3171; Usilipie unachoweza kupata bure.

Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye ukurasa uliopita wa 3170, tumejifunza kuhusu kulipa ada kupitia makosa mbalimbali tunayofanya kwenye maisha yetu.
Pia tukaona hekima ni kujifunza kupitia makosa ya wengine ili usiyarudie.

Kwenye ukurasa huu tunakwenda kuangalia zaidi kuhusu kujenga hekima kupitia makosa ya wengine.
Ndiyo maana ukurasa unaitwa usilipie unachoweza kupata bure.
Maana yake ni badala ya kufanya makosa wewe mwenyewe na yakakugharimu, unapaswa kujifunza kwa wengine ili usiyarudie makosa hayo.

Warren Buffett na Charlie Munger ni wawekezaji mabilionea ambao wana mafanikio makubwa sana.
Kwa zaidi ya miaka 50 wamekuwa wanapata matokeo mazuri kwenye uwekezaji.
Japo kwa miaka yote kumekuwa na wawekezaji ambao wanapata marejesho makubwa kuliko wao, kupitia kuchagua uwekezaji unaolipa zaidi.
Lakini hao wawekezaji, mara kwa mara wamekuwa wakipoteza kwa ukubwa.

Kwenye vipindi mbalimbali, Buffett na Munger wamekuwa wanakataa kuwekeza maeneo ambayo yalikuwa na marejesho makubwa lakini yenye hatari kubwa pia.
Miaka ya 1990 mwishoni kulikuwa na ukuaji wa kasi wa makampuni ya teknolojia. Watu wengi waliwekeza huko na kupata marejesho makubwa kwa kipindi kifupi.
Lakini Buffett na Munger walikataa kuwekeza kwenye makampuni hayo. Watu waliwasema vibaya kwamba wanapitwa na fursa nzuri kwa sababu ya kuwa wagumu kubadilika.
Lakini haikuchukua muda makampuni hayo ya teknolojia yalipata hasara kubwa na wote waliowekeza kupoteza mitaji yao.
Buffett na Munger walibaki bila ya hasara yoyote.

Buffett na Munger wanapoulizwa kuhusu falsafa yao ya uwekezaji wamekuwa wanajibu vitu viwili vikubwa;
Moja ni wanawekeza kwenye yale maeneo ambayo wana uelewa nayo na pale unapotokea uwekezaji ambao una faida kubwa ila hawana uelewa nao huwa hawakimbilii kuwekeza, badala yake wanasubiri huku wakiangalia.

Na mbili ni badala ya kutaka kuonyesha wana akili sana, wao wamekuwa wanakazana kuepuka kuwa wapumbavu.
Na ndiyo maana wamekuwa hawapati marejesho makubwa kwa mara moja kama wawekezaji wengine, ila mwisho wa siku wamekuwa wanapata matokeo mazuri.

Kitu kikubwa tunachojifunza hapa ni kutokukubali kufanya makosa wewe mwenyewe, bali kujifunza kupitia makosa ya watu wengine.

Watu wengi waliofanikiwa huwa wanaonekana kama ni mgando, wanaozingatia misimamo yao ambayo kwa haraka inaweza kuonekana kuwapa hasara.
Lakini kwa muda mrefu, waliofanikiwa wanazidi kupata mafanikio makubwa, huku wale walioshindwa, ambao kila mara wanahangaika na mambo mapya wakizidi kushindwa.
Tofauti hapo ni makosa, waliofanikiwa wanajifunza kupitia makosa ya wengine na hivyo kutokuyarudia. Wakati walioshindwa wakirudia makosa yote peke yao.

Kwenye kujifunza kupitia makosa ya wengine kuna kitu kinaitwa hekima ya kundi. Kwamba ndani ya kundi, kila mtu kuna makosa ambayo anakuwa anayafanya.
Kama kila aliyepo kwenye kundi husika atajifunza kupitia makosa ya wengine na kutokuyarudia, ndani ya muda mfupi makosa kwenye kundi hilo yanakuwa madogo na watu wote kwa ujumla kupata matokeo bora.

Ndani ya kundi letu la Bilionea Mafunzoni tuna hazina kubwa ya makosa mengi ambayo watu wameshayafanya.
Kama tutajifunza makosa hayo kwa kina na kuepuka kuyarudia, tutaishia kupata matokeo makubwa sana.
Muhimu ni tusiwe na tamaa za muda mfupi na wakati mwingine tuwe tayari hata kupoteza faida kubwa za haraka ili kubaki na faida ndogo za muda mrefu.

Kwa maana hiyo basi tunakwenda kushirikishana makosa ambayo tayari tumeshayafanya na hatuwezi kuyarudia tena wala kuwashauri wengine kuyafanya.

Kwenye sehemu ya maoni hapo chini, orodhesha makosa yote ambayo umewahi kuyafanya wewe binafsi kwenye mchakato wa Bilionea Mafunzoni ambayo kamwe hutakuja kuyarudia na unashauri wengine wasiyarudie.

Pia shirikisha makosa uliyojifunza kupitia watu wengine ambao wameyafanya na yakawagharimu sana. Hivyo wewe umejizuia usiyarudie makosa hayo hayo.

Kila mmoja wetu ashirikishe aina hizo mbili za makosa, uliyofanya binafsi na uliyojifunza kwa wengine kwenye huu mchakato ili tuweze kutengeneza hekima ya kundi.
Kupitia uzoefu wa kila mmoja tutakuwa na orodha ya mambo ambayo hatupaswi kuyafanya.
Tutajenga msimamo mkali kwenye kuepuka mambo hayo ili tusirudie makosa ambayo yameshawagharimu wengine.

Haina maana kulipia kitu ambacho unaweza kukipata bure.
Japo wengi huwa hawathamini vitu vya bure, lakini kwenye makosa, kuna manufaa makubwa sana ya kujifunza kutoka kwa wengine.

Karibu ushirikishe kwenye maoni hapo chini makosa uliyowahi kufanya mwenyewe na kamwe hutakuja kuyarudia.
Pia shirikisha makosa uliyojifunza kwa wengine ambayo kamwe hutayafanya tena wewe mwenyewe.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe