3189; Unaanza na kufanya.

Rafiki yangu mpendwa,
Kinachowakwamisha watu wengi kupata kile wanachotaka kwenye maisha yao ni kushindwa kuelewa jinsi mipango, hamasa na ufanyaji vinavyohusiana.

Hivyo wengi huwa wanatumia muda wao mwingi kupanga nini watafanya. Na hata baada ya kupanga, bado wanatumia muda mwingi kupitia mipango waliyojiwekea.

Halafu wanakuja kusubiri mpaka wapate hamasa ndiyo waanze kufanya. Hilo limekuwa linawafanya watumie muda mwingi nje ya kufanya na hivyo kujikwamisha wao wenyewe kupiga hatua.

Watu wote waliofanikiwa kufanya makubwa kwenye maisha yao, wamekuwa na mkakati wa tofauti ambao ni kuanza na kufanya.
Pale wanapoamua watafanya kitu, wanaanza kukifanya mara moja, bila hata ya kusubiri wawe tayari kwa kila kitu.
Wanaanza kufanya kisha kuendelea kuboresha kadiri wanavyokwenda na matokeo wanayopata.

Wale waliofanikiwa hawasubiri mpaka wapate hamasa ndiyo wafanye, badala yake wanaanza kufanya na hilo linatengeneza hamasa kubwa ndani yao ya kuwasukuma waendelee kufanya.

Halafu pia kuna swala la uchovu.
Wengi hutumia uchovu na kukosa nguvu kama sababu ya kushindwa kufanya makubwa waliyopanga.
Wanasubiri mpaka wapate nguvu ndiyo waanze kufanya.
Wasichojua wengi ni kwamba nguvu hazitengenezwi kwa kupumzika, bali zinatengenezwa kwa matumizi ya nguvu.
Yaani utapata nguvu zaidi pale unapotumia nguvu kuliko ukiwa unasubiri.

Hivyo usikubali kwenda kinyume kwa kusubiri mpaka uwe na nguvu ndiyo uanze kuchukua hatua.
Badala yake unaanza na ufanyaji kwanza.
Kadiri unavyofanya ndivyo unavyouchochea mwili kutengeneza nguvu zaidi za kufanya.
Hatua unazokuwa umeanza kuchukua zinazalisha nguvu ya kuweza kufanya zaidi.
Nguvu unazozalisha zinakupa msukumo wa kuendelea kufanya kwa ukubwa zaidi.

Unaanza kwa kufanya,
Ambapo kunazalisha nguvu za kufanya zaidi.
Ambazo zinaleta matokeo bora.
Ambayo yanampa mtu hamasa ya kuendelea kufanya zaidi.
Mtu anapofanya zaidi ndivyo anavyopata matokeo makubwa zaidi.
Kuwa mtu wa kuanza na kufanya mara zote na utaweza kufanya makubwa sana kwenye maisha yako.

Usisubiri kuwa tayari ndiyo uanze,
Usisubiri uwe na nguvu ndiyo uanze,
Usisubiri uwe na hamasa ndiyo uanze.
Anza kwanza, anzia pale ulipo kwa kile ulichonacho kisha nenda ukiboresha.
Ni bora ukosee ukiwa unafanya kuliko usikosee huku ukiwa hufanyi.

Kufanya kumefunika yote.
Julikana kama mtu wa kufanya na siyo wa visingizio.
Ni kwa njia hiyo ndiyo utaweza kufanya makubwa zaidi kwenye maisha yako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe