3152; Umajinuni na ulazima.

Rafiki yangu mpendwa,
Wakati nipo shule ya udaktari, kwenye kitengo cha magonjwa ya akili tulijifunza magonjwa mengi na sifa zake.
Tulikuwa na tabia ya kutaniana ukiambiwa lazima upate ugonjwa mmoja wa akili mtu utachagua upo?

Magonjwa ya akili yapo mengi kitabibu. Lakini kimazoea watu mpaka waone mtu anaokota makopo ndiyo wanasema ana ugonjwa wa akili, au kama wanavyoita kichaa.

Magonjwa mengi ya akili huwa hayaonekani kwa nje, bali huwa yapo ndani ya mtu. Mtu anakuwa na ugonjwa wa akili pale anaposhindwa kudhibiti akili yake mwenyewe.

Moja ya magonjwa ya akili ambayo huwa siyo rahisi kuonekana kwa nje, hasa kwenye hatua za awali ni magonjwa yanahohusisha hisia (mood)
Na hayo huwa yana pande mbili (bipolar).
Upande mmoja ni hisia za huzuni sana ambazo zinapelekea ugonjwa wa sonona (depression).
Na upande wa pili ni hisia za furaha sana ambazo zinapelekea ugonjwa wa mtu kuwa na msukumo wa kufanya zaidi (mania).

Sasa basi, tukirudi kwenye utani wa hapo juu, nilikuwa nasema kama nitaambiwa lazima niwe na ugonjwa mmoja wa akili, basi nitachagua huo wa mania.
Kwani watu wenye ugonjwa huo huwa wanakuwa na mawazo mengi, wanafanya mambo mengi na hawazuiliki.
Japo kuna hatua inafika huo msukumo unakuwa na madhara kwao, mfano kukosa usingizi na hatimaye kurudi kwenye upande wa pili wa sonona.

Nilichoendelea kujifunza ni kwamba watu wengi waliopata mafanikio makubwa, huwa wana kiwango kidogo cha hayo magonjwa ya akili, hasa huo wa mania.
Kwa jinsi mafanikio makubwa yalivyo magumu, mtu mwenye akili timamu hawezi kuhangaika nayo, au hata kuyavumilia.

Kabla hatujaendelea nikuhakikishie hapa kuna namna sisi tuliopo hapa akili zetu hazipo sawa kwa vipimo vya watu wa kawaida.
Kama akili zetu zingekuwa zinafikiri kama wengi wanavyofikiri, tusingejitesa kwa namna hii.
Kuna namna tuna ukichaa mdogo na hilo ni sawa kabisa.
Hivyo pale wengine wanaposikia mipango yako na kuangalia hatua unazochukua na kukuambia umechanganyikiwa, unaweza kuwajibu wamechelewa sana kung’amua hilo.

Hapa kuna ugonjwa mwingine wa akili ambao ninataka ujitengenezee na kuudhibiti ili uweze kufanya makubwa sana kwenye maisha yako.
Ugonjwa huo unaitwa Obsessive and Compulsive Disorder (OCD).
Ugonjwa huo una dalili za mtu kuwa na mapenzi makali juu ya kitu (Obsession) au umajinuni na msukumo wa kuchukua hatua pale kitu hakijakaa sawa (Compulsion) au ulazima.

Nikupe mfano ili tuelewane vizuri. Kila mtu anamjua mtu ambaye anaweza kufunga mlango na kutoka, kisha akafika njiani na kujiuliza kama amefunga au la. Anashindwa kuendelea na safari yake mpaka arudi kuhakikisha amefunga mlango. Hiyo ni ngazi ya chini ya ulazima (Compulsion), unakuwa ugonjw ambaya pale mtu anapotoka na bado akarudi tena kuhakikisha kama amefunga, hata baada ya kuhakikisha, bado atarudi tena. Yaani mtu anaweza kushindwa kuendelea na kitu kingine kwa sababu ya hilo.

Mfano wa pili ni mtu anayekuwa amepanga vitu vyake kwa namna fulani, ukienda kubadilisha anakasirika na kurudisha kama alivyokuwa amepanga. Yaani hata ukisogeza kitu kidogo tu, hatakaa sawa mpaka amerudisha kama ilivyokuwa. Hivyo ndivyo umajinuni (Obsession) inavyokuwa.

Umajinuni (Obsession) ni kuwa na mapenzi makubwa sana juu ya kitu kiasi kwamba huwezi kujizuia katika kukifanya. Unakuwa kama umeingiwa na pepo juu ya kitu hicho. Unaweza kukifuatilia na kukifanya kwa muda mrefu bila kuchoka.
Unaweza hata kusahau kula pale unapokuwa unafanya kitu hicho.
Hakuna starehe yoyote inayoweza kukuondoa kwenye kufanya kitu hicho.

Ulazima (Compulsion) ni msukumo wa kuchukua hatua juu ya kitu kwa wakati huo huo bila kusubiri. Ulazima ndiyo unaokusukuma kuchukua hatua haraka kwenye mambo muhimu bila kuahirisha.
Unapokuwa na ulazima kwenye kitu, huwezi kabisa kuahirisha. Hupati utulivu ndani yako mpaka umekamilisha kufanya.

Sehemu ambayo nataka wote tuwe na huu ugonjwa ni kwenye mchakato wa Bilionea Mafunzoni.
Nataka tuwe na umajinuni (Obsession) kwenye huu mchakato. Tuupende na kuukubali sana kuliko kitu kingine chochote. Uwe kipaumbele cha kwanza kwetu na kusiwe na kitu au mtu yeyote anayeweza kututoa kwenye mchakato huu.

Kisha tuwe na ulazima (Compulsion) kwenye kuchukua hatua za mchakato huu wa Bilionea Mafunzoni. Tusukumwe sana kuchukua hatua kiasi cha kukosa kabisa utulivu kama hatujachukua hatua. Isiwe rahisi kwetu kuahirisha kuchukua hatua ambazo tumepanga.
Hata pale tunapokutana na changamoto na vikwazo mbalimbali, bado hatukubali kuacha kutekeleza mchakato wetu. Kwa sababu msukumo ulio ndani yetu hauwezi kutulizwa na chochote.

Umajinuni (Obsession) na Ulazima (Compulsion) ni vitu viwili ambavyo ukiwa navyo unakuwa mtu hatari sana kuweza kujenga mafanikio makubwa ambayo wengi hawawezi hata kuyaota.
Wengi wanachukulia hayo mawili kama ugonjwa kwa sababu wanashindwa kuyadhibiti. Lakini wewe ukiweza kuyadhibiti, yatakuwa baraka kubwa sana kwako.

Kuwa na mapenzi makubwa (Obsession) juu ya kitu kiasi cha kukifikiria muda wote na kuwa na msukumo (Compulsion) wa kufanya kitu hicho bila kukubali kuahirisha kwa namna yoyote ile. Hivyo ndivyo unavyoweza kujenga mafanikio yoyote makubwa unayotaka kuwa nayo kwenye maisha yako.
Na kama watu watakuambia umechanganyikiwa, wacheke, kwa sababu hakuna mwenye akili timamu aliyeweza kufanya mambo makubwa hapa duniani.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe