3183; Nini naweza kupenda kwake?

Rafiki yangu mpendwa,
Wateja tulionao kwenye kile tunachouza ni watu muhimu sana kwetu.
Hao ndiyo wanaotuwezesha kulipa gharama mbalimbali kwenye maisha yetu.

Ni kupitia wao kununua kwetu ndiyo tunapata fedha za kuyaendesha maisha yetu.
Wateja wanaonunua kwetu ni watu muhimu sana kwetu.
Swali ni je tunawafanyaje ili waweze kujiona ni muhimu kabisa kwetu?

Njia kuu ya kuwafanya watu waoje jinsi walivyo na umuhimu kwetu ni kuwapenda kweli kutoka ndani ya mioyo yetu.
Kwa wateja wetu, tunapaswa kuwapenda kweli na siyo kwa sababu wanatuletea fedha.

Fedha zinapohusika kwenye jambo lolote lile, huwa ni vigumu kujua kama mapenzi yanayokuwepo ni ya kweli au ya fedha.
Kwa wateja wetu na umuhimu walionao kwetu, tunapaswa kuwa na mapenzi ya kweli kwao ambayo hayaangalii tu fedha.

Hiyo ni kwa sababu wateja hao licha ya kuwa na uhuru wa kununua kwa wengi wanaouza kile tunachouza, wamechagua kununua kwetu kwa kila manunuzi yao.
Ni wajibu wetu kuwaonyesha wateja hao kwamba wamefanya maamuzi sahihi kutuchagua sisi.

Hivyo basi, zoezi la kuwa na mapenzi ya dhati na wateja wetu halikwepeki.
Swali linalofuata ni je nini unaweza kupenda kwa wateja wako?
Hili ni swali ambalo huwezi kujibia kwa kundi, bali unaweza kujibu vizuri kwa mtu mmoja mmoja.

Ili kuweza kukamilisha zoezi la kuwapenda wateja wako, jiulize swali hili kwa kila mteja; ni kitu gani ninachoweza kupenda kuhusu yeye?
Hili ni swali ambalo linakupa sababu halisi za kumpenda mtu.
Kwa kulijibu swali hilo vizuri unakuwa na uelewa mkubwa kwa kila mteja wako na kuwa na sababu sahihi za kumpenda.

Kwenye kulijibu swali hilo, lazima utaje kitu halisi kutoka kwa kila mteja.
Usiwe na majibu ya jumla kwako, mfano kusema nampenda fulani kwa sababu ananunua kwangu.
Majibu ya aina hiyo hayatakuwa na msaada kwako.
Badala yake chagua tabia na sifa mahsusi anazokuwa nazo mtu na ambazo zina manufaa makubwa kwako.

Japokuwa hatuwezi kuvuka maslahi yetu binafsi kwamba kitu cha kwanza kinachotusukuma kuwapenda ni manunuzi wanayofanya kwetu, bado kwa kuwa na sababu nyingine za msingi zinazotusukuma kuwapenda wateja zinachangia kwenye kuboresha mahusiano yetu na wateja wetu.

Ni kitu gani unachoweza kupenda kutoka kwa kila mteja anayenunua kwako ni swali muhimu kuwa na majibu nalo kwa kila mteja.
Majibu hayo yanakuwa na nguvu ya kuimarisha mahusiano yako na wateja hao.
Kwa mahusiano imara, wateja wanaendelea kurudi kununua kwako.
Wanaporudi kununua wanapata thamani kubwa na kushawishika kununua zaidi ya walivyopanga.
Lakini zaidi wanakuwa tayari kuwaleta wateja wengine kwenye biashara yako.

Kazi yako kuu kwenye maisha kama muuzaji ni kujenga na kuboresha mahusiano na wateja wa aina hiyo wengi.
Kadiri unavyokuwa na wateja wa aina hiyo wengi, ndivyo unavyoweza kuwa na maisha bora na yenye uhuru mkubwa.
Unakuwa unayafanya maisha yao kuwa bora kwa thamani kubwa unayowapa ambayo hawawezi kuipata pengine.
Na wao wanayafanya maisha yako kuwa bora kwa kukupa fedha za kuyaendesha maisha yako.

Kwa kuwapenda kweli wateja wako kutoka ndani ya moyo wako, hasa kwa kuwa una sababu ya kumpenda kila mmoja, unakuwa umeufungua moyo wako kwa wateja wako na wao kujiachia zaidi kwako.

Pamoja na wateja wengi unaoweza kuwa unawauzia, ni wajibu wako kumfanya kila mmteja kujiona wa kipekee kabisa kwako.
Hilo linawezekana pale unapokuwa na mapenzi ya kweli kwa kila mmteja mmoja mmoja.

Hiyo inaweza kuonekana ni kazi kubwa.
Ya nini ujisumbue kutaka kumpenda kila mteja wakati tayari wananunua kwako?
Na jibu ni rahisi, unachotaka ni kila mteja kuwa wako milele.
Asiwe tu mteja wako kwa kununua kwako.
Bali pia awe shabiki wa ukweli kwenye biashara yako.
Kwa kuipambania kuhakikisha inawafikia wengi kama yeye.

Hivyo basi, kama tukiacha uvivu na kuufungua mioyo yetu kwa wateja wetu, tunakwenda kupata manufaa makubwa sana.
Tuwapende wateja wetu kwa sababu maalumu kwa kila mmoja na tutaweza kujenga mahusiano bora na wateja hao na kudumu nao milele.

Mapenzi yana nguvu,
Mapenzi yanaendesha dubia,
Na mapenzi yanaweza kutupa chochote tunachotaka.
Tuwe na mapenzi ya kweli kwa wateja wetu na tutaweza kupata chochote tunachotaka kwenye maisha yetu.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe