3182; Suuza kisha rudia.

Rafiki yangu mpendwa,
Japokuwa safari ya kupata mafanikio makubwa kwenye maisha ni ngumu, watu wamekuwa wanazidisha ugumu huo kwa kuamua kuacha kufanya yale ya msingi kwenye hiyo safari.

Kwenye kila eneo la maisha, huwa kuna mambo mengi ya kufanya.
Lakini yapo ya msingi kabisa ambayo ni lazima yafanywe kwa kurudia rudia bila kujali mtu umefikia hatua gani.

Mafanikio makubwa kwenye eneo lolote la maisha huwa yanajengwa kwa kurudia rudia kufanya mambo ya msingi bila kuacha.
Iwe mtu ndiyo anaianza safari ya mafanikio au ameshapiga hatua, yale ya msingi hayapaswi kuachwa kabisa.

Hiyo ndiyo dhana nzima ya suuza kisha rudia na inavyopaswa kufanyiwa kazi kwenye safari ya mafanikio.
Kwa kuchagua mambo ya msingi kabisa kisha kuyafanya kwa kurudia rudia bila kuacha, hata iweje.
Inyeshe mvua, liwake jua, wewe unafanya yale ya msingi.

Lakini cha kushangaza sasa, watu huwa wanaanza kufanya hayo ya msingi, lakini hawafiki mbali, wanaishia njiani.
Siyo kwa sababu wanashindwa kuyafanya hayo ya msingi.
Bali kwa sababu wanazoea na kuchoshwa na kurudia rudia mambo yale yale kila wakati.
Wanaona kama vile kufanya hayo ya msingi haitoshi tena, na hivyo kuhangaika kutafuta mapya ya kufanya.
Wanajikuta wanahangaika na mengi mapya ambayo hayana mchango wa moja kwa moja kwenye mafanikio wanayotaka kujenga.
Hilo linakuwa usumbufu kwao na kuwazuia kuendelea kupata matokeo mazuri.

Watu huwa hawapendi kurudia mambo yale yale kila wakati, hata kama yanawapa matokeo mazuri.
Bali huwa wanapenda kuhangaika na mambo ya kusisimua, ambayo hawana hata uhakika nayo kama yanafanya kazi.
Tuchukue mfano kwenye eneo la fedha, kanuni kuu ya kujenga utajiri ni kipato kuwa kikubwa kuliko matumizi na kuweka akiba na kuwekeza kwenye kila kipato.
Unapaswa kufanya hivyo kwa kurudia rudia kila mara bila kuchoka na kuacha.
Kwa kanuni hiyo rahisi ungedhani kila mtu angeifanya kwa msimamo mara zote bila kuacha.
Lakini unapokuja kwenye uhalisia matokeo yatakushangaza.
Watu watafanya kwa muda mfupi, kisha kuacha.
Wakati wanaacha watatoa sababu mbalimbali zinazoonekana ni nzuri, lakini siyo za kweli.
Sasa subiri kwa mtu huyo huyo asikie kuna mchezo fulani wa kupanda fedha zake na zinakua mara mbili ndani ya muda mfupi, ghafla anapata fedha za kufanya hiyo.
Anaweka fedha huko japo haelewi inafanyaje kazi, mwishowe anapoteza.
Kama mtu huyu angeenda kwa mpango wa kusuuza na kurudia kwenye yale ya msingi, asingepoteza fedha.

Kwenye mchakato wetu wa bilionea mafunzoni, mwendo ni KUSUUZA KISHA KURUDIA.
Tunaenda na huu mchakato bila kuacha wala kuchoka.
Tunakaa kwenye mchakato, tunapata matokeo, tunaendelea kukaa kwenye mchakato na kuendelea kupata matokeo.
Hakuna hatua ambayo tutafika na kuuacha huu mchakato, ni mwendo wa kusuuza na kurudia.

Hizi zitakuwa habari mbaya sana kwa wale wanaofikiri mchakato ni wa kipindi fulani tu, kisha tukishafikia ngazi fulani tunaachana na mchakato na ‘kula bata’.
Hicho kitu sahau kabisa, huu mchakato hauna mwisho, ni mwendo wa kusuuza kisha kurudia.
Zaidi tu tutaenda tukiuboresha huu mchakato zaidi.
Hatuhangaiki na mambo tusiyoyajua, bali yale ambayo tayari tuna uhakika nayo, ambao ni huu mchakato.

Kama unadhani, katika kipindi chochote kijacho utaachana na huu mchakato, basi unapaswa kuachana nao sasa.
Maana kuendelea nao ni kujipotezea muda, hakuna kitakachobadilika zaidi ya kusuuza na kurudia.
Kufanikiwa siyo kuacha kufanya yale ya msingi, bali ndiyo unayafanya kwa uhakika zaidi.
Kadiri unavyofanikiwa ndivyo unavyopaswa kusema hapana nyingi zaidi kwenye vitu vipya na vya kusisimua vinavyokuondoa kwenye yale ya msingi.
Tayari unakuwa na kanuni ya uhakika ambayo imeshakupa matokeo, kwa nini uiache na kuhangaika na mambo ambayo huna uhakika nayo?
Mwendo ni kusuuza kisha kurudia, hakuna kuacha, kwa namna yoyote ile.

Tumalizie na hadithi fupi yenye funzo kubwa kuhusu dhana hii.
Kijana mmoja alienda kwenye shule ya kusomea utawa (Monk), alikuwa na shauku kubwa ya kufikia ngazi ya juu kabisa ya utambuzi (Enlightenment).
Hiyo ndiyo ngazi ambayo mtawa akiifikia, anakuwa amekamilisha lengo na maisha yake yanakuwa ya tofauti.
Kijana huyo alimuuliza mwalimu wake, nini anapaswa kufanya kwa uhakika ili aweze kufikia ngazi hiyo ya juu ya utambuzi?
Mwalimu alimjibu ni kuchota maji na kupasua kuni.
Jibu lilimfikirisha kijana, kisha akauliza tena, nini atakuwa anafanya baada ya kufikia huo utambuzi wa juu.
Mwalimu wake akamjibu tena; utaendelea kuchota maji na kupasua kuni.

Hivyo ndivyo safari tuliyopo ya kufikia ubilionea ilivyo.
Kabla ya kupata ubilionea tunakaa kwenye mchakato kwa msimamo bila kuacha.
Na hata baada ya kufikia ubilionea, bado tutaendelea kukaa kwenye mchakato kwa msimamo bila kuacha.
Hii ni safari ya maisha,
Sawa na kifungo cha maisha,
Ambacho hakina hata msamaha wa raisi.

Kama unaufanya huu mchakato kwa kuigiza, ukidhani ni kitu cha muda tu au cha kupita, nakushauri tu uachane nao mapema.
Maana hakuna njia ya hovyo utakayokuwa umechagua ya kuyapoteza maisha yako zaidi ya hiyo.
Kwa kuwa ni kitu cha maisha yetu yote, hakuna namna utaweza kuigiza kwa muda mrefu kiasi hicho.
Wakati ni ukuta, utaishia kugonga tu kwenye huo ukuta.

Mambo yote ya msingi kwenye maisha tunayafanya kwa mfumo wa kusuuza kisha kurudia. Kupumua, kula, kulala, kuoga n.k.
Unaendelea kuyafanya kwa kurudia rudia bila kuacha kwa miaka yako yote.
Kwa nini unadhani kukaa kwenye mchakato wa ubilionea kutakuwa tofauti?

Mwendo ni kusuuza na kurudia,
Mzunguko ule ule,
Kama saa ya mshale,
Au kanda mbovu.
Rudia, rudia, rudia.
Hakuna mwisho.
Ni kusuuza na kurudia.
Huwezi, acha mapema.
Maana hakuna namna mchakato utaachwa, milele.
Kama huwezi kufanya sasa kwa msimamo bila kuacha, hakuna wakati utaliweza hilo.
Amua sasa kuenda na huu mchakato kwa ukamilifu wake, au kuachana nao.
Amua kusuuza na kurudia au kuacha kabisa.
Hakuna namna nyingine.
Hakuna njia ya mkato.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe