3145; Ni wewe.

Rafiki yangu mpendwa,
Huwa kuna usemi maarufu kwenye tasnia ya mafunzo ya maendeleo binafsi kwamba kama unataka kumwona mtu anayekuzuia wewe kufanikiwa basi simama mbele ya kioo.
Ikimaanisha kwamba wewe ndiye kikwazo cha kwanza kwako kufanikiwa.

Hicho ni kitu ambacho watu wengi wanakichukulia poa sana. Wengi wakiwa hawakiamini kweli na hilo kuwapelekea kuhangaika na mambo mengi ambayo hayana tija.

Watu wote ambao wameweza kujenga mafanikio makubwa sana kwenye maisha yao, walianzia chini kabisa.
Na zaidi, kuna kipindi walipitia anguko kubwa, wakapoteza kila kitu kabisa.
Lakini waliweza kusimama tena na kujenga mafanikio makubwa kuliko waliyopoteza.
Unajua kwa nini?

Donald Trump aliwahi kupitia anguko kubwa na kufilisika kabisa. Alivunja rekodi ya kitabu cha maajabu ya dunia kwa kuwa mtu aliyepoteza utajiri mkubwa ndani ya muda mfupi.
Lakini haikupita muda mrefu akawa amerudisha utajiri wake wote na kujenga mwingine wa ziada kabisa.

Kuna vitu vingi ambavyo watu wanaweza kukuibia kwenye maisha yako.
Wezi wanaweza kuiba fedha na mali zako.
Serikali inaweza kutaifisha mali zako.
Uchumi unaweza kuyumba na ukaishia kupoteza uwekezaji mkubwa uliofanya kwa maisha yako yote.
Unapokutana na hayo kwenye maisha, unaweza kupata anguko kubwa na kujikuta uko chini kabisa.

Lakini je unadhani utakuwa sawa na wakati unaanza?
Jibu ni hapana kama utakuwa umejijengea vitu vitatu ambavyo hakuna mtu, serikali au uchumi unaoweza kukunyang’anya.

Kuna vitu vitatu unavyopaswa kujijengea kwa uhakika, ambavyo vitakuhakikishia mafanikio wakati wote na hakuna yeyote au chochote kinachoweza kukuibia.
Ukiweza kujenga vitu hivi vitatu, hakuna namna utashindwa, kama bado upo hai.

Kitu cha kwanza ni Imani.
Unapaswa kuamini bila ya shaka yoyote ile kwamba unao uwezo na utaweza kupata chochote unachotaka kwenye maisha yako.
Wasiwasi kwamba unaweza usipate unachotaka haupaswi kupata nafasi yoyote kwenye fikra zako.
Imani unayokuwa nayo juu yako inapaswa kuwa imara sana kiasi cha kukuona kama umechanganyikiwa hivi.
Unapaswa kuwapuuza wote ambao hawaamini vile unavyoamini wewe.
Hiyo ndiyo itakuwa kinga ya kuwazuia wengine wasivuruge imani yako.

Hatua ya kufanyia kazi; amini bila ya shaka yoyote kwamba utapata kile hasa unachotaka. Kuwa na uhakika kwamba dunia itakula njama kuhakikisha unapata unachotaka.

Kitu cha pili ni Ujuzi.
Unaweza kufanya nini ni kitu kingine muhimu ambacho ukijijengea hakuna mtu yeyote anayeweza kukunyang’anya. Ukishakuwa na ujuzi, utakuwa nao kwa kipindi chote cha maisha yako.
Na kadiri unavyotumia ujuzi wako, ndivyo unavyozidi kuwa bora kwenye ujuzi huo.
Kuna ujuzi wa aina nyingi hapa duniani, lakini sisi tunahitaji kujenga ujuzi wa aina mbili tu; biashara na uwekezaji.
Ujuzi wa biashara nao unahusisha ujuzi mwingine mwingi ndani yake, kama masoko, mauzo, usimamizi, fedha n.k.
Ujuzi wa uwekezaji unahusisha kuelewa aina ya uwekezaji unaofanya, kuanza mapema, kufanya kwa msimamo na kuwa na subira.

Hatua ya kufanyia kazi; jijengee ujuzi wa biashara na uwekezaji na kila siku endelea kujifunza kubobea kwenye maeneo hayo na kutumia yale unayojifunza kuboresha zaidi ujuzi wako. Kila siku kuwa bora zaidi kwenye kile unachofanya kuliko ulivyokuwa siku za nyuma. Wekeza kwenye ujuzi wako, itakulipa mara dufu.

Kitu cha tatu ni Tabia.
Huwa kuna kauli inayosema; huwa tunajenga tabia, kisha tabia zinatujenga. Sehemu kubwa ya mambo unayofanya kila siku unayafanya kwa tabia. Tabia zinakuongoza na kutawala maisha yako.
Na pia kuna usemi mwingine unaosema tabia ni ngozi, huwa ni ngumu sana kubadili.
Watu wanaweza kufanya mambo mengi kwako, lakini hawawezi kukulazimisha kubadili tabia yako.
Wanaweza kukunyang’anya kila kitu, ila tabia zako zitabaki na wewe.
Kuna tabia ngingi unazopaswa kujijengea kwenye maisha yako, lakini tabia moja unayopaswa kuipa uzito zaidi ni KUPENDA KUFANYA KAZI KWA JUHUDI KUBWA.
Jijengee tabia ya kupenda kufanya kazi kwa juhudi kubwa. Kipaumbele cha kwanza kwako kiwe kazi kabla ya vitu vingine vyote kwenye maisha yako.
Rafiki yako wa kwanza awe kazi, mpenzi wako wa kwanza awe kazi, ndugu yako wa thamani awe kazi.
Popote unapokuwa, hakikisha unajulikana kama mtu anayefanya kazi kwa juhudi kubwa kuliko wote.
Kwa tabia hiyo ya kupenda na kuthamini kazi, hata ikitokea umepoteza kila kitu, utaweza kujenga upya kupitia kazi.
Kwa kuwa unapenda kazi, hutaona aibu kuanzia tena chini na kuweka kazi ili kujenga mafanikio yako upya.

Hatua ya kufanyia kazi; kwenye muda wako wa siku, fanya kazi kuwa kipaumbele cha kwanza kwako. Kwenye masas yako 24 ya siku, angalau theluthi mbili (masaa 16) inapaswa kuwa muda wa kufanya kazi. Fanya hivyo kila siku kwa maisha yako yote na hakuna namna utaweza kushindwa.

Imani, Ujuzi, Tabia.
Amini bila ya shaka yoyote kwamba utapata kile unachotaka.
Jenga na boresha ujuzi kwenye biashara na uwekezaji. Hapa ujuzi mkuu ukiwa mauzo.
Jenga tabia bora kabisa zinazokufikisha kwenye unachotaka. Hapa tabia kuu ikiwa ni kupenda sana kazi.
Simamia hayo matatu na hakuna namna utaweza kushindwa kwenye maisha yako.
Hata ukipoteza kila kitu, utaweza kuanza tena na ndani ya muda mfupi ukapata zaidi ya ulivyopoteza.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe