3161; Nipe nikupe haitoshi.

Rafiki yangu mpendwa,
Sehemu kubwa ya mahusiano yetu sisi binadamu yamejengwa kwenye msingi wa nipe nikupe.
Kwa sababu kwa asili watu ni wabinafsi, ambao wanajali zaidi maslahi yao kuliko maslahi ya watu wengine.

Kupitia hilo la watu kujali zaidi maslahi yao binafsi, ndiyo kanuni kuu ya ushirikiano na watu wengine imetengenezwa.
Kanuni hiyo ni nipe nikupe.
Kwa kanuni hii, mtu unatoa kwanza kitu kwa wengine, kwa mategemeo ya wao kukupa kikubwa zaidi.

Ni kanuni inayofanya kazi vizuri na imekuwa na manufaa mazuri kwa wote ambao wamekuwa wanaitumia vizuri.
Kwa sababu pale watu wanapopata kitu, wanajiona wakiwa na deni la kutakiwa kurudisha kwa wale waliowapa.

Vipi kama nikikuambia kuna kanuni nyingine yenye nguvu kuliko nipe nikupe?
Vipi kama nikikuambia kanuni hiyo ndiyo inawatofautisha wale wanaopata mafanikio makubwa na wanaopata mafanikio makubwa?

Ni kweli ipo kanuni yenye nguvu kuliko nipe nikupe kwenye mahusiano baina ya watu.
Kanuni hiyo ni NAKUPA USHINDI.
Kanuni ya nipe nikupe imekaa kimtego, unampa mtu kitu, halafu baada ya hapo unamtaka naye akupe kitu.
Wenye uelewa wanakuwa wanapata wasiwasi pale unapowapa kitu, wakijiuliza ni kitu gani utakachowataka wakupe.
Na hilo kinadhoofisha nguvu ya NIPE NIKUPE.

Kanuni ya NAKUPA USHINDI inalenga kuwapa watu wengine ushindi kwenye maisha yao.
Kwa kanuni hiyo unachofanya ni kuhakikisha unawasababishia watu ushindi mkubwa kwenye maisha yao.
Hivyo kinachofanyika ni kuchagua ni ushindi gani unaoona watu wanaweza kuupata kisha kuwekeza kila kilicho ndani ya uwezo wako kuhakikisha watu wanapata ushindi huo.

Kwa kanuni hii huangalii umetoa nini wala kupata nini.
Unachoangalia ni ushindi gani ambao mtu amepata.
Huwaambii watu wakupe vitu fulani kwa sababu kuna vitu umeshawapa.
Badala yake unakazana kuwapa watu ushindi ambao hawawezi kuusahau kwenye maisha yao.

Manufaa ya kanuni hiyo yapo kwenye utegemezi mkubwa unaokuwa umeujenga kwa watu.
Kwa sababu umewapa ushindi na watu wanapenda kupata na kubaki na ushindi, hawatataka kukupoteza.
Hivyo wataendelea kuimarisha mahusiano na wewe, ili waendelee kupata na kubaki kwenye ushindi mkubwa.
Na hapo ndipo wanapokuwa tayari kukupa kwa ukubwa kuliko ambavyo ungewataka wakupe.

Kwa kuwa ushindi unahitaji mtu aweke juhudi binafsi pia, unalazimika kuwachuja vizuri watu kabla hujawaingiza kwenye mkakati wako wa NAKUPA USHINDI.
Unawachagua wale ambao wana kiu kubwa ya kupata ushindi na wamejitoa kwa kila namna kupata ushindi huo.
Yaani wanakuwa tayari kufanya kila kinachohitajika kufanyika ili ushindi upatikanani.
Kwa wavivu na wazembe, ambao wanataka ushindi wa haraka bila kuweka kazi, kanuni hiyo haiwezi kufanya kazi kwao.

Hivyo basi rafiki yangu,
1. Jua maeneo ambayo unaweza kuwasaidia watu wengine kupata ushindi mkubwa.
Maeneo yenye nguvu kwako ni yale ambayo kwako ni kama mchezo wakati kwa wengine ni majukumu makubwa na ya mateso.
2. Kisha chagua watu ambao wana kiu kubwa ya mafanikio, ambao wamejitoa kuhakikisha wanapata ushindi wanaoutaka.
Hawa ni wale ambao siyo wavivu wala wazembe, bali wanaoamini kwenye mchakato sahihi.
3. Jua maeneo ambayo watu hao wanakwama kwenye kupata ushindi.
Maeneo hayo yanakuwa ni vikwazo mbalimbali wanavyokuwa navyo, ambavyo wao wenyewe wanakuwa hawavioni.
4. Wasaidie kuondoa vikwazo hivyo na kuhakikisha wanapata ushindi.
Hapa unajipa wajibu wa kuhakikisha wanapata ushindi mkubwa kwenye maisha yao.
Matokeo unayoyataka wewe ni wao wapate ushindi kwanza, mengine zaidi ya hapo huyaruhusu yawe usumbufu kwako.

Swali unaloweza kuwa unajiuliza vipi kama nikiwapa watu ushindi na wasiwe tayari kurudisha chochote kwangu?
Majibu ni mawili;
1. Hujawapa ushindi mkubwa kama unavyodhani.
2. Wewe mwenyewe huna ushindi wa kutosha kwenye maisha yako.
Ukiwa na ushindi wa kutosha kwenye maisha yako na ukawapambania wengine kupata ushindi, hakuna namna utashindwa.

Ushindi wangu ni wewe ushinde.
Je umejitoa vya kutosha kupata ushindi mkubwa kwenye maisha yako?
Je upo tayari kuachana kabisa na uvivu na uzembe ili uweze kufanya kila kinachohitajika kufanyika ili kupata ushindi?
Kwa sababu ninachofanya ni kukuondolea kila aina ya kikwazo kilicho kati yako na ushindi wako, ili uweze kuufikia kwa uhakika.
Sikupi ili unipe, bali nakupa ushindi wa uhakika.

Hivyo vigezo hapo juu huwa siyo vya kusema kwa maneno au kuahidi.
Ni vitu vinavyokuwa ndani ya mtu au kutokuwepo.
Unaweza kuwa unatamani sana, lakini ikawa tu vigezo ndani yako havipo.
Na hapo ndipo unapohitajika kujisukuma mno ili kujenga vigezo hivyo.
La sivyo asili inakuweka kwenye fungu la kukosa.

Je utafanya kazi yako au utaiachia asili ifanye kazi yake?

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe