3157; Akili na Kipaji.

Rafiki yangu mpendwa,
Hapa nina habari nzuri na mbaya kwako.
Na tutaanza na habari mbaya.
Habari mbaya ni kwamba ili upate mafanikio makubwa unahitaji kuwa na akili kubwa na kipaji cha kipekee.
Na ubaya wa habari hiyo ni kwamba hivyo ni vitu viwili ambavyo huwezi kuvibadili.
Huwezi kujiongeza akili wala kujipa kipaji.
Hizo ni habari mbaya na za kusikitisha, kwamba kuna vikwazo unavyoweza kuwa navyo ambavyo vinakuzuia usifanikiwe.

Sasa ni wakati wa kwenda kwenye habari nzuri.
Na habari hizo nzuri ni kwamba kuna vitu unaweza kufanya na ukahakikisha akili na kipaji haviwi kikwazo kwako.
Vitu hivyo vipo ndani ya uwezo wako kabisa kuvifanyia kazi.
Kwa kuchukua hatua kwenye maeneo hayo mawili makuu, inakupa uhakika wa kujenga mafanikio makubwa.

Moja; kama huna akili nyingi, kuwa na shauku kubwa.

“Being enthusiastic is worth 25 IQ points.” –Kevin Kelly
Kevin Kelly alinukuliwa akisema kuwa na shauku ni sawa na alama 25 za akili.
Hiyo ina maana kwamba mtu ukiwa na shauku kubwa, inaondoa kikwazo cha akili kwenye mafanikio.
Unapokuwa na shauku kubwa, unakuwa na nguvu ya kuwashawishi wengine kukubaliana na wewe.
Na uwezo wako wa kuwashawishi watu wengine ndiyo akili muhimu kwa mafanikio.

Mbili; kama huna kipaji, amka mapema.

“I don’t have talent, so I just get up earlier.” – Henry Rollins
Henry Rollins alisema yeye hana kipaji, hivyo huwa anaamka mapema.
Wale wenye vipaji huwa wanafanya mambo kwa urahisi kuliko wasiokuwa na kipaji.
Lakini wasiokuwa na kipaji wakiweza kuweka juhudi kubwa, wanaweza kupata matokeo makubwa kuliko hata wenye vipaji.
Lakini hilo linahitaji sana mtu kuweka kazi kubwa na kwa muda mrefu.
Kwa kuamka mapema na kuweka juhudi za kipekee, utaweza kufanya makubwa kuliko hata wale ambao wana vipaji vikubwa.
Nidhamu kali ya kufanya bila kuacha inakuwezesha kufidia palipopelea kwa kipaji.

Rafiki, tumeona jinsi ambavyo akili na kipaji ni mahitaji muhimu kwenye mafanikio.
Lakini pia tumeona jinsi ya kuhakikisha vitu hivyo viwili haviwi kikwazo kwako kufanikiwa.
Kwa kuwa na shauku kubwa ambayo inakuvusha kwenye akili na kuamka mapema ambako kunakuvusha kwenye kipaji.

Sasa basi, hebu fikiria ukiwa na akili halafu pia ukawa na shauku kubwa, utakuwa wa moto sana.
Kadhalika fikiria una kipaji halafu pia ukawa unaamka mapema na kuweka juhudi kubwa, utafanya makubwa mno.
Amua kufanyia kazi maeneo hayo mawili, iwe unajiona una akili na kipaji au la.
Mara zote juwa na shauku kubwa huku pia ukiamka mapema na kuweka juhudi kubwa.
Lazima utaweza kufanya makubwa sana.

Huwa hatupo vizuri kwenye kujikadiria, hivyo ni vyema kuchukua hatua sahihi iwe tuna sifa au hatuna.
Unapofanya yale yaliyo ndani ya uwezo wako, unajiweka kwenye nafasi ya kupata matokeo bora kabisa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe