3147; Tumia sababu zote za kushindwa.

Rafiki yangu mpendwa,
Wote tunakumbuka wakati tupo shuleni.
Tulijua kuna mitihani ambayo inakuja.
Pale tulipojiandaa vyema na mitihani hiyo na ikatokea tukafanya vibaya, huwa hatuumii sana, kwa sababu tunajua tumefanya kila kitu.
Lakini pale ambapo hatukujiandaa vyema na ikatokea tumefanya vibaya, huwa tunaumia sana.
Tunajiambia kama tungejiandaa vyema, huenda tungefanya vizuri.
Kwa kifupi tunakuwa na majuto pale ambapo hatujafanya maandalizi mazuri.

Na hivyo ndivyo ilivyo kwenye maisha yetu yote.
Huwa tunatengeneza majuto makubwa kwenye maisha pale tunapokuwa tunajua tunachopaswa kufanya ila hatukifanyi.
Tunapoishia kuwa na maisha ambayo hatuyataki, tunajiambia kama tungechukua hatua, tusingeishia kwenye maisha ya aina hiyo.

Leo nataka ujifunze na uchukue hatua ambayo itafuta kabisa majuto kwenye maisha yako.
Na hilo linahusisha hatua kadhaa za kufanyia kazi.

Kwanza kabisa unaanza na kile hasa unachotaka kupata kwenye maisha yako. Wapi ambapo unataka kufika. Nini ukifikia utayahesabu maisha yako kuwa ya mafanikio?

Pili orodhesha sababu zote zinazoweza kukuzuia kupata hicho unachotaka. Orodhesha kila kitu kinachoweza kukukwamisha.

Tatu ni kuzifanyia kazi hizo sababu za kushindwa. Hapo unachukua hatua kuzishughulikia sababu zote zinazoweza kuwa kikwazo kwako.
Hii ni hatua inayohitaji kazi kubwa sana.
Hupaswi kuacha chochote kinachoweza kukuzuia kupata ushindi na ukaja kukitumia kama sababu.

Baada ya hatua hizo, kinachofuata ni kuwa na subira kwenye kupata matokeo.
Matokeo yanapokuja vizuri, unafurahia kwa juhudi zote ulizoweka.
Na pale matokeo yanapokuja vibaya, huwi na majuto wala sababu, kwa sababu unajua umefanya kila kilichopaswa kufanyika.
Kama umeshindwa siyo kwa uzembe wako, bali kwa mambo yaliyo nje ya uwezo wako.

Timu inayotoka uwanjani ikiwa imeshindwa na kutoa sababu za kushindwa ni timu iliyoingia uwanjani ikijua kabisa inaenda kushindwa.
Kama ingekuwa imejiandaa kwa ushindi kamili, isingekuwa na sababu pale inaposhindwa.

Hivyo ndivyo unavyopaswa kuyaendesha maisha yako ya mafanikio.
Hakikisha pale unaposhindwa unakuwa huna sababu yoyote ya kuelezea kushindwa kwako.
Unakuwa umetumia sababu zote kabisa.
Hilo linakutaka ujitume kupitiliza, zaidi ya wengine wote wanavyojituma.
Halafu kitu kizuri ni kadiri unavyojituma, ndivyo unavyojiweka kwenye nafasi nzuri zaidi ya kupata ushindi kwa uhakika.

Unaweza usiamini hili, lakini wewe mwenyewe umekuwa unajihujumu usishinde.
Unajua kabisa sababu zotakazochangia kushindwa, lakini bado huzifanyii kazi.
Na pale inapotokea umeshindwa, unatumia sababu hizo hizo, ambazo ulizijua tangu mwanzo ila hukufanya chochote.

Unakuwa kama mwanafunzi ambaye hasomi, halafu anapofeli mtihani anajiambia kama angesoma angefaulu.
Kwani nini kilimzuia asisome?
Mwanafunzi kazi yake si kusoma?

Ukiifanya kazi yako vizuri, kwa kutekeleza kila kinachopaswa kutekelezwa, unakuwa umetumia sababu zote za kushindwa.
Unakuwa umejiweka kwenye nafasi kubwa ya kupata ushindi.
Na hata kama hutapata ushindi, hutakuwa na majuto yoyote.
Badala yake utaendelea na kufanya yaliyo sahihi mpaka upate unachotaka.

Ukishindwa hakikisha huna sababu.
Ukishakuwa tu na sababu ya kushindwa, basi jua umejitakia wewe mwenyewe kushindwa.
Unakuwa hujaifanya kazi yako kwa uhakika.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe