3170; Umelipa ada.

Rafiki yangu mpendwa,
Hakuna kitu ambacho kinauma kwenye maisha kama kufanya makosa.
Na hilo huwa linaumiza zaidi pale makosa yanayofanyika yanapokuwa ya kifedha.
Yaani pale unapokosea na kuingia gharama kwenye makosa hayo huwa linaumiza sana.

Mwenzetu mmoja hapa amekuwa na safari ya kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kukuza zaidi biashara yake.
Siku ya safari akachelewa kidogo kufika uwanja wa ndege na kukuta wameshafunga kupokea abiria.
Alihangaika kwa njia mbalimbali ili aweze kuruhusiwa kuendelea na safari, lakini hilo halikuwezekana.
Hivyo ikambidi abadili tarehe za safari.
Kwa kufanya hivyo, kukawa na gharama za ziada za kulipia.
Gharama hizo zilimuumiza sana na kuona ni kitu ambacho amejisababishia mwenyewe.

Unapofanya  makosa yenye gharama kama hivyo ni rahisi sana kuumia moyo.
Lakini kosa likishatokea limetokea, hata ujilaumu kiasi gani, hakuna unachoweza kubadili kwenye makosa ambayo umeshayafanya.

Waswahili huwa wanasema kufanya kosa siyo kosa, bali kurudia kosa ndiyo kosa.
Kitu kikubwa unachopaswa kuondoka nacho kwenye kila kosa unalofanya ni funzo unalokuwa umejifunza kupitia kosa hilo.
Na gharama unayokuwa umeingia kupitia kosa hilo unapaswa kuichukulia kama ada ya mafunzo ambayo umeilipa.
Hivyo wajibu wako ni kuhakikisha wakati mwingine hurudii tena makosa uliyoyafanya na kuingia gharama ambazo umeingia.

Pale gharama ya makosa inapokuwa kubwa na ya kuumiza, ndivyo funzo linavyopaswa kuwa kubwa na la kusisitiza.
Hupaswi kuangalia gharama ya makosa kama hasara.
Badala yake unapaswa kuangalia gharama ya makosa kama ada ya mafunzo.
Kama utarudia tena kosa hilo hilo na kuingia gharama hizo hizo, hapo ndipo unapokuwa umeharibu mwenyewe.

Pale unapokosea na kuingia gharama, kokotoa gharama ulizoingia kisha jiambie wazi kwamba tayari umeshalipa ada kwenye funzo ulilopata.
Kila wakati unapokuwa kwenye hali ya kurudia kosa lililokugharimu unajiambia nililipa ada kubwa kwenye hili funzo, wacha nizingatie nisiwe nimepoteza ada hiyo.
Kwa kujikumbusha hivyo, kila kosa unalofanya litakuwa limepunguza uwezekano wa kurudia kosa hilo hilo.
Hivyo kadiri unavyokwenda ndivyo unavyopunguza makosa zaidi.

Huwa kuna ngazi tatu za kujifunza.
Ngazi ya kwanza ni ya mtu mpumbavu.
Huyu huwa hajifunzi kwa namna yoyote ile.
Ataona wengine wanakosea na atawacheka.
Halafu ataenda kufanya makosa yale yale ya wengine na yatamgharimu.
Na bado hatajifunza, ataendelea kuyarudia makosa yake mwenyewe.
Hivyo mpumbavu huwa anaingia gharama kila wakati.
Tena gharama ambazo zinaendelea kukua kadiri anavyokwenda.

Ngazi ya pili ni ya mtu mjinga.
Huyu huwa anajifunza kupitia makosa yake mwenyewe.
Ataona wengine wanakosea na atajifunza, ila hatazingatia sana.
Ataenda kufanya makosa yale yale ambayo wengine wameyafanya na yanawagharimu.
Lakini baada ya kuingia gharama kwa makosa yao wenyewe, huwa wanajifunza na kutokurudia tena makosa waliyofanya.
Hivyo mjinga huwa anaingia gharama mara moja na haijirudii tena.
Na gharama zake huwa zinaenda zikipungua kadiri anavyokwenda.

Ngazi ya tatu ni mtu mwenye hekima.
Huyu huwa anajifunza kupitia makosa ya watu wengine.
Ataona wengine wanakosea, atajifunza na hatarudia makosa ambayo wengine wameyafanya.
Hivyo haingii gharama zozote kwa sababu hafanyi makosa ambayo wengine wameshayafanya.

Kwa haraka haraka kila mtu atapenda kuwa kwenye kundi la tatu.
Lakini siyo rahisi kujua kama una hekima au la.
Hivyo njia rahisi ni kuanzia kwenye ujinga, kwa kujifunza kupitia makosa yako mwenyewe na kuhakikisha huyarudii kamwe.
Kwani hata mtu mwenye hekima kuliko wote kuwahi kutokea duniani, mwanafalsafa Socrates alipoulizwa siri ya yeye kuwa na hekima alijibu anachojua ni kwamba hajui chochote.
Hivyo hekima inaanzia kwenye ujinga na kupata msukumo wa kujifunza kwa kasi.

Kwa maneno mengine, kitu kikubwa sana cha kuepuka kwenye maisha ni usiwe mpumbavu.
Kwa sababu upumbavu una gharama kubwa mno na zinazoendelea kukua kadiri muda unavyokwenda.
Ukiwa mjinga kuna nafuu.
Lakini ukiwa mpumbavu umekwisha.

Ujinga ndiyo njia ya kuelekea kwenye ubobezi.
Kwani huwa wanasema aliyebobea ni yule ambaye amefanya makosa yote yanayoweza kufanyika kwenye kitu hicho anakuwa hana tena cha kukosea.
Sasa hebu fikiria kama mtu ataanza kwa makosa yake mwenyewe, kisha akaongeza kasi kwa kujifunza kupitia makosa ya wengine?

Hicho ndiyo tunachojenga kwenye hii safari na jumuia ya Bilionea Mafunzoni.
Tunafanya makosa na kujifunza ili kutokuyarudia.
Lakini zaidi tunajifunza kupitia makosa ya wengine.
Hivyo kama kuna kosa ambalo mwenzetu ameshalifanya na likamgharimu, hatulirudii.
Kwa maana hiyo tunakuwa tumetumia ada ya wengine kujifunza, kitu ambacho kinatupa hekima.

Lakini tukiwa na upumbavu na kiburi,
Cha kuona kwamba kwetu itakuwa tofauti, kwa sababu labda tunajiona ni wajanja zaidi.
Kisha tukarudia makosa yale yale ambayo wengine wameshayafanya na yakawagharimu,
Tunakuwa tumepoteza fursa ya kuwa na hekima kupitia ushirikiano wetu.
Moja ya vitu vya kunufaika navyo kwa kuwa kwenye hii jumuia ni kupata hekima ya kundi, kwa kutokurudia makosa ambayo wengine wameshayafanya.

Kitendo tu cha kuwa kwenye kikundi cha watu ambao mnaelekea kwenye safari moja na mnashirikiana kwa karibu kwa kuwa na uwazi, kinapaswa kurahisisha zaidi safari yako kuliko ukiwa kwenye safari hiyo hiyo peke yako.
Jifunze sana kupitia makosa ya wengine na epuka sana upumbavu na kiburi.
Kamwe usijiambie kwako itakuwa tofauti.
Huwa hakuna tofauti kubwa, kilichomuumiza mwingine, ukikirudia na wewe kitakuumiza pia.
Ni kama kushika moto.
Kama kuna kitu chenye moto ila hamkijui, mwenzako akikishika na akaungua, unatakiwa ujifunze na usishike.
Utakuwa mpumbavu kama utajiambia hebu na mimi nishike nione kama kweli inaunguza.
Mnaishia kuwa mmeungua watu wawili.
Na inakuwa haina maana kuwa wawili.

Nimeeleza vitu vingi hapa, ambavyo vimekuja baada ya kuanza kuandikia kosa alilofanya mwenzetu, ili tusilirudie.
Mengi haya yanaweza kukuchanganya kabisa au yanaweza kukupa funzo la juu kuliko kosa alilofanya mwenzetu.
Utachagua upande wako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe