Barua ya XX; Kuhusu kuishi yale unayohubiri.
Rafiki yangu Mstoa,
Kusema huwa ni rahisi sana, kila mtu ni msemaji mzuri. Lakini inapokuja kwenye kutenda, wengi siyo wazuri.
Kushauri wengine pia ni rahisi sana, na wengi ni washauri wazuri. Lakini mara nyingi unakuta anayetoa ushauri ndiye anauhitaji zaidi huo ushauri anaotoa, ila bado haufanyii kazi.
Tunaweza kusema kwa uhakika kabisa kwamba matatizo mengi ambayo watu tunayapitia kwenye maisha, ni kwa sababu hatuishi yale tunayoyahubiri.
Maneno yetu na matendo yetu yanatofautiana sana.
Hatupo kitu kimoja nje na ndani yetu.
Na hapo ndipo changamoto nyingi zinapojitokeza.
Hilo halijaanza leo, kwani hata Seneca aliliandikia kwenye barua yake ya 20 kwa rafiki yake Lucilius. Alieleza jinsi wengi wanashindwa kuishi yale wanayohubiri na namna bora ya kujenga maisha yako kuwa imara na tulivu kwa kuishi yale unayohubiri.
Karibu tujifunze kutoka kwenye barua hii na kuendelea kujiimarisha kama Wastoa.
1. Thibitisha maneno yako kwa vitendo.
Seneca anamsifu rafiki yake Lucilius kwa kusema anaendelea vizuri kiafya na anajiona akiweza kujidhibiti yeye mwenyewe.
Seneca anamwambia anafurahia hilo na kuona anastahili sifa kwa sababu amefanya kazi kubwa ya kumtoa kwenye mafuriko ambayo asingeweza kutoka yeye mwenyewe.
Lakini Seneca anamsisitiza kwamba kusema tu haitoshi, lazima athibitishe kwa vitendo pia.
Anamtaka apokee hekima kwenye roho yake na kupima maendeleo yake kwa uimara wa roho yake na kupungua kwa tamaa zake.
Hapa Seneca ametupa vipimo viwili muhimu vya kutathmini maendeleo yetu kama Wastoa; uimara wetu kiroho kwa kutokuyumbishwa na yale tunayopitia na udhibiti tulionao kwenye tamaa zetu.
Hiyo ina maana kama bado tunayumbishwa na mambo tunayokuwa tunapitia na kuongozwa kwa tamaa, bado hatujakomaa kama Wastoa.
Hatua ya kuchukua;
Kila siku jitathmini ukomavu wako wa Kistoa kwa namna ulivyoweza kuwa imara licha ya mambo unayopitia ambayo yangeweza kukuteteresha na pia umewezaje kudhibiti tamaa ambazo unakuwa nazo.
Kila siku kazana kuwa bora kwenye maeneo hayo mawili na utaweza kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako.
Nukuu;
“I ask and beg of you, on your part, that you let wisdom sink into your soul, and test your progress, not by mere speech or writings, but by stoutness of heart and decrease of desire. Prove your words by your deeds.” – Seneca
“Nakuomba uruhusu hekima izame ndani ya roho yako na upime maendeleo yako siyo kwa hotuba au maandishi, bali kwa uimara wa roho na udhibiti wa tamaa. Thibitisha maneno yako kwa vitendo vyako.” – Seneca
2. Ishi kwa viwango vyako vya kifalsafa.
Seneca anasema wapo watu ambao huwa wanaongea ili kupata sifa kutoka kwa wengine kwamba wanaongea vizuri. Pia wapo wanaoongea ili tu kuwashawishi wengine.
Falsafa inatufundisha kufanya na siyo kusema, inamtaka mtu kuishi kwa viwango vyake mwenyewe.
Maisha tulivu ni yale yenye maelewano baina ya maneno na matendo ya mtu.
Seneca anasisitiza sana matendo kuwa sawa na matendo, kila kinachoonekana nje kiwe hivyo ndani.
Sababu kubwa ya watu kukosa utulivu kwenye maisha yao ni pale matendo na maneno vinapotofautiana.
Ukishindwa hili, maana yake umekosa hekima na ukikosa hekima huwezi kuiishi falsafa.
Hekima ni maarifa yanayofanyiwa kazi. Hivyo wapo wengi wanaojua, ila hawana hekima kwa sababu hawaishi kile wanachokijua.
Hatua ya kuchukua;
Hakikisha matendo yako yanaendana na maneno yako. Ni bora usiwe mtu wa kuongea sana, ila ukawa mtu wa vitendo. Itakupunguzia msongo usio na lazima, pale unapojikuta unaongea sana na kushindwa kutekeleza.
Ongea kidogo, fanya zaidi.
Nukuu;
“This, I say, is the highest duty and the highest proof of wisdom, – that deed and word should be in accord, that a man should be equal to himself under all conditions, and always the same.” – Seneca
“Hili ndiyo jukumu kubwa na uthibitisho wa juu wa hekima – matendo na maneno kuwa sawa, mtu anapaswa kuwa mmoja katika hali zote na mara zote kuwa sawa.” – Seneca
3. Hata kama hutafikia viwango, kazana kuviishi.
Seneca anajibu swali la Lucilius aliyeuliza nani anaweza kufikia viwango vya juu kiasi hicho?
Anamwambia wapo wachache sana ambao wanaweza kuvifikia viwango hivyo, lakini wapo kwa uhakika.
Seneca anakiri ni zoezi gumu kuhakikisha maneno na matendo vinaendana.
Anakubali pia siyo mara zote mwanafalsafa anaweza kufikia hilo.
Lakini mara zote mtu anaweza kuwa kwenye safari ya kutekeleza hilo.
Hivyo basi, hata kama mara zote hutaweza kutekeleza maneno na matendo kuwa sawa, usiache kukazana kufanyia kazi.
Endelea na nia ya kuwa mtu mmoja, kuwa sawa mara zote na utapata matokeo mazuri kuliko ukiwa tofauti.
Seneca anataka tujichunguze wenyewe kwenye mambo yetu yote ili kuhakikisha hakuna kutofautiana kati ya maneno na vitendo.
Ujiangalie kama yale unayoonyesha kwa watu wa nje ndiyo pia unayoyaishi kwa ndani.
Bila ya msimamo kati ya maneno na matendo na nje na ndani, huwezi kupata utulivu wa ndani.
Hatua ya kuchukua;
Usiache kuishi viwango vya juu vya maneno kuwa sawa na matendo kwa sababu ni zoezi gumu na linakushinda.
Badala yake endelea kukazana kila mara kuhakikisha maneno na matendo yako vinaendana.
Nukuu;
“Observe yourself, then, and see whether your dress and your house are inconsistent, whether you treat yourself lavishly and your family meanly, whether you eat frugal dinners and yet build luxurious houses.” – Seneca
“Jichunguze wewe mwenyewe uone kama mavazi yako na nyumba yako vinatofautiana, kama unaishi kwa anasa huku familia yako ikiteseka, kama unakula kwa ubahili huku ukijenga nyumba za kifahari.” – Seneca
4. Tengeneza mchakato wa maisha yako ya kila siku.
Seneca anaendelea kushauri kwa sababu ni vigumu kila mara kuhakikisha maneno na matendo vinaendana, njia bora ya kurahisisha hilo ni kutengeneza mchakato wako wa maisha ya kila siku, kisha kuufuata mchakato huo kama ulivyouweka.
Mchakato wako wa siku unakuwa ndiyo nguzo yako, ambayo utajipima nayo pale unapoitathmini kila siku yako.
Lengo lako ni kuhakikisha unatekeleza mchakato wako wa kila siku kama ulivyopanga.
Na hapo matendo yako na maneno yako vitakuwa sawa.
Seneca anasema ukishakuwa na mchakato wako, unapaswa kuufuata huo kwa msimamo wa hali ya juu.
Anaeleza wengi huwa wanapanga nini watafanya, lakini inapofika wakati wa kufanya wanaenda tofauti.
Wewe usiwe hivyo, panga na fanya kama ulivyopanga.
Ukishaamua na kupanga, fanya kama ulivyopanga bila kuacha.
Hiyo ndiyo njia pekee ya kupata matokeo bora kwenye maisha yako.
Seneca anasisitiza kwamba kitu chochote kile sahihi ambacho kinafanyika kwa muda mrefu, lazima kitaleta matokeo makubwa na mazuri.
Wengi wamekuwa hawapati matokeo mazuri kwa sababu hawafanyi kitu sahihi kwa muda mrefu.
Hatua ya kuchukua;
Tengeneza mchakato wa maisha yako ya kila siku, wa mambo yote unayopaswa kuyafanya kisha hakikisha unajisukuma kuyafanya kila siku. Jitathmini kwa kutumia mchakato huo.
Nukuu;
“You should lay hold, once for all, upon a single norm to live by, and should regulate your whole life according to this norm.” – Seneca
“Unapaswa kutengeneza mchakato wa maisha yako ya kila siku na kuishi kwa kuzingatia mchakato huo. Utayadhibiti maisha yako kwa kutumia mchakato huo.” – Seneca
5. Umasikini utakufanya uwajue marafiki wa kweli.
Kitu kikubwa ambacho Seneca alikuwa anamwelekeza rafiki yake Lucilius ni kwamba hata kama ana mali nyingi, ayaishi maisha yake kama vile hana mali hizo.
Lucilius akamjibu kama atafanya hivyo, atawapoteza marafiki zake.
Na hapo Seneca akamwambia ni sahihi, anapaswa kufanya hivyo ili aweze kuwajua marafiki wake wa kweli.
Anasisitiza kwamba ukiwa umezungukwa na kundi kubwa la watu, unaweza kudhani wote wapo kwa ajili yako.
Ni mpaka pale watu wanapokosa walichokuwa wanapata kwako ndiyo utazijua rangi zao za kweli.
Wengi ambao walikuwa kimaslahi wataondoka.
Watakaobaki ni wale marafiki wa kweli kabisa, ambao wapo kwa ajili yako na siyo kwa ajili ya ulichonacho au wanachoweza kupata kwako.
Seneca anaendelea kueleza kwamba utajifunza mambo mengi sana kupitia umasikini ambayo huwezi kujifunza kwa njia nyingine.
Kuwajua marafiki wa kweli ni kitu cha kwanza.
Kitu cha pili utakachojifunza kupitia umasikini ni hakuna atakayekudanganya, watu watakuambia ukweli. Hapa anaeleza watu huwa wanawadanganya matajiri ili wapate wanachotaka, kwa kuwa hakuna wanachoweza kupata kwa masikini, hawajisumbui kuwadanganya.
Kitu cha tatu ni umasikini unakufikisha kwenye ngazi ambayo huwezi kukataliwa. Unapokuwa ngazi ya chini kabisa, unakuwa huna pa kuangukia, yaani upo chini kabisa na hivyo huwezi kuanguka chini ya hapo.
Hatua ya kuchukua;
Hata kama una uwezo wa kupata kila unachotaka, ishi maisha yako bila ya kuonyesha hilo, kwa kuendelea kupata mahitaji ya msingi.
Kama watu watakukimbia kwa maisha hayo uliyoyachagua, jua hawakuwa watu sahihi kwako.
Usiishi kama watu wanavyotaka ili kuwazuia watu wasikuache, bali ishi kwa viwango vyako na walio sahihi watabaki kwako.
Nukuu;
“Poverty will keep for you your true and tried friends; you will be rid of the men who were not seeking you for yourself, but for something which you have.” – Seneca
“Umasikini utakuachia marafiki ambao ni wa kweli; utawaondoa wale ambao wanakuja kwako siyo kwa ajili yako, bali kwa vitu ulivyonavyo.” – Seneca
6. Kama hujafanya, hujamaanisha unachosema.
Seneca anamnukuu Epicurus anayesema maneno yanakuwa na uzito pale unapoyaweka kwenye vitendo.
Kwa sababu ni kupitia kufanya ndiyo hasa unaelewa ugumu wa kitu na uzito wake.
Kama ambavyo tumeshaona, kusema ni rahisi, lakini kutekeleza ni vigumu.
Na inapokuja kwenye kuishi maisha ya kawaida licha ya kuwa na uwezo mkubwa, maneno ni rahisi, lakini matendo ni magumu.
Kwenye hiyo nukuu Epicurus alieleza maneno yako juu ya umasikini yatakuwa na uzito kama umelala kwenye kitanda cha gunia na kujifunika na kipande cha nguo.
Kwa njia hiyo unakuwa shuhuda wa ukweli wa yale ambayo unayahubiri.
Hatua ya kuchukua;
Kujua ugumu na maana ya kitu, kifanye.
Hata kama unakiona ni rahisi kiasi gani kwa maneno, kifanye kwa vitendo na kuna mengi sana utakayojifunza.
Nukuu;
“Believe me, your words will be more imposing if you sleep on a cot and wear rags. For in that case you will not be merely saying them; you will be demonstrating their truth.” – Epicurus
“Niamini mimi, maneno yako yatakuwa na uzito kama umelala kwenye kitanda cha gunia na kufunika mwili wako kwa kitambaa . Kwa sababu katika hali hiyo siyo tu utakuwa unayasema hayo maneno, bali utakuwa unaonyesha ukweli wake.” – Epicurus
7. Huwa tunajisahau haraka sana.
Seneca anatukumbusha kwamba;
A. Mahitaji ya asili ni machache sana na ambayo yapo ndani ya uwezo wa kila mtu.
B. Hakuna aliyezaliwa akiwa tajiri.
C. Tulipozaliwa tu, mahitaji makuu mawili yalitutosha; maziwa na kitambaa cha kufunikwa.
Lakini cha kushangaza sasa, tunavyoenda na maisha tunajisahau sana na kujikuta tukiwa haturidhishwi hata na mambo makubwa ambayo tumeyafikia.
Hata mtu akipewa himaya aitawale, bado hataridhika.
Huko ndiko kujisahau kunakofanya maisha ya wengi yakose utulivu.
Seneca anatukumbusha tunachopaswa kufanya ili kuondokana na hali hiyo ya kujisahau.
Ambapo ni kutenga siku chache ambazo tutaishi kimasikini kabisa. Kwa kuishi kama hatuna kila tulichonacho.
Kufanya hivyo inatuondoa kwenye ulegevu wa mazoea ya kuwa na vitu.
Lakini pia inatufanya tuvithamini vitu tulivyonavyo na kuridhika navyo.
Na zaidi, tunakuwa tayari kuukabili umasikini bila hofu, kwa sababu kunakuwa siyo kitu kigeni kwetu.
Hatua ya kuchukua;
Tenga siku ambazo utaishi kimasikini kabisa kwa kutokutumia vitu ulivyonavyo. Kula chakula cha hadhi ya chini kabisa, lala chini badala ya kitandani na tembea kwa miguu kwenye umbali mrefu badala ya kutumia usafiri.
Utathamini vitu ulivyonavyo lakini pia utakuwa imara kiroho pale lolote linapotokea.
Nukuu;
“No man is born rich. Every man, when he first sees light, is commanded to be content with milk and rags. Such is our beginning, and yet kingdoms are all too small for us!” – Seneca
“Hakuna mtu aliyezaliwa akiwa tajiri. Kila mtu alipoona mwanga kwa mara ya kwanza, litosheka kwa maziwa na kitambaa. Huo ndiyo mwanzo wetu, lakini bado hata falme ni ndogo sana kwetu!” – Seneca
Mstoa mwenzangu, tumejifunza mengi kwenye barua hii kuhusu kuishi kwa vitendo yale tunayoyahubiri.
Kitu kikubwa kwetu kuondoka nacho hapa ni kujiwekea viwango vya juu kabisa vya matendo yetu kuendana na maneno yetu na kupambania hilo muda wote bila kuishia njiani.
Haitakuwa rahisi, lakini inawezekana, pale tunapoamua kweli na kufanya.
Tuwe na maisha ya aina moja, yaliyo sawa mara zote.
Kutoka kwa Mstoa mwenzako,
Kocha Dr Makirita Amani.
Asante sana Kocha Dr. Makirita Amani.
Ni muhimu sana kutenga siku za kuishi umasikini.
Tuhubiri kwa vitendo na siyo kwa maneno.
LikeLike
Hakika
LikeLike
Asante sana kocha Nimetenga siku za kuishi masikini
LikeLike
Vizuri
LikeLike
Kutoka katika barua hii nimeandika mambo kumi ya kufanyia rejea za mara kwa mara. Moja ya jambo muhimu nitakalo liishi kila siku ni kuamua na kupanga na kufanya kama nilivyopanga bila kuacha.
Asante sana Kocha
LikeLike
Kila la kheri.
LikeLike
Tunapaswa kuyaishi maneno yetu ikiwa na maana ukisema na utekeleze kwa viwango ulivyosema
Tuishi kulinganana na muonekano wa ndano na nje ikiwa na maana tusilaze watito njaa na huku sisi tukiponda bata
Hata kama hutafika viwango vya juu usiache kuvifuata fuata maana kuna siku utavifikia
Umaskini utakifanya uwajue marafiki wengi maana wako aatakaokukimbia ajili umeishiwa na wako watakaoendelea kuwa na wewe
LikeLike
Hakika.
LikeLike
Asante kocha,Ni kweli kabisa maisha ya kukaa masikini nimeweza kuwatambua watu muhimu kwangu kama marafiki sio kuishi kwa kujionyesha maisha ya kitajiri kwamba una fedha nje kumbe ndani huna kitu.hivyo inabidi kuishi kwa uharisia sahihi.
LikeLike
Ndiyo
LikeLike
Nitaendelea kujitahidi kuhakikisha maneno yangu yanaendana na matendo yangu.
LikeLike
Vizuri sana.
LikeLike
Nitahakikisha ninaset jinsi yakutekereza mipango yangu.
Kwa viwango vya juu. Hata pale itakapokuwa ikitokea nimeshindwa kufikia viwango hivyo , nitaendelea kujisukuma kufanya Kwa msimamo ili kuvifikia viwango hivyo nilivyo panga.
Asante kocha kwa barua ya xx
LikeLike
Vizuri
LikeLike
Hakikisha matendo yako yanaendana na maneno yako. Ni bora usiwe mtu wa kuongea sana, ila ukawa mtu wa vitendo. Itakupunguzia msongo usio na lazima, pale unapojikuta unaongea sana na kushindwa kutekeleza.
Ongea kidogo, fanya zaidi.
LikeLike
Ndiyo
LikeLike
Ustoa unanifanya ni-balance sana maisha, muongozo wa kuishi, marafiki, mali, kujisahau.
Hekima iliyo katika barua hii pekee nikiiweka katika matendo kwa ukamilifu wake nitaiushi kwa utulivu sana maisha yote.
LikeLike
Kila la kheri.
LikeLike