3124; 1, 10, 100, 1,000 na kuendelea.

Rafiki yangu mpendwa,
Mafanikio yoyote unayoyataka kwenye maisha yako, ni muhimu ukawa na namba za kuyapima.
Hiyo ni kwa sababu kitu chochote kile ambacho hakipimwi, hakiwezi kuboreshwa wala kukuzwa.

Pamoja na umuhimu huo mkubwa wa namba na kupima, bado watu wengi sana hawana namba wanazojipima nazo, kitu kinachokuwa kikwazo kikubwa kwao kupata mafanikio wanayokuwa wanayataka.

Hapa kuna namba rahisi sana ambazo nataka uanze kujipima nazo ili kuweza kupata mafanikio makubwa unayoyataka, kupitia biashara unayofanya.

Anza kwa kufikiria mteja mmoja anayekufurahisha sana kwenye biashara yako. Mteja ambaye unatamani wengine wote wangekuwa kama yeye.
Huyo ni mteja anayeielewa thamani unayoitoa, analipia kwa ukamilifu na kwa wakati, anarudi kununua mara kwa mara na kwa wingi na anawaleta wateja wengine wengi kwenye biashara.

Kisha jiulize kama ungekuwa na wateja wa aina hiyo 10 ni manufaa kiasi gani ungeyapata kwenye biashara yako?
Vipi ukiwa nao 100, au1,000 na kuendelea?
Kokotoa manufaa ya kuwa na wateja hao wazuri 10, 100, 1,000 na kuendelea.
Kwa kila namba utakuwa unajionea jinsi ambavyo manufaa ni makubwa.

Ukiwa na wateja bora 10, unaondoa kabisa wasiwasi wa iwapo mmoja akiondoka itakuwaje. Unapokuwa na mmoja pekee, kila mara unahofia kuondoka kwake. Lakini wanapokuwa 10, hata kama hupati faida kubwa, unakuwa huna wasiwasi mkubwa.

Ukiwa na wateja bora 100, biashara yako inakuwa inaweza kujiendesha vizuri kabisa na kwa faida. Wateja bora 100 ni idadi nzuri ya kukuwezesha kuendesha biashara yako vile unavyotaka wewe, huku ukiyafurahia maisha yako.
Idadi ya 100 unaweza kuihudumia vizuri na kwa upekee mkubwa kitu ambacho unaweza kuwabakisha kwenye biashara yako kwa muda mrefu.
Ukiweza kutengeneza wateja bora 100 na ambao ni mashabiki wa kweli wa biashara yako, unakuwa umejitengenezea uhakika kwenye biashara yako.

Ukiwa na wateja bora 1,000 na kuendelea, unakuwa umejihakikishia kupata mafanikio makubwa sana unayotaka kuyapata. Kwa namba hiyo ya elfu moja, hakuna chochote ambacho kinaweza kushindikana.
Wateja wa uhakika elfu moja na kuendelea ni kama bima ya uhakika kwenye biashara na maisha yako. Kwani hao wana nguvu ya kuweza kuikuza biashara kupitia manunuzi ya mara kwa mara, makubwa na kwa kuwaambia wengine.
Ukishafikia namba ya elfu moja, kwenda zaidi ya hapo ni rahisi kuliko ilivyokuwa kwenye kufika hapo.

Tukirudi kwenye namba 1, hii nina uhakika kabisa kwamba unayo.
Kwa wateja wote ulionao sasa, kuna mmoja ambaye anakufurahisha sana kwenye biashara yako.
Anza kwa kujiwekea lengo la kutengeneza wateja 10 wa aina hiyo.
Angalia ni kwa jinsi gani ulimpata huyo na umekuwa unamhudumiaje mara zote.
Kisha rudia zoezi hilo kwa wengine mpaka ujenge 10 ambao ni wa uhakika kabisa.

Baada ya kujenga wateja hao wa uhakika 10, lengo linalofuata ni kufikia 100. Hapo pia unarudia mchakato uliokufikisha kwenye 10 na kuufanya kwa ukubwa ili kufika kwenye 100.
Kadhalika kwenye kufikia wateja wa uhakika 1,000 na kuendelea, unarudia zoezi hilo hilo.

Kitu kimoja kitakachokushangaza ni kadiri unavyokwenda, ndivyo zoezi linavyokuwa rahisi.
Ukianza na mteja 1 kwenda 10, kazi inakuwa kubwa na ngumu. Na pia inaweza kuchukua muda mrefu kukamilisha.
Kutoka 10 kwenda 100, ugumu wa kazi unapungua huku pia muda wa kufanikisha ukiwa mdogo kuliko hatua ya nyuma.
Kutoka 100 kwenda 1,000 kazi pia inakuwa rahisi huku muda nao ukiwa mdogo kuliko hatua iliyopita.
Na kuanzia 1,000 na kuendelea, kazi unaweza hata usiifanye wewe, bali wateja bora wakawa wanakuja wenyewe kwa sababu tayari wengine bora wapo.

Kabla hujaanza utekelezaji wa zoezi hilo unaweza kuliona ni gumu kadiri unavyokwenda mbele.
Lakini uhalisia ni kinyume chake, linakuwa rahisi zaidi kadiri unavyokwenda.

Kilicho muhimu ni uepuke tamaa ya makubwa kabla hujakamilisha madogo.
Unaweza kuona 10 ni ndogo hivyo kukimbilia 100 kabisa.
Ni fikra nzuri, lakini kwenye utekelezaji ni vigumu.
Ni rahisi sana kuanza kutekeleza 10 kabla ya 100.
Ukishakamilisha wateja wa uhakika 10, ni rahisi sana kwenda kwenye lengo la 100.
Kadhalika kwenye namba zinazoendelea, unapokamilisha kwa namba za chini, inakuwa rahisi zaidi kwenda kukamilisha kwenye namba za juu.

Mafanikio makubwa unayoyataka yapo kwenye kujenga wateja bora na wa uhakika wa biashara yako.
Weka juhudi kubwa kwenye hilo na utaweza kupata chochote kile unachotaka.
Uzuri ni kwamba kama umeweza 1, utaweza pia 10, kisha 100, 1,000 na kuendelea.
Ukiangalia hizo namba zinakwenda kwa mara 10 na siyo kujumlisha, kwa sababu ukuaji unaohitajika ni mkubwa ili mafanikio makubwa yaweze kufikiwa kwa uhakika.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe