3150; Tatu ndani ya moja.

Rafiki yangu mpendwa,
Unaweza kudhani tayari unajua kila kitu kuhusu matumizi bora ya muda wako kwenye kupata uzalishaji na ufanisi mkubwa.
Lakini hivyo sivyo ilivyo.
Bado kuna mengi hujayajua kwenye matumizi bora ya muda.
Na kupata uzalishaji na ufanisi mkubwa kwenye muda ni kitendawili kikubwa kwa watu wengi.

Mwanafalsafa Seneca amewahi kunukuliwa akisema kwamba tatizo la muda siyo kwamba ni mchache na haututoshi, bali ni mwingi sana mpaka tunaupoteza.
Na huo ndiyo ukweli.
Inapokuja kwenye muda, tunapoteza zaidi muda kuliko muda kutokutosheleza.
Kwa kifupi kila mmoja wetu kuna muda anaopoteza, ambao akiutumia vizuri, ataweza kuwa na tija zaidi.

Siku yetu kwa kawaida ina masaa 24.
Wengi huyagawa masaa ya siku kwenye makundi matatu ya masaa 8.
Kundi moja ni masaa 8 ya kazi, kundi jingine masaa 8 ya kulala na yanayobaki 8 kwa ajili ya mambo mengine.
Tayari tunajua kwa ukubwa wa malengo tuliyonayo, hatuna anasa ya kutumia masaa 8 ya siku kwenye mambo mengine.
Hivyo tunaboresha na kuwa na masaa 16 ya kazi na 8 ya kulala.
Lakini pia tunajua kulala masaa 8 kwa siku ni anasa ambayo hatuwezi kuimudu.
Hivyo tunaweza kuboresha zaidi na kupata masaa 18 ya kazi na masaa 6 ya kulala, muda ambao ukitumika vizuri unatosha kabisa.

Sasa basi, tunaona hapo tuna muda mwingi wa kazi kwenye siku, masaa 18.
Kwa kuyahesabu ni mengi sana, ambayo unaweza kupanga kufanya mengi na makubwa.
Lakini inapokuja kwenye uhalisia, ni vigumu sana kuweza kuwa na uzalishaji na ufanisi kwa masaa yote 18 ya siku.
Tunapoianza siku huwa tunakuwa na nguvu kubwa, na hivyo kuweza kufanya makubwa.
Lakini kadiri muda unavyokwenda tunachoka na hivyo uzalishaji na ufanisi vinapungua.
Hapo ndipo tunapojikuta tuna muda mwingi, lakini pia tunaupoteza.

Njia ya kuondokana na changamoto hiyo ya kupoteza muda kunakotokana na uchovu wa urefu wa siku ni kuigawa siku yako moja kuzalisha siku 3.
Unayagawa masaa 18 ya kazi kwenye siku kupata siku 3 za masaa 6 kila moja.
Hivyo ndani ya siku moja, unazalisha siku 3 za kazi.

Unachofanya ni kuhesabu kila kipande cha masaa 6 kama siku iliyojitosheleza, ambayo unaipangilia vizuri na kuitumia kwa tija.
Kwenye siku ya kawaida ya watu wengi ambayo ina masaa 8 ya kazi, muda ambao wanautukia kwenye kazi kweli hauzidi masaa 4 na hapo ni kwa wale wanaojitahidi kweli.
Walio wengi wanafanya kazi yenye tija kwa masaa mawili halafu muda mwingine wanaupoteza kwa mambo yasiyo na tija.

Wewe unachofanya ni kupangilia kila kipande cha masaa 6 kwa ukamilifu wake. Unatumia kipande hicho kwa ufanisi kama ulivyopanga.
Ukimaliza unahamia kwenye kipande kingine kama vile ni siku mpya.
Faida ya hilo ni kubadili mtazamo wako kwenye muda.
Badala ya kuona una siku ndefu na hivyo kuridhika kiasi cha kupoteza muda, unaona una siku fupi na hivyo kuthamini zaidi muda.

Zoezi kubwa tunalofanya hapo kwenye kuigawa siku moja ya kazi kupata siku 3 ni kuichezea akili yetu ili iweke thamani kubwa zaidi kwenye muda ambao tunao.
Ukiwa na masaa 18 yaliyounganika ya kazi kwa siku, ukishafanya kama masaa 10 kwa uhakika, 8 yanayobaki huwa yanapotea sana.
Kwa sababu akili yako inaona tayari imeshafanya mengi sana na hivyo kuchoka.
Lakini unapokuwa umegawa kwa masaa 6, akili inakiangalia kipande hicho tu na hivyo huridhiki kama hakuna chenye tija ulichozalisha kwenye huo muda.

Naomba nisisitize, hakuna chochote tunachobadili kwenye muda wetu wa kawaida wa kazi.
Bado masaa ni yale yale ambayo tayari tunayatumia sasa.
Tunachofanya hapa ni kucheza na akili zetu ili tuwe na uzalishaji na ufanisi mkubwa kwenye hayo hayo masaa ya siku.

Kwa mfano, wengi wetu masaa yetu 18 ya kazi kwa siku yanaanzia saa 10 alfajiri mpaka saa 4 usiku.
Hata kama hufanyi kazi kwenye hayo masaa yote, huo ndiyo muda unaokuwa macho, yaani hujalala.
Wengi tunalala kuanzia saa 4 usiku mpaka saa 10 alfajiri.

Sasa ukiiangalia saa 10 alfajiri mpaka saa 4 usiku ni muda mrefu mno, ambapo inakuwa rahisi sana kupoteza muda hapo katikati.
Asubuhi na mchana unaweza kufanya vizuri, lakini jioni na usiku unaweza usiweze kuhesabu nini chenye tija unachokuwa umekamilisha.

Lakini kwa kugawa muda huo huo kwenye siku tatu, unapata kama ifuatavyo;
Siku ya kwanza ni kuanzia saa 10 alfajiri mpaka saa 4 asubuhi (4 AM – 10 AM)
Siku ya pili ni kuanzia saa 4 asubuhi mpaka saa 10 jioni (10 AM – 4 PM)
Siku ya tatu ni kuanzia saa 10 jioni mpaka saa 4 usiku (4 PM – 10 PM)
Saa nne usiku mpaka saa 10 alfajiri (10 PM – 4 AM) unakuwa muda wa kulala ambao haupaswi kuingiliwa na chochote.

Hapo sasa unahakikisha kwenye kila siku yako ya masaa 6 kwenye siku tatu zilizo ndani ya siku moja unakuwa na uzalishaji na ufanisi mkubwa.
Unapomaliza hicho kipande cha masaa 6 unahesabu kabisa yale uliyofanikisha.
Kisha unaingia kwenye kipande kingine kama siku mpya kabisa.
Unaacha kuhesabu vipande vilivyopita na kuangalia hicho kimoja pekee.
Unahakikisha kwenye kila kipande unaweza kuhesabu kabisa yapi makubwa uliyoweza kukamilisha.

Kwenye kila kipande cha siku ya masaa 6, unakigawa kulingana na majukumu yako.
Lakini pia kuhakikisha ndani ya kila kipande cha masaa 6, unakuwa na muda wa kupumzika usiopungua nusu saa na usiozidi saa moja.
Unaweza kutenga muda wa kupumzika kuwa mmoja na mwishoni mwa kipande cha masaa 6.
Au unaweza kugawa muda wa kupumzika kwa vipande.
Kwa mfano dakika 100 za kazi zikifuatiwa na dakika 20 za mapumziko. Ukifanya hivyo mara 3 umemaliza kipande cha masaa 6.
Hivyo kwa kila kipande ukipanga majukumu makubwa matatu na kuweka umakini wako wote kwenye hayo, utakuwa na uzalishaji na ufanisi mkubwa sana.

Usiwe na muda mwingi wa kazi kwenye siku na kuishia kuupoteza kwa mtazamo wa urefu, uchovu na kuona umefanya mengi.
Bali ugawe muda wako wa siku kwenye vipande vitatu na kila kipande kihesabie kama siku inayojitegemea na hivyo kuhakikisha unaiishi kwa ukamilifu wake.

Kama vipande vya masaa 6 ni virefu kwako, nenda na vipande vya masaa 5, bado ukifanya mara 3 ni masaa 15 ya kazi. Ukiyatumia kwa tija utapata uzalishaji na ufanisi mkubwa.
Na kama siku yako inaenda tofauti na hiyo ya kuanza saa 10 alfajiri, nenda nayo vile unavyoanza.
Mfano kwa tunaoanza siku saa 9 alfajiri, unaenda nayo hivyo hivyo kwa vipande vya masaa 6.

Utakachopata kwa kufanyia kazi mkakati huu wa kuigawa siku moja kupata siku tatu ni ndani ya wiki moja utaweza kukamilisha yanayowachukua wengine mwezi mzima.
Na ndani ya mwaka mmoja utakamilisha ambayo yangechukua miaka mitatu.
Sasa hebu jiulize ni hatua kubwa kiasi gani utakazopiga kama ndani ya mwaka mmoja utafanikisha mambo yanayochukua miaka matatu?
Kwa hakika tunao uwezo wa kufanya makubwa mno kama tutaweza kudhibiti na kutumia muda wetu vizuri.

Ukisoma ukurasa huu kwa haraka unaweza kumaliza na ukawa hujaelewa kipi cha kuondoka nacho na kwenda kufanyia kazi.
Hivyo kama umesoma na kufika hapa, rudi tena uanze kusoma kwa umakini mkubwa na kwa sauti.
Kisha kaa na uigawe siku yako moja kwenye siku 3 za kikazi.
Halafu shirikisha kwenye maoni hapo chini jinsi ulivyogawa siku yako na jinsi utakavyohakikisha kila siku ya ndani ya siku inakuwa na tija kubwa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe