayari ulishaanza biashara bila ya kuzingatia hii misingi uliyojifunza hapa, bado hujachelewa, anza sasa kufanya hivyo.

Biashara inaweza kukupa kiasi chochote cha fedha unachotaka, kama itajengwa kwenye msingi wa kutatua matatizo makubwa ambayo watu wengi wanayo.
Tuzingatie hilo kwa umakini mkubwa sana na tutaweza kufanya biashara kwa mafanikio makubwa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe