3158; Mateso bila chuki.

Rafiki yangu mpendwa,
Tumechagua kuingia kwenye hizi biashara tunazofanya kwa sababu mbalimbali.
Lakini sababu kubwa kabisa ni kupata uhuru kamili kwenye maisha yetu.
Yaani kuanzia kupata uhuru wa kifedha, muda, eneo na watu.

Lakini matokeo ambayo watu wengi wanaoingia kwenye biashara wanayapata ni tofauti kabisa na matarajio wanayokuwa nayo.
Badala ya kupata uhuru ambao wengi waliutaka, wanajikuta wameingia kwenye utumwa mkubwa kuliko hata ule wanaokuwa wameukimbia walipoingia kwenye biashara.

Na hiyo ni kwa sababu wanakuwa wamechagua mateso na chuki.
Iko hivi rafiki, kuanzisha, kujenga na kukuza biashara yenye mafanikio ni mateso makubwa sana.
Ni kitu ambacho kinakutaka mtu ujitoe kweli kweli na utoe kafara mambo mengi kwenye maisha yako.
Unakubali kupitia mateso hayo kwa sababu ya matumaini ya kupata uhuru unayokuwa nayo.

Lakini sasa, tunajikuta siyo tu tunapata mateso, bali na chuki pia inaingia katikati.
Yaani tunajikuta tunapitia mateso huku tukiwa tunachukia hali hiyo.
Na hilo linasababishwa na baadhi ya watu ambao wanayazidisha mateso tunayoyapata kwenye kujenga biashara.

Kwenye kuanzia na kujenga biashara yako, unalazimika kushirikiana na watu mbalimbali.
Inaweza kuwa washirika wako wa kibiashara, wanaokusambazia vitu, wafanyakazi au wateja.
Huwezi kuwakwepa watu kwenye kuanzisha na kujenga biashara yenye mafanikio makubwa.

Watu wanakuwa chanzo cha chuki pale wanapokuwa siyo waaminifu na wala huwezi kuwategemea.
Kwa njia hiyo watu hao wanakuwa wanakuangusha kila mara, hasa pale unapokuwa unawategemea zaidi.

Tunajikuta kwenye hiyo hali ya kuwa na chuki zinazotokana na watu kwa sababu tumekuwa tunamkubali kila mtu kwenye biashara zetu.
Kwa sababu tunataka sana kukua na kufanikiwa kwenye biashara, tunaona kama kuna uhaba wa watu na hivyo kuchukua yeyote anayejitokeza.

Tunashindwa kuweka vigezo ambavyo watu tunaoshirikiana nao lazima wawe navyo.
Kwa kukosa vigezo tunamkubali kila mtu na mwisho wake tunajikuta kwenye nyakati ngumu zinazotufanya tuzichukie biashara.

Ili kuondoka kwenye hiyo hali ya kujikuta kwenye mateso yenye chuki, weka vigezo vya kuwachuja watu na vitumie kuwakataa watu wengi kuliko unaowakubali.
Unafanya hivyo kwa watu wote unaoshirikiana nao, kuanzia wabia wa kibiashara, wasambazaji, wafanyakazi na hata wateja.

Shirikiana na wale tu ambao ni waaminifu na wanaweza kutegemewa kwa asilimia 100 bila ya shaka yoyote ile.

Kwa wabia wa kibiashara, wanatakiwa kuwa na maono makubwa kwenye maisha yao yanayoendana na maono makubwa ya biashara. Pia wanapaswa kuwa watu wanaocheza mchezo wa muda mrefu na siyo wanaotafuta njia za mkato na kupata matokeo ya haraka bila kuweka kazi.

Kwa wasambazaji, unapaswa kujihusisha na wale wanaoahidi kile wanachotimiza, kwa usahihi na kwa wakati. Ni muhimu na wao pia wawe na maono makubwa na kukuona wewe kama sehemu ya wao kufikia maono yao makubwa.

Kwa wafanyakazi ndiyo pagumu, kwa sababu hao ni watu utakaowategemea zaidi. Kama wasipokuwa waaminifu na wa kutegemewa, kuendesha biashara kutakuwa kwa mateso makubwa na yenye chuki. Uaminifu ni sifa ya kwanza na muhimu sana kuangalia na kuzingatia. Hii ikishavunjwa tu kwa namna yoyote, hupaswi kumvumilia mtu. Halafu kuna sifa nyingine muhimu kama kujituma kwenye majukumu ya kazi na kushirikiana vizuri na watu wengine.

Kwa watena ndipo penye changamoto kubwa zaidi. Kwa kuwa tunataka kuuza, tunaona kila anayehitaji kununua basi ni mteja sahihi kwetu.
Na hapo ndipo tunapokaribisha mateso yenye chuki kubwa.
Wateja ambao hawaioni wala kuijali thamani kubwa unayotoa huwa ni wateja ambao wanakupa mateso makubwa zaidi.
Ni muhimu sana kuwachuja wateja unaojihusisha nao kwa kuangalia jinsi wanavyochukulia thamani unayoitoa.
Kama hawaithamini kwa namna unavyotaka, achana nao mara moja.

Sehemu kubwa ya changamoto tunazokutana nazo kwenye maisha yetu huwa zinaanzia kwa watu.
Tukiweza kutatua hilo la watu, tutabaki na mateso ya kawaida kwenye biashara ambayo hayatupeleki kwenye chuki.

Warren Buffet anasema unapoangalia mtu wa kushirikiana nao, angalia sifa tatu; akili (intelligence), nguvu/afya (energy) na uaminifu/uadilifu (integrity).
Hakuishia tu hapo, bali akaendelea kusisitiza akisema, kama mtu hana hiyo sifa ya tatu, sifa mbili za kwanza zitakumaliza kabisa.

Kwa maneno mengine ni uaminifu na uadilifu inapaswa kuwa sifa namba moja kwa watu wote unaojihusisha nao.
Na uaminifu na uadilifu huo huupimi tu kwa namna wanavyochangamana na wengine, bali hata wanavyokwenda wao binafsi.
Mtu anapaswa kuwa na maisha ya aina moja, akiwa faraghani au hadharani.
Mtu akishakuwa na maisha ya tofauti faraghani na hadharani, anakuwa na changamoto kubwa zaidi.

Mwisho kabisa, kile ambacho tunakitaka kwa wengine, lazima sisi wenyewe tuwe nacho pia.
Kutegemea wengine wakupe kile ambacho umeshindwa hata kujipa mwenyewe ni kujidanganya.

Chagua kushirikiana na watu sahihi ili kuanzisha na kujenga kwako biashara kuwe ni mateso yasiyokuwa na chuki.
Utaweza kufanikisha hilo kwa kuwachuja watu wote kulingana na vigezo ulivyojiwekea.
Hakikisha unaowakataa ni wengi kuliko unaowakubali.
Na kamwe usiseme hakuna watu sahihi kwako.
Wapo wengi sana, anza kwa wewe kuwa sahihi kisha kataa wote ambao hawafikii usahihi unaoutaka wewe.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe