Barua ya XIII; Kuhusu hofu zisizo za msingi.

Rafiki yangu Mstoa,
Sisi kama binadamu huwa tuna malengo na mipango mbalimbali kwenye maisha yetu.
Kuna namna ambavyo huwa tunataka maisha yetu yawe.
Lakini pamoja na malengo na mipango hiyo, bado kwa sehemu kubwa maisha ya wengi yamekuwa yakiishia kuwa ya kawaida.
Wengi wanashindwa kuchukua hatua kwenye mambo waliyopanga wao wenyewe, kwa sababu ya hofu.

Hofu imekuwa kikwazo kikubwa kwa watu wengi kuchukua hatua na kuwa na maisha wanayoyataka.
Kitu kikubwa na cha kushangaza kuhusu hofu ni mambo mengi ambayo watu wamekuwa wanayahofia huwa hata hayatokei.
Watu husumbuka sana na hofu na kushindwa kuchukua hatua walizopanga kuchukua, halafu yale wanayokuwa wanahofia hata hayatokei.

Hiyo ni hali ambayo imekuwepo kwa binadamu tangu enzi na enzi.
Mwanafalsafa Seneca aliona hili kwenye enzi zao na jinsi ambavyo lilikuwa kikwazo kwa watu kuishi maisha wanayoyataka.
Aliona jinsi watu wanazipa hofu nguvu, wakati hazina nguvu kubwa kiasi hicho.
Ndiyo maana kwenye barua yake ya 13 kwenda kwa rafiki yake Lucilius alieleza jinsi hofu zinavyowazuia watu wengi zisivyokuwa na msingi wowote.

Kwenye barua hiyo Seneca anatushirikisha jinsi tunavyoweza kuzivuka hofu na kuwa na maisha tunayoyataka.
Karibu tujifunze kama Wastoa, tuchukue hatua ili tuweze kuwa na maisha bora kabisa.

1. Uimara wako unapimwa kwa magumu unayopitia.

Watu wengi ni kama huwa wanataka kuishi maisha ambayo hayana changamoto yoyote ile.
Kitu ambacho kwa uhalisia hakiwezekani. Hakuna namna tunaweza kuendesha maisha ambayo hayana changamoto kabisa.
Changamoto tunazokutana nazo kwenye maisha ni njia ya asili ya kupima uimara wetu.
Hivyo badala ya kuhofia na kuchukia pale tunapokutana na magumu, tunapaswa kufurahia kwa sababu tunapata fursa ya kupima uimara wetu.

Seneca anatupa mfano wa wapiganaji, hawawezi kuwa imara kwenye mapambano kama hawajawahi kukutana na ugumu kwenye maandalizi yao.
Kama mambo ni rahisi kwao muda wote, wanakuwa dhaifu na kushindwa haraka.
Lakini wanapopitia magumu, wanakuwa imara na kuweza kushinda chochote.

Hatua ya kuchukua;
Umapokutana na magumu kwenye maisha yako usihofie wala kuumia, badala yake jua ni fursa ya kupima uimara wako. Yatumie magumu unayokutana nayo kuwa imara zaidi.

Nukuu;
“For our powers can never inspire in us implicit faith in ourselves except when many difficulties have confronted us on this side and on that, and have occasionally even come to close quarters with us.” – Seneca

“Huwezi kujua uimara wa nguvu zako mpaka pale unapokutana na magumu.” – Seneca

2. Tunateseka zaidi kifikra kuliko uhalisia.

Hofu siyo kitu ambacho kipo kwenye uhalisia, bali ni kitu tunachokuwa kwenye fikra zetu.
Tunaumia zaidi siyo kwa kile ambacho tayari kimeshatokea, bali kwa fikra tunazokuwa nazo kwa yale yanayoweza kutokea.
Ambayo kwa sehemu kubwa sana huwa hayatokei na hivyo tunaishia kuwa tumejiumiza bure tu.

Seneca anasema kuna vitu vingi ambavyo huwa vinatupa hofu, kuliko ambavyo vinatuumiza, tunateseka zaidi kifikra kuliko kwenye uhalisia.

Seneca anatushauri tusikubali kukosa furaha kabla hata jambo tunalotarajia litokee halijatokea.
Mambo mengi tunayokuwa tunayahofia, kwa kutarajia kwamba yatatokea, huwa hata hayatokei.
Hivyo hatupaswi kujinyima furaha sasa kwa mambo ya baadaye.

Seneca pia anasisitiza kwamba huwa tuna tabia ya kukuza mambo kuliko uhalisia wake.
Na hasa mambo ambayo bado hayajatokea, kifikra tunayakuza kuliko uhalisia wake.

Hatua ya kuchukua;
Chochote unachohofia kwamba kitatokea, usikiruhusu kikunyime furaha kabla hata hakijatokea.
Ishi kwenye uhalisia wako kwa wakati unaokuwepo na siyo kuishi kwenye fikra za yajayo.

Nukuu;
“There are more things, Lucilius, likely to frighten us than there are to crush us; we suffer more often in imagination than in reality.” – Seneca

“Lucilius, kuna mambo mengi yanayotutisha kuliko yanayotuumiza; tunateseka zaidi kifikra kuliko kwenye uhalisia.” – Seneca

3. Zingatia hisia zako na siyo yale unayoambiwa na wengine.

Unaweza kuwa unaendelea na maisha yako kwa utulivu kabisa, lakini watu wakakuambia mambo ambayo yanaibua hofu kubwa sana ndani yako.
Ni kawaida ya watu ambao wana hofu kwenye maisha yao, kuhakikisha na wengine pia wanakuwa na hofu kama waliyonayo.
Hivyo huwa wanahakikisha wanasambaza taarifa ambazo zitaibua hofu kwa wengine.

Seneca anatuambia hatupaswi kuruhusu yale tunayosikia kwa wengine yaathiri hisia zetu. Badala yake tunapaswa kuzingatia hisia tulizonazo sisi wenyewe na siyo tunazochochewa na wengine.
Seneca anatuambia tusikubali kupokea kitu chochote kinachoathiri hisia zetu kutoka kwa wengine bila ya kukihoji.
Tunapaswa kuhoji kama ni sahihi kujihusisha nacho kihisia na kwa nini tuache hisia zetu na kuchukua hizo za wengine.
Kwa kuhoji hivyo tunavinyima nguvu vitu vingi vinavyoletwa kwetu kwa lengo la kutupa hofu.

Kitu chochote kinachokupa hofu, hoji usahihi na uzito wake.
Hoji kama kweli kipo kwenye uhalisia au kwenye fikra.
Huwa tunavipa nguvu vitu ambavyo havipo kwenye uhalisia na wala havitokei.
Tusipokee kitu chochote bila ya kukihoji kwa kina.

Hatua ya kuchukua;
Chochote unachohofia kihoji na kukichunguza kwa undani. Hapo utagundua siyo kikubwa kama unavyodhania.

Nukuu;
“We do not put to the test those things which cause our fear; we do not examine into them; we blench and retreat just like soldiers who are forced to abandon their camp because of a dust-cloud raised by stampeding cattle, or are thrown into a panic by the spreading of some unauthenticated rumour.” – Seneca

“Huwa hatuviweki kwenye majaribio vitu vinavyotupa hofu; hatuvichunguzi; tunarudi nyuma na kukimbia kama wanajeshi walioacha kambi yao kwa kishindo cha kundi la ng’ombe au kwa tetesi zisizo za kweli.” – Seneca

4. Usiyaharakishe mateso, kama yatakuja, yaache yaje kwa wakati wake.

Hofu ni kama kuyaishi mambo ambayo bado hayajatokea na ambayo kwa sehemu kubwa hayatatokea.
Kuhofia mambo ambayo bado hayajatokea ni kuharakisha mateso kabla ya muda wake.

Seneca anatutaka tujiulize ni mara ngapi mambo ambayo hatukuwa tunayategemea kutokea yamekuwa yanatokea?
Ni mara ngapi mambo tunayotegemea yatokee hayatokei?
Na hata kama yatatokea, tunakuwa tumefaidika nini kukubali yatutese kabla hata hayajatokea?
Majibu yapo wazi, yanayotokea huwa ni tofauti kabisa na tunayokuwa tunatarajia.
Haina haja ya kujitesa kwa mambo ambayo kwa sehemu kubwa hayatatokea.

Huwa kuna kauli inayosema utalivuka daraja pale unapolifikia.
Hata usumbuke kiasi gani kwenye fikra zako kwa daraja lililo mbele yako, hakuna namna utaweza kulivuka kabla hujalifikia.
Kauli hii inatusisitiza kusubiri mambo mpaka yatokee kuliko kusumbuka nayo kabla hayajatokea.

Hatua ya kuchukua;
Pale unapokuwa unahofia kitu chochote, jiulize je tayari kimeshatokea? Kama jibu ni bado hakijatokea, basi usijiruhusu kukihofia, badala yake jiambie utakihofia kitakapotokea.

Nukuu;
“What does it avail to run out to meet your suffering? You will suffer soon enough, when it arrives; so look forward meanwhile to better things.” – Seneca

“Unanufaika nini kuyakimbilia mateso yako? Utateseka vya kutosha wakati utakapofika; ila kwa sasa angalia vile vizuri.” – Seneca

5. Akili ina tabia ya kutengeneza vitu visivyokuwepo kabisa.

Ni mara ngapi unakuta mambo yanaenda vizuri tu kwenye maisha yako, ghafla unapata fikra fulani na zinafanya uone kila kitu hakipo sawa kwenye maisha hayo.
Labda ni mteja amekujibu vibaya na hapo ukaona unampoteza mteja huyo, halafu utawapoteza wateja wote na utakuwa huna tena biashara.
Hivyo ndivyo akili zetu zilivyo na nguvu kubwa ya kutengeneza vitu ambavyo havipo kabisa na kuvipa nguvu ya kutusumbua sana.

Seneca ameelezea nguvu hiyo ya akili zetu kutengeneza hofu kwa vitu vya kudhaniwa, ambavyo havipo kabisa.
Akili ina tabia ya kuchukua kitu kidogo na cha kawaida kabisa na kukikuza kwa upande ambao ni mbaya, hali ambayo huwa inatupa hofu kubwa sana.

Huwa kuna kauli inayosema hofu ni matumizi mabaya ya uwezo mkubwa wa akili zetu kuumba, kuumba vitu vibaya na ambavyo havipo kabisa.
Yaani akili yako inaweza kuumba chochote kile kifikra, lakini mtu unaamua kutumia uwezo huo kuumba vitu vibaya ambavyo vinakupa hofu.

Hatua ya kuchukua;
Dhibiti uwezo mkubwa wa akili yako kuumba, ili uweze kuumba mambo chanya na siyo hasi.
Tengeneza taswira ya kifikra ya maisha mazuri unayoyataka na hiyo ndiyo itawale akili yako muda wote ili kusiwe na nafasi ya hofu kutawala.

Nukuu;
“The mind at times fashions for itself false shapes of evil when there are no signs that point to any evil; it twists into the worst construction some word of doubtful meaning.” – Seneca

“Akili huwa ina tabia ya kutengeneza mambo mabaya wakati hakuna mabaya yanayoendelea; inageuza mambo madogo kuwa makubwa.” – Seneca

6. Usijiandae kuishi, ishi.

Watu wengi sana wanashindwa kuyafurahia maisha yao kwa sababu wanayamaliza kabla hawajayaishi.
Kila wakati wanakuwa wanafanya maandalizi ya kuishi.
Wanaenda hivyo kwa miaka yao yote, wasipate muda ambao wameishi maisha waliyokuwa wanayataka.
Hiyo imekuwa inachangiwa pia na hofu ambazo watu wanakuwa nazo.
Hivyo kila wakati wanajikuta wakijiandaa na hofu ambazo hata hazitokei.
Na kwa kuwa hofu huwa haziishi, kila wakati wanakuwa kwenye maandalizi ya kuishi, badala ya kuishi.

Seneca anasema ni upumbavu kwa watu kuamua kuyapoteza maisha yao kwa njia hiyo.
Kila wakati mtu anakuwa kwenye maandalizi ya kuanza kuishi, kitu ambacho huwa hakitokei mpaka mtu anaingia kaburini.

Maisha uliyonayo sasa ndiyo maisha pekee uliyonayo, unapaswa kuyaishi kwa ukamilifu wake.
Usiruhusu hofu zozote zile zikufanye uahirishe kuyaishi maisha yako kwa ukamilifu wake.
Ishi kwa kukabiliana na kile kilicho mbele yako kwa sasa, yanayokuja utakabiliana nayo wakati yatakapokuja na siyo kuahirisha maisha yako ya sasa kwa kujiandaa na hayo yajayo.

Hatua ya kuchukua;
Kumbuka kwamba kila siku inayopita ni siku ambayo hutakuja kuipata tena kwenye maisha yako. Hivyo ishi kila siku kwa ukamilifu wake ili usije ukayapoteza maisha yako yote kwa maandalizi ambayo hayakamiliki.

Nukuu;
“The fool, with all his other faults, has this also, – he is always getting ready to live.” – Seneca

“Mpumbavu, pamoja na makosa mengine anayofanya, huwa pia ana tabia ya kila wakati kuwa anajiandaa kuishi.” – Seneca

Rafiki yangu Mstoa, kama tulivyojifunza kwenye barua hii, hofu siyo kitu cha uhalisia, bali ni kitu cha kifikra.
Tusikubali hofu kutuzuia kuishi maisha ambayo tunataka kuyaishi.
Tukumbuke maisha tuliyonayo sasa ndiyo maisha pekee tuliyonayo, hivyo tuyaishi kwa ukamilifu na kutoruhusu hofu ziwe sababu ya kuahirisha maisha yetu.

Kutoka kwa Mstoa mwenzako,
Kocha Dr Makirita Amani.