3155; Uhitaji na Upatikanaji.

Rafiki yangu mpendwa,
Msingi mkuu wa uchumi umejengwa kwenye kanuni ya Uhitaji na Upatikanaji (Demand and Supply).
Kanuni hiyo inasema kitu kinapokuwa na uhitaji mkubwa kuliko upatikanaji wake, thamani yake inakuwa kubwa zaidi.

Kwa lugha rahisi ni kwamba kama vitu ni vichache na wanaovitaka ni wengi, bei inakuwa kubwa.
Na kinyume chake ni sahihi, kama upatikanaji ni mkubwa kuliko uhitaji, bei inakwenda chini.

Tupate mfano kabla hatujaenda kwenye namna ya kutumia hii kanuni.
Dhahabu na Chuma yote ni madini.
Yanapatikana ardhini.
Kimatumizi, chuma ina matumizi mengi kwenye maisha ya kila siku kuliko dhahabu.
Lakini cha kushangaza sana, thamani ya dhahabu ni kubwa sana kuliko ya chuma.
Unajua sababu ni nini?
Uhitaji na upatikanaji.
Chuma inapatikana kwa wingi sana, hivyo bei yake siyo kubwa.
Wakati dhahabu inapatikana kwa uchache sana na ndiyo maana bei yake ni kubwa.

Sasa turudi kwenye somo la leo.
Kuna maeneo mengi sana ya kutumia hii kanuni.
Kwa hakika ni kanuni unayopaswa kuitumia kwenye kila eneo la maisha yako.
Kwa kuhakikisha unatengeneza uhitaji mkubwa kuliko upatikanaji uliopo.
Kwa mfano kama unataka thamani ya muda wako iwe kubwa, fanya watu wengi sana watake kupata muda wako kuliko unavyopatikana.
Kadhalika kwa mambo mengine.

Sasa tuingie kwenye somo la leo, ambalo linahusisha kanuni hiyo ya uhitaji na upatikanaji, kwenye eneo la mauzo.
Na eneo la mauzo ni pana, hivyo tutaenda kuangalia eneo la wateja.

Njia ya kupata wateja bora kabisa ambao utafurahia kufanya nao biashara ni kutumia kanuni ya uhitaji na upatikanaji.
Unachotakiwa kufanya ni kutengeneza wateja tarajiwa wengi zaidi ya uwezo wako wa kuwahudumia.

Kwa kufanya hivyo unakuwa umetengeneza uhitaji mkubwa kuliko upatikanaji uliopo. Hilo linatengeneza hali ya uhaba ambayo inawasukuma watu kuchukua hatua ili wasikose.

Unapokuwa na wateja tarajiwa wengi kuliko unavyohitaji, na wote ukawa unawafanyia mchakato wa kuwageuza kuwa kamili, utakuwa na nguvu ya kuchagua ni wateja wa aina gani ufanye nao kazi.
Kwa kuwa huna tamaa ya kupata wateja haraka, utachukua muda kuwachuja ili kupata wale walio bora.

Na wakati unaendelea kupata walio bora, utaweza kuwaondoa wateja ulionao ambao wamekuwa siyo bora kama ulivyokuwa unategemea.
Kwa sababu kila wakati unaendelea kugeuza wateja, ambao huna tamaa nao, utaweza kupunguza wale ambao hutaki kuendelea kufanya nao biashara.

Kuwa na uhitaji mkubwa kuliko upatikanaji uliopo, kunakupa nguvu kuchagua na kubaki na wale walio bora.
Lakini ikiwa kinyume na hayo, yaani ukawa na upatikanaji mkubwa kuliko uhitaji, unalazimika kufanya kazi na kila aina ya wateja, hata kama siyo bora kama ulivyotaka.

Unapokuwa na tamaa ya kupata wateja zaidi kwa sababu uhitaji wako ni mkubwa kuliko upatikanaji uliopo, unakuwa huna namna bali kupokea kila aina ya wateja wanaopatikana.
Kuwa kwenye hiyo hali kutakusukuma ufanye kazi na wateja ambao hufurahii kuwa nao, lakini unakuwa huna namna bali kuwapokea, kwa kuwa huna wateja wengi.

Mara zote hakikisha unao wateja wengi kuliko unavyohitaji.
Halafu pia unakuwa na wateja tarajiwa wengi kuliko unavyohitaji.
Unapokuwa kwenye hizo hali, usiridhike na kuacha mchakato wa kugeuza wateja tarajiwa kuwa kamili.
Badala yake ongeza viwango vya sifa unazoangalia ili kumkubali mtu kuwa mteja.

Wanasema wakati mzuri wa kununua mwavuli ni kabla mvua haijaanza kunyesha. Maana hapo bei yake inakuwa chini na unaweza kuchagua ubora unaotaka.
Lakini mvua inapoanza kunyesha, bei ya mwavuli inakuwa kubwa na utalazimika kuchukua wowote unaopatikana bila kujali ubora.

Wakati mzuri wa kupata wateja bora ni pale unapokuwa huna uhitaji mkubwa wa wateja. Hapo ndipo unapoweza kuweka vigezo vya wateja gani ufanye nao kazi.
Lakini ukisubiri mpaka wateja wako wamepungua ndiyo uanze kutafuta wengine, utalazimika kuchukua yeyote bila kuangalia ubora.

Kuna kauli mbiu moja muhimu sana ambayo kila muuzaji anapaswa kujiambia kila mara. Kauli hiyo ni; Wateja tarajiwa wapo wengi.
Jikumbushe hilo kila mara kisha fanyia kazi kwa kuhakikisha mara zote una wateja tarajiwa wengi unaowatengeneza na kuwafanyia kazi.

Zoezi la kutengeneza wateja tarajiwa kwenye biashara yako linapaswa kuwa endelevu.
Linapaswa kufanyika muda wote bila kupoa.
Hata pale unapoona tayari una wateja wa kutosha, usiache kuendelea na zoezi la kutengeneza wateja wapya tarajiwa.

Mara zote ifanye nguvu ya kanuni ya Uhitaji na Upatikanaji iwe upande wako.
Kwa kuhitajika kwako kuwa kukubwa kuliko upatikanaji wako.
Kwani hata wateja wanapojua wapo wengi kuliko unavyowahitaji, wanathamini kile unachowapa.

Lakini hapo unahitaji vitu viwili vya ziada;
Moja ni kutoa thamani kubwa sana ambayo wateja hawawezi kuipata mahali pengine popote. Yaani kuwapa dili nzuri kabisa ambayo watajiona wajinga kuikataa.
Mbili ni kuwahudumia vizuri kuliko wanavyoweza kuhudumiwa mahali pengine popote.

Kwa hivyo viwili kuwepo muda wote kwa msimamo, huku nafasi zikiwa chache, thamani yako inakuwa kubwa zaidi.
Hilo linakupa nguvu ya kuweza kufanya kazi na aina ya wateja unaofurahia kufanya kazi, huku ukiwapunguza wale ambao hufurahii kufanya nao kazi.

Kuwa na wateja wengi kuliko unavyohitaji.
Wape thamani ambayo hawawezi kuipata kwingine.
Wahudumie vizuri kuliko wanavyoweza kuhudumiwa pengine.
Na mara zote endelea kutengeneza wateja wapya tarajiwa.
Fanya hayo kwa msimamo na utaweza kujenga biashara bora sana kwako, ukiwa na mauzo makubwa huku ukifurahia kile unachofanya.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe