3127; Nilikuwa nakufikiria.

Rafiki yangu mpendwa,
Pata picha umempigia mtu simu na akaanza kwa kukuambia bora umempigia maana alikuwa anakufikiria, utajisikiaje?
Halafu pia pata picha mtu amekupigia simu na kuanza kwa kukuambia alikuwa anakufikiria, utajisikiaje?

Katika hali zote, utajisikia vizuri, kwamba mtu amekuwa anakufikiria, maana yake wewe ni wa muhimu kwake.
Lakini kwenye hali ya pili, ambapo mtu amekupigia simu na kukuambia hivyo, inakuwa na uzito zaidi, maana yeye ndiye amechukua hatua.
Kwenye hali ya kwanza unaweza kupata wasiwasi kama kweli anamaanisha, maana wewe ndiye umempigia.

Kitu kikubwa unachojifunza hapa ni kwamba huwa unapenda pale wengine wanapokupigia simu na kukuambia walikuwa wanakufikiria.
Unajua nani wengine ambao pia huwa wanapenda hilo?
Ni wateja wako.
Wateja wowote ulionao kwenye biashara unazofanya, huwa wanapenda sana kusikia kwamba ulikuwa unawafikiria.
Hivyo unapowapigia simu wateja wako na kuanza na maneno hayo, yanakuwa na uzito mkubwa sana kwao.

Wateja wanakuona wewe ni mtu unayewajali pale unapowapigia simu na kuwaambia ulikuwa unawafikiria.
Au kuwatembelea walipo na kuwaambia hivyo.
Wakati mwingine hata ujumbe wa maandishi wa simu pia unaweza kuwa na nguvu hiyo hiyo ya kuwafanya wateja wajione ni wa muhimu.

Moja ya njia ya uhakika ya kukuza mauzo kwenye biashara yako ni kujenga mahusiano mazuri na wateja wako.
Unayajenga mahusiano hayo kupitia kujali maslahi yao.
Na simu za kuwapa wateja salamu ni sehemu muhimu ya kujenga na kuboresha mahusiano na wateja wako.

Wengi wamekuwa wanakwama kwenye hili la kuboresha mahusiano na wateja kwa kutokujua nini wafanye.
Hapa unakwenda kujifunza hatua za kuchukua kwenye kukamilisha hilo.

Hatua muhimu za kuchukua ili kuboresha mahusiano na wateja wako ambayo yatapelekea ukuze zaidi mauzo;
1. Kuwa na orodha kamili ya wateja wako wote pamoja na hali yao ya manunuzi na mawasiliano ambayo umekuwa unafanya nao.
2. Wagawe wateja wako kwenye makundi mbalimbali kama; wateja wakubwa, wanaonunua mara kwa mara, ambao hawajanunua muda mrefu, uliowapoteza na unaowafuatilia ambao bado hawajajunua.
3. Kila siku chagua wateja wasiopungua watano ambao utawasiliana nao kwa mkakati huu wa kuwakumbuka.
4. Wapigie simu na maelezo yawe hivi; Habari John, nilikuwa nakufikiria, vipi unaendeleaje? Familia inaendeleaje?
5. Msikilize kwa yale atakayokujibu na endeleza mazungumzo kulingana na majibu yake.
6. Kwenye hayo mazungumzo chomekea kitu ambacho kitaweza kumeshawishi anunue, kwa kukuuliza kama ana oda, kumpendekezea bidhaa zilizopo, kumkumbusha ofa nzuri iliyopo au kumwomba rufaa.
7. Endelea na mazungumzo na mteja wako kadiri yanavyokwenda na onyesha kweli unajali na tumia kila fursa unayoipata kuuliza vitu zaidi kwake vitakavyopelekea ukuze mauzo.

Uzuri wa zoezi hilo la kuwapigia wateja na kuwaambia ulikuwa unawafikiria, huku ukitaka kujua wanaendeleaje wao na familia zao, lina nguvu kubwa sana ya ushawishi kwenye kujenga mahusiano bora na wateja na hata kukuza mauzo.
Mteja atajisikia vizuri sana na kuona unajali kuhusu yeye na haupo tu kumuuzia.
Ni vigumu mteja akakukasirikia na kukukatia simu kwa sababu umekuwa unamkumbuka na umetaka kujua anaendeleaje.
Lakini pia ni vigumu kwake kukataa kukujibu maswali uliyomuuliza kuhusu maendeleo yake na ya familia yake.

Rafiki, hili ni zoezi ambalo lipo ndani ya uwezo wa kila mmoja wetu kulifanya.
Ni zoezi rahisi na lenye nguvu kubwa sana ya ushawishi.
Usiache kufanya zoezi hili kila siku.
Pia hakikisha timu yako yote ya mauzo inafanya zoezi hili.
Muda mzuri wa kulifanya ni mapema siku inapoanza, kabla mambo hayajawa mengi.

Ukiweza kufanya zoezi hili kwa muda mrefu na kwa msimamo bila kuacha, matokeo yake yatakuwa makubwa na mazuri sana.
Mahusiano yako na wateja yatakuwa bora na imara.
Na zaidi, utaweza kukuza zaidi mauzo yako, kwa sababu wateja watajisikia vizuri na kununua zaidi kwako.

Mauzo ni mahusiano, jenga mahusiano bora na wateja wako na utaweza kuuza zaidi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe