Barua ya XVIII; Kuhusu sherehe na kufunga.

Rafiki yangu Mstoa,
Kwenye mwaka huwa kuna miezi ambayo huwa ina sherehe nyingi.
Ni miezi ambayo watu hupumzika kabisa kazi zao na kusherekea.
Katika kipindi hicho, watu hula na kunywa mpaka kusaza.
Hiyo huwa ni miezi ambayo watu hushindwa kujizuia hasa kwenye nidhamu walizokuwa wanajijengea.
Mfano mtu ambaye alikuwa amepanga kupunguza au kuacha pombe, kwenye miezi ya sherehe anajikuta akiwa na wakati mgumu kwenye hilo.

Hii siyo hali mpya, bali imekuwepo kwa muda mrefu. Kwenye barua yake ya 18 kwa rafiki yake Lucilius, mwanafalsafa Seneca alimweleza jinsi ya kuendana na kipindi cha sherehe ili kutovuruga nidhamu yao ya falsafa ya Ustoa.

Karibu tujifunze mambo ya kuzingatia kwenye hizo nyakati, kwani kwenye zama hizi zimekuwa ni nyingi.
Zamani ilikuwa ni miezi ya mwisho wa mwaka, ila sasa ni siku za mwisho wa wiki.
Yaani ni kama vile kila mwisho wa wiki kuna sherehe mbalimbali, ambazo zinakuweka kwenye mtego wa kuvunja nidhamu ulizopanga kujijengea.
Kukabiliana vyema na hali hizi, tuzingatie yale ambayo Seneca anatufundisha kwenye barua hii.

1. Unaweza kusherekea bila anasa.

Seneca anaanza barua hii kwa kueleza njia mbili za kukabiliana na hali ya sherehe ambazo zinawachukua watu kwa mkumbo.
Njia moja ni kufuata mkumbo na kufanya yale ambayo wengine wanafanya. Hapo unakuwa umevunja kabisa nidhamu ya Kistoa ambayo umekuwa unajijengea.
Njia nyingine ni kuepuka kabisa kusherekea, ambapo utatunza nidhamu yako, lakini utaibua upinzani mkali kutoka kwa wengine, kitu ambacho kitaleta usumbufu kwako.

Njia bora ambayo Seneca anashauri siyo kati ya hizo mbili, bali ya katikati, ambayo ni kusherekea bila ya kufanya anasa.
Kwa njia hiyo huvunji nidhamu yako, lakini pia hukaribishi usumbufu wa watu kwako.

Hivi pia ndivyo tunavyopaswa kufanya kwenye misingi yote ya Kistoa tunayochagua kuiishi. Tusiivunje kwa kufuata mkumbo wa wengi na wala tusijionyeshe sisi ni bora kuliko hao wengi kwa sababu tuna hii misingi.
Badala yake tuchague kuiishi misingi hiyo kwa namna yenye manufaa kwetu na tuwaache wengine wakigangaika na kufuata mkumbo.
Tukiingia tu kwenye mtego wa kutaka kuwaonyesha wengine wanakosea kwa mkumbo wanaofuata, watatusumbua mpaka tushindwe kuiishi misingi yetu.

Hatua za kuchukua;
Chagua kuiishi misingi ya Ustoa kwa namna ambayo ina manufaa kwako na waache wengine wahangaike na mambo yao.
Usiungane nao kwa kufuata mkumbo na wala usiwapinge kwa kuwaonyesha wanakosea.
Wewe hangaika na mambo yako na waache wengine wahangaike na yao.
Na wale wanaokuja kwako wakitaka kuishi kwa misingi kama yako ndiyo utawashirikisha.

Nukuu;
“It shows much more courage to remain dry and sober when the mob is drunk and vomiting; but it shows greater self-control to refuse to withdraw oneself and to do what the crowd does, but in a different way, – thus neither making oneself conspicuous nor becoming one of the crowd. For one may keep holiday without extravagance.” – Seneca

“Inaonyesha ujasiri kuwa timamu pale wengine wamelewa; lakini inaonyesha udhibiti binafsi kutokujitenga na wengine kabisa lakini pia kutokufanya wanayofanya, – hivyo huungani na kundi na wala hulipongi. Kwa sababu unaweza kusherekea bila anasa.” – Seneca

2. Dawa ya hofu ni kufanya unachohofia.

Seneca anagusia eneo jingine ambalo limekuwa mzigo kwa watu wengi.
Eneo hilo ni hofu ambayo watu wanakuwa nayo kuhusu umasikini.
Pale mtu anapotengeneza utajiri, badala ya kuwa huru na kuufurahia, unageuka kuwa mateso kwake kwa kuhofia kupoteza utajiri huo na kurudi kwenye umasikini.
Kwenye hali hiyo Seneca anatukumbusha dawa ya hofu ni kufanya kila unachohofia.
Na kwenye hofu ya umasikini, dawa na kuuishi umasikini.

Seneca anasema unapaswa kutenga siku ambazo utaishi kimasikini kabisa, kama vile umepoteza kila ulichonacho.
Halafu unajiuliza, je hiki ndiyo ninachohofia?
Unakula chakula cha chini kabisa na wakati mwingine kutokula kabisa.
Unavaa nguo za bei rahisi kabisa na kuishi kwa gharama za chini kama masikini wengi wanavyoishi.
Utakachokipata kwenye zoezi hilo kitakuwa kikubwa sana.
Kwanza utagundua mambo hayatakuwa magumu kama ulivyokuwa unayahofia.
Na mbili utaweza kuthamini na kufurahia kila ulichonacho kwa wakati unacho kwa sababu unajua unaweza kupoteza kila kitu.

Seneca anatutahadharisha tunapofanya zoezi hilo la kujaribu umasikini tusijione kama tumefanya zoezi la kishujaa sana.
Kwa sababu kuna watu wengi hayo ndiyo maisha yao ya kila siku na yanaenda.
Hili ni zoezi la kukuimarisha wewe uli usibweteke na ulivyonavyo na hofu kukuzuia usifurahie ulivyonavyo kwa kuhofia kuvipoteza.

Hatua ya kuchukua;
Pamoja na vitu vyote ulivyonavyo vya kukuwezesha kuyarahisisha maisha yako, tenga siku ambazo utaishi bila kutumia vitu hivyo kabisa.
Una usafiri binafsi lakini chagua kutumia usafiri wa umma au kutembea kwa miguu.
Una kitanda kizuri lakini chagua kulala chini au kutokulala kabisa.
Unaweza kupata chakula kizuri lakini chagua kula chakula cha hadhi ya chini au kutokula kabisa.
Chochote ambacho umeshakizoea, chagua kuishi bila hicho na utaona maisha yanaenda tu, huku hofu ikiwa haikusumbui.

3. Maandalizi ni kabla ya tukio.

Seneca anaeleza wakati mzuri wa kufanya maandalizi ya kitu ni kabla ya tukio au kukihitaji kitu hicho.
Anatoa mfano kwamba wanajeshi huwa wanafanya mazoezi ya vita wakati wa amani.
Chochote ambacho tunataka kuwa imara, tunapaswa kukifanyia mazoezi kabla hatujawa na uhitaji nacho.

Na hapa ni msisitizo wa kufanya zoezi la kuishi kimasikini wakati una utajiri.
Unaweza kusema ya nini ujitese, kama umasikini utakuja utauishi kadiri unavyokuja.
Na hapo itakuwa ni sawa na mwanajeshi anayesema hana haja ya kufanya mazoezi wakati wa amani, kwani vita ikija ataikabili wakati huo.
Tunajua mwanajeshi wa aina hiyo ataishia kuumizwa vibaya vitani, kama siyo kufa kabisa.

Chochote tunachotaka kuwa tayari nacho, tunapaswa kujiandaa kabla hatujawa na uhitaji nacho.
Ili pale tunapokuwa na uhiyaji, tuweze kutumia vizuri maandalizi ambayo tumeshayafanya kwa muda mrefu.

Hatua ya kuchukua;
Fanya maandalizi ya vitu mapema kabla hujawa na uhitaji navyo.
Ukisubiri mpaka pale unapohitaji kitu ndiyo ujiandae, unakuwa tayari umeshachelewa.
Fanya mapema mazoezi ya kile unachokiendea ili unapokifikia kisikusumbue.

Nukuu;
“If you would not have a man flinch when the crisis comes, train him before it comes.” – Seneca

“Kama unataka mtu asiwe mlegevu anapokutana na magumu, mpe mafunzo kabla ya magumu hayo hayajamfika.” – Seneca

4. Kuufurahia utajiri, usiusujudu.

Seneca anatupa mfano kwa nini Mungu ana nguvu kuliko vitu vyote? Jibu ni kwa sababu hana anachokisujudu.
Hivyo anatuambia kama na sisi tunataka kuwa na nguvu kama za Mungu basi hatupaswi kusujudu chochote.
Hasa utajiri, maana huo ndiyo umewashika mateka watu wengi.

Seneca anasisitiza kwamba hakatazi mtu kuwa na utajiri, bali awe nao bila ya hofu yoyote. Akijua maisha yake yatakuwa na furaha akiwa na utajiri na hata asipokuwa nao.
Tunapoacha kukisujudu kitu, hakiwezi kututawala.
Hivyo kama tunataka kutawala vyote basi hatupaswi kusujudu chochote.

Hatua za kuchukua;
Usikipe kitu chochote umuhimu mkubwa kwenye maisha yako kuliko maisha yako yenyewe.
Maisha yako yanapaswa kuwa kipaumbele cha kwanza na vingine vyote kuwa vya kutumia tu wakati vipo na kama havipo maisha haweze kuendelea.
Usiwe na utegemezi mkubwa kwa kitu chochote kile kwenye maisha yako.

Nukuu;
“For he alone is in kinship with God who has scorned wealth. Of course I do not forbid you to possess it, but I would have you reach the point at which you possess it dauntlessly; this can be accomplished only by persuading yourself that you can live happily without it as well as with it, and by regarding riches always as likely to elude you.” – Seneca

“Ana undugu na Mungu ule asiyesujudu utajiri. Sikukatazi kuwa na utajiri, bali nataka ufikie hatua ambayo unaumiliki bila hofu, ukiwa nao una furaha na ukiwa hunao pia unakuwa na furaha. Usiruhusu utajiri ukuhadae.” – Seneca

5. Hasira ni sawa na ukichaa.

Seneca anamalizia barua hii kama ambavyo huwa anamalizia barua nyingine, kwa nukuu kutoka kwa mwanafalsafa Epicurus.
Hapa anamnukuu akisema hasira ambayo haidhibitiwi ni sawa na ukichaa.
Anafananisha hasira na moto mkali, ambao huwa unaunguza kila kitu kinachofikiwa na moto huo.
Kadhalika ndivyo hasira zilivyo, huwa zinaharibu kila kitu ambacho zinakigusa.
Seneca anatushauri njia pekee ya kuondokana na ukichaa huo wa hasira siyo kudhibiti hasira baada ya kuzipata, bali kuziepuka hasira kabisa.
Maana moto ukishawaka hata ukiuzima unakuwa umeacha madhara.
Lakini ukiuzuia moto usiwake kabisa, kunakuwa hakuna madhara yoyote.
Njia bora ya kuondokana na madhara ya hasira ni kujizuia usipate hasira kabisa kuliko kuzipata na kujaribu kuzidhibiti, kitu ambacho kitakushinda.

Hatua za kuchukua;
Jizuie usiingie kwenye hasira kwa kupuuza mambo yasiyokuwa na tija.
Hasira huwa zinawaka pale unapoyapa mambo umuhimu kuliko inavyopaswa.
Ukipuuza mambo mengi, huwezi kuwaka hasira.

Nukuu;
“The outcome of a mighty anger is madness, and hence anger should be avoided, not merely that we may escape excess, but that we may have a healthy mind.”

“Matokeo ya hasira kubwa ni ukichaa, hivyo hasira inapaswa kuepukwa, siyo tu kuondokana na madhara yake, bali pia kuwa na afya ya akili.” – Seneca

Rafiki yangu Mstoa, barua nyingi za Seneca zinazungumzia namna ya kwenda na utajiri ili usiwe mzigo kwetu.
Seneca aliandika barua hizi kwa uzoefu wake binafsi, alikuwa tajiri mkubwa wa Roma, lakini pia mwanafalsafa wa Ustoa.
Wengi walimshambulia na kumsema vibaya anakuwaje mwanafalsafa huku pia ana utajiri mkubwa.
Hivyo mara zote alionyesha jinsi ambavyo utajiri aliokuwa nao haukuwa kikwazo chochote kwake kuishi maisha bora na ya uhuru.
Kwake utajiri ilikuwa zana ya kutumia kuyaishi maisha na siyo kitu cha kusujudu.

Hiyo ndiyo njia sisi tuliyopo.
Kwa kuiishi falsafa ya Ustoa na mchakato wa Bilionea Mafunzoni tunajenga utajiri mkubwa sana.
Kama tusipokuwa na njia bora ya kuukabili utajiri huo mkubwa, utayaharibu kabisa maisha yetu.
Tunayo bahati ya kujifunza misingi hii kwenye maisha yetu, tuifanye kuwa sehemu ya maisha yetu kwa kuiishi kila siku.

Tunajenga utajiri mkubwa kwa sababu ipo ndani ya uwezo wetu, lakini hatuusujudu utajiri.
Tunautumia utajiri kuifanya dunia kuwa sehemu bora kabisa ya kuishi.
Na maisha yetu yana furaha na utulivu tukiwa na utajiri na hata tukiwa hatuna utajiri.
Sisi ni Mabilionea Wastoa, hakuna chochote chenye nguvu ya kututikisa.

Kutoka kwa Mstoa mwenzako,
Kocha Dr Makirita Amani.