3156; Hakuna ‘ni mara moja tu’.

Rafiki yangu mpendwa,
Huwa tunaweka malengo na mipango mbalimbali ya mambo gani tutafanya na yapi ambayo hatutayafanya.
Tunafanya hivyo kwa nia njema kabisa ya kuweza kupiga hatua ambazo tumepanga kupiga.

Lakini inapokuja kwenye utekelezaji, mambo ndiyo huwa magumu sana kufanya kama ulivyopanga.
Mtu unashawishika kwenda kinyume na utaratibu ambao alijiwekea yeye mwenyewe.

Mtu anafanya hivyo akijiambia ni mara moja tu anafanya au kutokufanya tofauti na alivyokuwa amepanga.
Kitu ambacho mtu anakuwa hazingatii ni kwamba kama mtu akiweza kufanya mara moja, ni rahisi kufanya kwa mara nyingine na nyingine na nyingine zaidi.
Na hapo ndipo mtu anapovunja malengo na mipango aliyokuwa amejiwekea, kwa sahabu tu ya kuanza mara moja.

Ni rahisi sana kusimamia kitu kwa asilimia 100 kuliko kusimamia kwa asilimia 99.
Ukiwa hujavunja yale uliyojipangia inakupa nguvu ya kuendelea bila kuvunja.
Lakini ukishavunja hata mara moja, unashawishika kuvunja tena na tena.

Ukishapanga yale utakayofanya au kutokufanya unapaswa kufuta sababu zote nzuri zinazokushawishi kwenda kinyume na malengo na mipango yako.
Usikubali hata kidogo kwenda kinyume na ulivyopanga.
Kwa sababu ukishavunja mara moja, ni rahisi kuvunja tena na tena.

Hayo tuliyojifunza ni kwa upande binafsi ambapo unapanga na kutekeleza kama ulivyopanga bila kuruhusu sababu zozote kwenda kinyume na mipango yako.

Inapokuja kwenye upande wa kushirikiana na wengine, utaratibu ni huo huo.
Chora mstari ambao hakuna mtu anaruhusiwa kuuvuka.
Unapaswa kuweka mipaka ambayo hakuna yetote anayeruhusiwa kuivunja.
Hapo hutafanya mambo kwa kuruhusu mtu yetote kuvuka mipaka uliyojiwekea.

Watu huwa wana tabia ya kujaribu kuvuka mipaka uliyoweka ili kuona utachukuliaje hilo.
Hivyo kama hujaweka mipaka imara na kuweka madhara pale mtu anaposhindwa kuizingatia, fujo zinakuwa nyingi sana.
Hakuna chochote kikubwa kitakachoweza kufanyika kwa kila mtu kujiamulia vile anavyotaka yeye mwenyewe.

Ukiwaruhusu watu kuvuka mipaka uliyoweka, hata kama ni kidogo tu, wataenda zaidi ya ulivyowaruhusu.
Na hapo unakuwa huna tena ujasiri wa kuwazuia kwa sababu umeshakubali kuvunja kile ulichoweka wewe mwenyewe.
Hapa tena kusimamia kitu kwa asilimia 100 ni rahisi kuliko kusimamia kwa asilimia 99.

Inakuwa na nguvu sana pale unapokuwa kwenye mwendo wa ufanyaji ambao hujavunja vile ulivyopanga.
Kuendeleza msimamo ni rahisi, kwa sababu unatunza sifa ambayo tayari unayo.
Lakini ukishavunja hata mara moja tu, unavunja sifa uliyokuwa umeshajenga kwa msimamo uliokuwa nao.
Baada ya kuvunja sifa na msimamo, mambo yanaanza kwenda hovyo kuliko ilivyokuwa awali.

Mara ya pili kufanya kitu huwa inakuwa rahisi kuliko mara ya kwanza.
Hivyo kama kuna vitu ambavyo hutaku kufanya, hakikisha unajenga sifa imara ya kutokuwahi kufanya vitu hivyo.
Hakikisha hujawahi kufanya kabisa na simamia kuendeleza sifa hiyo bila kuivunja.

Tekeleza yote uliyopanga kwa namna ulivyopanga bila kuruhusu sababu zozote ziingilie.
Tekeleza yale yote uliyowaahidi wengine bila ya kuruhusu sababu zozote zikufanye uvunje ahadi hizo.
Hata kama itakuingia gharama kubwa kukamilisha kama ulivyopanga au kuahidi, fanya tu hivyo kwa sababu ya sifa unayotaka kuendelea kujenga na kulinda.

Usiwe rahisi kuvunja mambo yako uliyopanga au kuahidi wewe mwenyewe.
Usiwaruhusu watu kuvuka mipaka ambayo umewawekea.
Jenga msimamo mkali kwenye maisha yako yote na yale unayofanya na utaweza kufanya makubwa sana.

Ndiyo kwa kusimamia misimamo yako kuna vitu unaweza kukosa, lakini vinakuwa vidogo kuliko unavyokosa kwa kutokusimamia misimamo yako au kwa kutokuwa na msimamo wowote.

Ukishapanga kinachofuata ni utekelezaji, usiruhusu kuvunja hilo kirahisi sana.
Iwe ni wewe binafsi au wengine, hakikisha yote uliyopanga yanaheshimiwa na kutekelezwa bila sababu zozote kuzuia.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe