3184; Haina Mjadala.

Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye safari ya kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha, lazima uwe na mchakato ambao unaufuata mara zote bila kuacha.
Unapaswa kuwa na mambo ambayo utayafanya bila ya kuruhusu hofu au sababu zozote zile kukuzuia.
Hii ni dhana inayoitwa Haina Mjadala (Non Negotiable).

Kwenye mambo hayo, hupotezi muda kujiuliza kama utafanya au hufanyi au ufanye muda gani.
Ni utafanya, kwa muda uliopanga kufanya, iwe unajisikia kufanya au la.

Tupo hai kwa sababu kuna mambo huwa tunayafanya bila ya mjadala.
Hujadili iwapo upumue au la, bali unalazimika kupumua, kwa sababu ni muhimu.
Kadhalika hata uwe umetingwa kiasi gani, huwezi kuahirisha kula chakula kwa siku kadhaa.
Hayo ni mambo muhimu, ambayo lazima uyafanye, liwake jua, inyeshe mvua.

Kama umeweza kula na kupumua kila siku, licha ya matatizo na changamoto nyingi ambazo umekuwa unakabiliana nazo, basi pia unaweza kupata mafanikio makubwa, hata kama unaanzia wapi.
Kitu pekee unachohitaji ni kuwa na mchakato wako wa mafanikio ambao unautekeleza kila siku bila ya mjadala.

Unapanga na kisha kufanya kama ulivyopanga.
Bila ya kuwa na hofu wala kukwamishwa na sababu zozote zile.
Ukishakuwa na hofu ya kufanya kitu, hofu hiyo inaendelea kuwa na nguvu kadiri unavyokuwa hukifanyi kitu hicho.
Ukishakuwa na sababu za kutokufanya kitu, kila wakati sababu hizo zitakuwa zinajitokeza.

Kusahau, kupitiwa na kuchoka ni mambo ambayo huwa yanatolewa na wale ambao hawajajitoa kweli kupata kile wanachotaka.
Lakini mtu anapokitaka kitu kweli na akawa hana mbadala mwingine wowote, lazima atakipata au atakufa akikipambania.

Huwa kuna kauli inayosema nionyeshe ratiba yako ya kila siku na nitakuonyesha utaenda kuwa mtu wa aina gani.
Hili halihitaji mtu uwe na nguvu za kutabiri mambo yajayo.
Bali unahitaji tu kuangalia yale mambo ambayo mtu anayapa kipaumbele zaidi na kujiuliza kama ataenda nayo hivyo kwa miaka mingi ni matokeo gani atapata?

Kwa sababu sisi binadamu ni viumbe wa tabia. Chochote tunachofanya mara moja, huwa tuna nafasi kubwa ya kurudia tena kufanya.
Hakuna kitu ambacho tunakifanya mara moja tu kwenye maisha yetu.
Huwa tunafanya kwa kurudia rudia.

Ndiyo maana mtu anayeshindwa kufanya kitu fulani ambacho ulitaka afanye, kwa sehemu kubwa hatafanya, hata kama atakuahidi kufanya.
Utahangaika naye sana, lakini mwisho wa siku hatafanya, kwa sababu ndivyo alivyo.

Kila unapokubali hofu ikuzuie kufanya kitu, unazidi kuipa hofu hiyo nguvu ya kuendelea kukuzuia kufanya. Hivyo ufanyaji unaendelea kuwa mgumu kwako.
Kila unaporuhusu sababu yoyote ikukwamishe kufanya, maana yake umejiambia wewe mwenyewe na wengine wote kwamba kuna vitu vingine muhimu kwako kuliko kufanya hicho ulichopanga kufanya.
Na kama kitu siyo muhimu kabisa kwako, hakuna namna kitafanyika.

Ni mambo gani kwenye mchakato wako wa mafanikio umeshayafanya kuwa haina mjadala?
Mambo gani ambayo kila siku lazima uyafanye hata iweje?
Karibu ushirikishe kwenye maoni hapo chini.
Muhimu ni shirikisha yale ambayo tayari unayafanya kila siku na siyo yale ambayo unatamani ungeweza kuyafanya kila siku.
Kuna tofauti kubwa sana hapo ambapo usipoielewa utajikwamisha sana kupiga hatua.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe