3134; Maswali mawili yatakayokuwezesha kuuza zaidi.

Rafiki yangu mpendwa,
Leo napenda nikupe taarifa ambazo zitakushtua kidogo.
Taarifa hizo zitakushtua kwa sababu ni tofauti kabisa na matarajio uliyonayo.

Kwenye biashara yako una wateja ambao tayari wananunua kwako mara kwa mara.
Lakini je unajua ni kwa kiasi gani wateja hao wanajua vitu vyote unavyoweza kuwauzia?

Unaweza kudhani wateja wako wanajua vitu vyote unavyouza, kwa sababu ulishawaambia.
Lakini huo siyo ukweli.
Wateja wanajua asilimia 20 tu ya vitu vyote ambavyo unauza.
Yaani kama unauza vitu 10, mteja wako anajua vitu viwili tu, vingine nane hajui kama unauza.

Unaweza kukataa hilo na kusema wateja wako wanajua vyote unavyouza kwa sababu umeshawaambia.
Lakini ukweli ni kwamba kwa sababu umewaambia wateja yote unayouza haimaanishi wanakumbuka.
Ni rahisi wewe kukumbuka vitu vyote unavyouza, kwa sababu ndiyo unavifikiria kwa muda mrefu.
Wateja wako wana mambo yao wanayoyafikiria kwa muda mrefu, ila biashara yako siyo moja kati ya hayo.

Kama bado inakuwa vigumu kwako kukubali hilo hebu jiulize ni mara ngapi umekutana na wateja wako wakiwa wananunua mahali pengine vitu ambavyo hata wewe unauza?
Na unapowauliza mbona hawanunui kwako wanakujibuje? Wengi watakuambia hawakujua kama pia unauza vitu hivyo.
Unaweza hata kuwaambia kwamba ulishawaambia, lakini bado haifasaidia.

Rafiki, sisi binadamu huwa tunaendesha maisha yetu kwa mazoea. Karibu nusu ya mambo tunayofanya kwenye siku yetu ni kwa mazoea, tunafanya kama ambavyo tumekuwa tunafanya.

Hivyo wateja wako pia tayari wanayo mazoea wanayoyatumia kwenye kufanya maamuzi ya manunuzi.
Tayari wameshazoea vitu gani wananunua kwako na vitu gani wananunua kwa wengine.

Kadhalika na wewe pia umekuwa unauza kwa mazoea.
Tayari unajua wateja wako wakija kwako wananunua vitu gani.
Unaweza kudhani ni vile tu wanavyonunua mara kwa mara ndiyo pekee wanavyohitaji.

Lakini kama ambavyo tayari tumeshaona, wateja wananunua zaidi, ila tu hawanunui kutoka kwetu.
Ili kuweza kuvuka hilo la wateja kututenga na sisi kuwatenga, tunatakiwa kuvunja hayo mazoea ambayo tayari yameshajengeka kati yetu na wateja.

Mazoea hayo yanavunjwa na maswali mawili ambayo unapaswa kuwauliza wateja wako wote mara kwa mara ili wajue vitu zaidi unavyouza na siyo vile tu walivyozoea wao.

Swali la kwanza ni; Hivi unajua …. ?
Hili ni swali ambalo unawauliza wateja wako kama wanajua kuhusu bidhaa au huduma nyingine unazouza, lakini hawajawahi kununua kwako.
Kwa mfano unaweza kumuuliza mteja; Hivi unajua pia tunauza … ambayo itakufaa sana kwa mahitaji/matumizi yako?
Hapo unachagua bidhaa au huduma ambazo unazo ila mteja hajawahi kununua kisha kumuuliza.
Unapaswa kuuliza swali hili mara kwa mara kwa wateja wako wote, hata kama ulishawaambia.
Kwa sababu kama hawajawahi kununua, jibu la kwanza ni kwamba hawajui kama  unauza, hivyo vuka hilo kwa kuwaambia na kuwauliza mara kwa mara.

Swali la pili ni; Ni vitu gani vingine unavyonunua kwa wafanyabiashara wengine ila hupati huduma nzuri kama kwetu?
Swali hili linamtaka mtu akueleze vitu ambavyo tayari ananunua kwa wafanyabiashara wengine, ambavyo haridhishwi navyo.
Kwa majibu anayokupa, unaweza kuona kama ni vitu ambavyo tayari unauza na hivyo kuweza kumuuzia moja kwa moja.
Na kama ni vitu ambavyo huuzi, unaweza kumuunganisha mteja wako na wafanyabiashara ambao watawahudumia vizuri.

Yaulize maswali haya mara kwa mara kwa wateja wako wote kila wanapofanya manunuzi kwako au unapokutana au kuwasiliana nao.
Usidhani kwamba wanajua yote unayouza.
Na hata kama wanajua, usidhani wanakumbuka mara zote.
Kama hawajawahi kununua kwako au ni muda mrefu hawajanunua, jua kwamba hawajui au hawakumbuki.
Uliza maswali hayo ili kuwafahamisha na kuwakumbusha.

Kwa takwimu zinazotokana na kanuni ya wastani, kwa wateja watano unaowauliza maswali hayo, angalau mmoja atafanya manunuzi ya ziada kwako. Hiyo ni asilimia 20, namba ambayo ni kubwa kwenye mauzo.
Hivyo maswali hayo mawili yana nguvu kubwa ya kuongeza mauzo yako kwa uhakika.
Yaulize maswali hayo kwa wateja wako wote na mara kwa mara.
Hata kama ni kwa kurudia rudia kwa kila mteja, fanya hivyo kwa sababu kama hajanunua, hajui au hakumbuki.

Na kama utamuuliza mteja na akakuambia tayari anajua, hakuna ulichopoteza. Utamwambia unapenda kuhakikisha wateja wako wanapata manufaa zaidi kwenye biashara yako.
Na hapo pia unaweza kukamilisha mauzo moja kwa moja.
Kwa kumwambia vizuri sana kwa kujua, leo unachukua ngapi?
Halafu unakaa kimya na kumwacha aongee.
Kama amejivunia kwako kwamba tayari anajua, ataona ana wajibu wa kununua kama anao uhitaji.

Uliza maswali haya kila mara na hakikisha timu yako ya mauzo inafanya hivyo pia ili kuweza kufanya mauzo makubwa zaidi kwa wateja ambao tayari wapo kwenye biashara yako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe