Barua ya XII; Kuhusu uzee.

Rafiki yangu Mstoa,
Wote tunajua mwenendo wa maisha yetu hapa duniani.
Tunazaliwa, kukua, kuzeeka na kufa. Katika kukua tunapitia utoto, ujana, utu uzima na hatimaye uzee.
Japo siyo lazima mtu apite hatua zote, wapo wanaokufa utotoni, wengine ujanani, wengine wakiwa watu wazina na wengine uzeeni.

Katika hatua hizo mbalimbali za maisha, nyingi huwa ni za matumaini makubwa, isipokuwa hatua ya uzee.
Hiyo ni hatua ambayo kwa wengi huambatana na changamoto mbalimbali za kiafya na mtu kujua kwa hakika muda wake hapa duniani umeisha.

Katika kukabiliana na hali ya uzee, wapo ambao huwa wanaikataa hali hiyo, kwa kujiona bado wana muda. Na wapo ambao huwa wanakatishwa tamaa na hali hiyo mpaka kufikia kupoteza matumaini.
Wote hao huishia kuwa na msongo unaotokana na hali hiyo kitu kinachopelekea washindwe kuishi maisha bora na kuyafurahia.

Kwa kuona hilo, Mwanafalsafa Seneca, kwenye moja ya barua zake kwa rafiki yake Lucilius alielezea hali hiyo ya uzee na jinsi ya kukabiliana nayo.
Kupitia barua hii Seneca ametushirikisha jinsi ya kuendelea kuishi maisha bora kwetu bila kujali ni hatua ipi ya maisha tupo.
Na anaenda mbali zaidi na kutuonyesha umri wa uzee ndiyo umri mzuri wa kuyafurahia maisha.

Karibu tujifunze kutoka kwenye barua hii na kuendelea kujenga maisha bora kabisa kwetu kwenye kila hatua ya maisha yetu.

1. Kila kitu kinazeeka.

Seneca anaianza barua kwa kueleza safari aliyofanya kwenda kwenye kijiji alichokulia na kukuta vitu alivyoacha havikuwa kwenye ubora ambao aliviacha navyo.
Alikuta nyumba imeanza kuharibika, mimea imepukutisha majani yake na wasaidizi wamezeeka.
Seneca alilaumu kwamba vitu hivyo havikutunzwa vizuri ndiyo maana vimefikia hali hiyo.
Lakini msaidizi wake alimkumbusha kwamba ni miaka mingi imepita na vitu hivyo vimezeeka.
Hilo linamfanya Seneca akumbuke kwamba hata yeye amezeeka.

Hatua ya kuchukua;
Kumbuka hakuna kitu kinachoendelea kubaki kama kilivyo milele. Kadiri muda unavyokwenda, vitu vinazeeka na kupoteza ubora wake, hata kama vinatunzwa kiasi gani.

Nukuu;
“I owe it to my country-place that my old age became apparent whithersoever I turned.” – Seneca

“Kila ninapotembelea kijiji nilichokulia, kila ninachoona kinanikumbusha kwamba nimezeeka.” – Seneca

2. Umri wa uzee ni wa kufurahia.

Kutokana na udhoofu unaoletwa na uzee, wengi huona umri wa uzee kama maisha ya mateso. Huona muda wa kuwa na maisha mazuri umepita na kilichobaki wakati wa uzee ni kumalizia ngwe iliyobaki.
Lakini Seneca anakataa hilo, anasema umri wa uzee ni wa kufurahia kwa sababu una raha nyingi kama mtu atajua jinsi ya kuzitumia.
Anaeleza jinsi ambavyo asili inaonyesha raha na utamu wa vitu vinapokaribia mwishoni.
Kwa mfano matunda huwa yanakuwa matamu zaidi wakati yanapoelekea mwisho wa msimu.
Na hata kwenye vilevi, ni kinywaji cha mwisho ndiyo humpa mtu raha anayopata kwa ulevi.
Seneca anasisitiza kila raha huwa inakuwa kubwa zaidi pale inapoelekea mwishoni.
Kwa maana hiyo basi, maisha pia yanakuwa ya raha zaidi kwenye umri wa uzeeni.

Raha nyingine ambayo mtu anaweza kuipata uzeeni ni kuwa ameshajaribu raha zote na hivyo hakuna kitu kipya kwake.
Mara nyingi wakati wa ujana mtu huwa na hamu ya kujatibu kila aina ya raha.
Lakini baada ya kujaribu raha zote ndiyo anakuja kugundua kwamba ni vitu vya kupita tu.
Kwa kufika uzeeni na kugundua hilo, unapata hali ya kuridhika na kuyafurahia zaidi maisha yako.

Hatua ya kuchukua;
Usichukulie uzee kama kipindi cha mateso, bali chukulia kama kipindi kizuri cha kuyafurahia maisha yako.
Ishi kwenye kila kipindi cha maisha yako kwa ukamilifu ili wakati wote uwe unayafurahia maisha yako.

Nukuu;
“Life is most delightful when it is on the downward slope, but has not yet reached the abrupt decline.” – Seneca

“Maisha huwa ni mazuri zaidi wakati yanaelekea mwishoni, ila kabla hayajakatika ghafla.” – Seneca

3. Kifo hakipo uzeeni pekee.

Kitu kingine kinachowafanya watu wengi wasiyafurahie maisha yao ya uzeeni ni ile hali ya kuona wamekikaribia kifo.
Uzee unachukuliwa kama kipindi ambacho mtu anakiangalia kifo chake.
Lakini Seneca hakubaliani na hilo, anaeleza wazi kwamba kila umri wa maisha, kila mtu anakiangalia kifo chake.
Na hilo ni dhahiri, kwani watoto wanakufa, vijana wanakufa, watu wazima wanakufa na wazee pia wanakufa.
Hivyo badala ya mtu kuona maisha ya uzeeni ni mabaya kwa sababu yanaendea kifo, anapaswa kufurahia kwa sababu ameweza kukikwepa kifo kwa muda mrefu wa maisha yake.
Seneca anasisitiza kifo hakitokei kwa mpangilio wa umri.
Na pia anaeleza hata mtu awe mzee kiasi gani, bado anaweza kufurahia hata siku moja ya ziada anayoweza kuipata.

Hatua ya kuchukua;
Usichukulie umri wa uzee kama wakati pekee ambapo unakuwa na hatari ya kifo, badala yake kumbuka kila wakati unapokuwa hai, unakuwa na hatari ya kifo, hivyo tumia muda wako kwa ukamilifu.

Nukuu;
“Death, however, should be looked in the face by young and old alike. We are not summoned according to our rating on the censor’s list.” – Seneca

“Kifo kinapaswa kuangaliwa usoni na vijana na wazee kwa usawa. Kifo hakituiti kwa kigezo cha umri.” – Seneca

4. Miduara ya maisha.

Seneca anaeleza kwamba maisha yetu yamegawanyika kwenye vipande ambavyo vinahusisha miduara mikubwa inayofunika miduara midogo.
Mduara mkubwa kabisa wa nje unajumuisha maisha yetu yote, tangu kuzaliwa mpaka kufa.
Mduara wa ndani unaofuatia unawakilisha maisha ya ujana mpaka utu uzima.
Mdura wa tatu kwenda ndani unajumuisha maisha yote ya utotoni.
Ndani zaidi kuna miduara inayowakilisha mwaka, mwezi na mpaka siku.
Na hata kwenye siku, kuna mwanzo na mwisho.
Tunapoyaangalia maisha uzeeni kama kitu kimoja, tunakosa fursa ya kuona hatua nyingi ambazo tumepiga mpaka kufika hapo.
Ni muhimu tuyaangalie maisha yetu kwa kila hatua na kuthamini yote ambayo tumepitia.

Hatua ya kuchukua;
Mara zote kumbuka huzaliwi na ukawa mzee,  badala yake unapitia hatua mbalimbali mpaka kufikia uzee.
Tumia kila hatua vizuri na uzeeni kumbuka hatua zote ili uzidi kuona thamani kubwa ya maisha yako.

Nukuu;
“Our span of life is divided into parts; it consists of large circles enclosing smaller.” – Seneca

“Maisha yetu yamegawanyika kwenye vipande; yanahusisha miduara mikubwa inayofunika miduara midogo.” – Seneca

5. Ishi kila siku kama vile ni ya mwisho kwako.

Kitu kingine kinachofanya watu washindwe kuyafurahia maisha yao ya uzeeni ni kujikuta kwenye hali ya uzee kabla hata hawajayaishi maisha yao.
Hiyo inatokana na tabia ya watu kuahirisha kufanya mambo yaliyo muhimu.
Kila wakati wanajiambia watafanya kesho, ambayo imekuwa haifiki.
Muda unazidi kwenda na siku moja watu wanazinduka wakiwa uzeeni na mengi waliyotaka kukamilisha kwenye maisha yao hawajayakamilisha.
Kuondokana na hali hiyo, Seneca anashauri zoezi la kuiishi kila siku kama vile ni siku yako ya mwisho hapa duniani.
Kuhakikisha unakamilisha kufanya yale yote muhimu uliyopaswa kuyafanya siku hiyo, ukijua kwamba kesho siyo yako.
Na kama utaiona kesho, basi unaichukulia kama zawadi ambayo nayo unaifurahia na kuitumia vizuri kama siku ya mwisho.
Ukienda kwa mpango huo, utaiishi kila siku kikamilifu na kuyafurahia maisha yako yote mpaka uzeeni.

Hatua ya kuchukua;
Kila siku panga na kukamilisha yale muhimu kwako kufanya. Pale unapojiambia utafanya kesho, jikumbushe kesho haipo, kwani leo ndiyo siku yako ya mwisho.
Nenda hivyo kila siku na utaweza kukamilisha yote muhimu na hivyo kuweza kuyafurahia maisha yako.

Nukuu;
“Let us go to our sleep with joy and gladness; let us say:
I have lived; the course which Fortune set for me Is finished.
And if God is pleased to add another day, we should welcome it with glad hearts.” – Seneca

“Tunapaswa kwenda kulala kwa furaha tukijiambia; nimekamilisha kuishi mwendo ambao asili imenipangia.
Na kama Mungu atapendezwa kutuongezea siku nyingine, tunapaswa kuipokea kwa moyo wenye furaha.” – Seneca

Rafiki yangu Mstoa, kama tulivyojifunza kwenye barua hii, umri wa uzee ni wa kuyafurahia maisha kama tumeyaishi vizuri na kwa ukamilifu wakati wote.
Hicho ni kitu ambacho tunaweza kuanza kukifanya sasa kama hatukuwa tunafanya huko nyuma.
Kwa kuanza kuiishi kila siku kwa ukamilifu wake, kama vile ndiyo siku yako ya mwisho hapa duniani.
Kwa hatua hiyo tu tunaweza kuyabadili sana maisha yetu, kwa kuyafanya kuwa bora zaidi na kuweza kuyafurahia kwa kipindi chote cha uhai wetu.

Kutoka kwa Mstoa mwenzako,
Kocha Dr Makirita Amani.