3144; Kuepuka kupoteza.

Rafiki yangu mpendwa,
Zipo njia mbalimbali za kujifunza kitu.
Njia ya kwanza ni jinsi ya kupata kitu hicho na njia ya pili ni jinsi ya kukikosa.

Tumezoea sana kujifunza njia ya kwanza ya kupata na kusahau njia ya pili ya kukosa, ambayo pia ina nguvu kubwa.

Bilionea mwekezaji Charlie Munger huwa ana kauli yake maarufu inayosema; ninachotaka kujua ni wapi nikienda nitakufa ili nisiende hapo.

Nukuu hiyo inaonyesha nguvu ya kujifunza kwa kuepuka kupoteza badala ya kutaka kupata.

Kujifunza kupitia uzoefu wa wengine huwa kuna nguvu kubwa kuliko tu kutegemea uzoefu wako binafsi.

Sasa kwa kuwa kwenye jamii tunazungukwa na watu wengi walioshindwa kuliko waliofanikiwa, tunapaswa kuangalia yale walioshindwa wanapenda kuyafanya na kwenda kinyume na hayo.

Mwandishi, mjasiriamali na mwekezaji Alex Hormozi ametupa orodha ya mambo ambayo kwa uhakika yanawaweka watu wengi kwenye umasikini.
Kwa kuyajua na kuyaepuka mambo hayo, inakuwa na nguvu ya kuwatoa watu kwenye umasikini na kuwafikisha kwenye utajiri.

Kwa majibu wa Hormozi, ambao pia ndiyo uhalisia, hivi ndivyo watu wengi wanavyobaki kwenye umasikini;

1. Kila siku kusema wataanza kesho, kitu ambacho hawaanzi kabisa.

2. Kusoma vitabu bila ya kufanya chochote.

3. Kuchukua ushauri wa watu masikini wa jinsi ya kuwa tajiri.

4. Kuchagua mwenza ambaye anakufanya ujione una hatia pale unapofanya kazi zaidi.

5. Kushindwa mara moja na kukata tamaa milele.

6. Kulaumu hali unazopitia.

7. Kusubiri mpaka kila kitu kiwe na ukamilifu.

8. Kuwalaumu wengine.

9. Kutegemea serikali ikusaidie.

10. Kuthamini maoni ya wengine kuliko maoni yako binafsi.

11. Kulalamika.

12. Kukwepa usumbufu.

13. Kufaka matokeo ya haraka baada ya kazi.

14. Kuvumilia viwango vya chini.

15. Kuahidi halafu kutokutimiza ahadi hizo.

16. Kutaka kuonekana tajiri badala ya kuwa tajiri.

17. Kufanya kazi kwa juhudi kwenye mambo yasiyo muhimu.

18. Kusema utafanya kitu, halafu usikifanye.

19. Kusubiri mpaka uwe tayari.

20. Kufanya kazi kwa asilimia 99, kutegemea matokeo kwa asilimia 1.

21. Kufanya unachoweza badala ya kufanya kinachohitajika.

22. Kusema upo kwenye umasikini kwa sababu hutaki kuvunja maadili yako.

23. Kuongea sana na kutokufanya chochote.

24. Kuanza kitu kipya leo, kuanza kitu kipya kesho na kurudia huo mzunguko.

25. Kufikiria kununua na kuuza hisa wakati hujawa na kipato cha uhakika.

26. Kufanya makosa na kurudia makosa hayo.

27. Kupata kitu kinachofanya kazi, kisha kuacha kukifanya.

28. Kudhani mara zote upo sahihi.

29. Kuchukia pale mtu anapokuwa hakubaliani na wewe.

30. Kuongeza kipato chako kisha kuongeza matumizi mara dufu.

31. Kubadili malengo yako pale yanapokuwa magumu.

32. Kufanya yale ambayo kila mtu anayafanya na kutegemea kupata matokeo ya tofauti.

33. Kutumia gharama kubwa kwenye burudani badala ya elimu.

34. Kutokufanya maandalizi.

35. Kuamini yale ambayo watu wanasema kuliko yale wanayofanya.

36. Kuona wengine wanakosea na wewe kurudia makosa hayo.

37. Kudhani kwa sababu huwezi kumudu kitu basi mteja pia hawezi kukimudu.

38. Kutaka kila mtu akupende.

39. Kudhani kupata pesa na kutunza pesa ni kitu kimoja.

40. Kudhani kwamba usipochukua hatua za hatari basi umekwepa hatari kubwa kuliko zote – kutokufanya chochote.

Rafiki, ni orodha ndefu ambayo imejumuisha tabia zote ambazo zinawaweka watu wengi kwenye umasikini.

Je ni tabia zipi kati ya hizo unazo kwa ukubwa?
Unafanyaje ili kuondokana na tabia hizo ili uweze kuondoka kwenye umasikini?
Shirikisha majibu ya haya maswali kwenye maoni hapo chini.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe