3191; Ujuzi, Tabia Na Muda.

Rafiki yangu mpendwa,
Hali ya watu kutafuta njia ya mkato ya kupata mafanikio halijaanza leo na wala halitaisha leo.
Tangu enzi na enzi watu wamekuwa wanatafuta hizo njia za mkato.
Lakini kwa bahati mbaya sana, wamekuwa wanaishia kupoteza nguvu, fedha na muda.
Haijawahi kuwepo njia ya mkato ambayo inampa mtu mafanikio ya kudumu.

Njia ya mafanikio makubwa ni ndefu na yenye ngazi tofauti za mtu kuchukua katika nyakati tofauti za maisha yake.

Wakati mtu anaianza safari yake, ngazi ya kwanza kabisa ni kujenga ujuzi ambao unaweza kumwingizia kipato kikubwa na endelevu.
Hii ndiyo hatua ya kuanzia kwa mtu yeyote yule anayetaka kufanikiwa.
Kwa bahati mbaya sana, wengi wanapoanza huwa wanaangalia zaidi upande wa kipato, wafanye nini ili waingize kipato.
Hapo wanajikuta wakihangaika na kufanya vitu mbalimbali vya kuwaingizia kipato, ila wanakuwa hawajengi ujuzi wowote ambao unawapa fursa ya kuendelea kulipwa kwa uhakika na ukubwa kadiri muda unavyokwenda.

Wewe usiangalie tu nini ukifanya kinakuingizia fedha, bali angalia ni ujuzi gani unaojenga ambao kadiri muda unavyokwenda unazidi kubobea na malipo unayoingiza kuzidi kuongezeka.
Kuuza ni ujuzi ambao una nguvu ya kuwavusha watu wengi kutoka ngazi ya chini kabisa kwenda ngazi ya juu.
Kadiri unavyoendelea kujifunza na kubobea mauzo, ndivyo unavyozidi kuingiza kipato kikubwa.
Kujenga biashara ni ujuzi wa juu ambao ukiweza kuujenga na kubobea utaweza kupata mafanikio makubwa unayoyataka.

Vitu muhimu kwenye kujenga ujuzi ni kupata maarifa endelevu na kuchukua hatua za kuboresha kila unachofanya.
Kwenye kujenga ujuzi epuka sana kufanya vitu rahisi na kwa mazoea ya kuiga wengine.
Hivyo haviwezi kukujengea ujuzi utakaokulipa kwa kiwango kikubwa kiasi cha wewe kuweza kuelekea kwenye mafanikio makubwa unayoyataka.

Ngazi ya pili ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa unayoyataka ni tabia.
Ukishakuwa na ujuzi ambao unakuingizia kipato kikubwa na kwa mwendelezo, kitakachoamua upige hatua ni tabia zako.
Wengi wamekuwa wanaharibikiwa kwenye ngazi hii kutokana na kukosa tabia nzuri.
Mtu anakuwa na ujuzi wa kumwingizia kipato, lakini anakuwa na tabia ambazo zinakuwa kikwazo kikubwa kwake kupiga hatua.
Kwa mfano mtu ambaye anakosa tabia ya kuweka akiba na kuwekeza sehemu ya kipato chake, hata aingize kipato kikubwa kiasi gani, ataendelea kubaki kwenye umasikini.
Kadhalika mtu ambaye amekosa uaminifu na uadilifu, ataharibu fursa nzuri anazopata za kumwezesha kukua zaidi.
Kwa mfano mtu anapoanza na ujuzi mzuri na watu wakapenda kufanya naye kazi, anapokosa uaminifu watu hawarudi tena kufanya naye kazi, kitu kinachokuwa kikwazo kwake.

Kilicho muhimu kwenye tabia ni maadili unayokuwa nayo na nidhamu uliyojijengea kwenye kila eneo la maisha yako.
Kama huna maadili ya msingi unayoyasimamia, kila hatua unayokuwa unapiga unakuwa unajipeleka kwenye hatari kubwa zaidi kwako.
Na pia kukosa nidhamu kwenye maeneo yote ya maisha yako kunakufanya uwe dhaifu na unayeweza kuangushwa na kitu chochote kinachotokea kwenye maisha yako.

Ngazi ya tatu kwenye safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa ni muda.
Hapa ndipo wengi wanaoanza vizuri huwa wanamalizia vibaya.
Wanaweza kuanza kwa kujenga ujuzi ambao unawaingizia kipato na hata wakawa na tabia zinazowadumisha kwenye hatua wanazopiga. Lakini wanapokuwa na mtazamo wa kutaka njia ya mkato ya kukua zaidi, ndipo wanapoharibu.
Ngazi ya tatu ya kujenga mafanikio makubwa ni kujipa muda wa kutosha.
Unajipa muda wa kutosha wa kuendelea kubobea kwenye ujuzi uliochagua na kuyadhibiti vizuri matokeo unayokuwa unayapata kupitia tabia nzuri unazokuwa nazo.

Muda unataka sana mtu kujitoa moja kwa moja na kuwa na ung’ang’anizi mkubwa kwenye anachofanya.
Muda unataka mtu kuwa na maono makubwa na ya muda mrefu kisha kukaa kwenye maono hayo kwa msimamo bila kuacha.
Kwenye muda mtu anakuwa anaendelea kujiboresha kadiri anavyokwenda.

Kama utakaa kwenye safari yoyote ile kwa muda mrefu zaidi, ukiwa umejijengea ujuzi unaokulipa vizuri na kwa uendelevu, huku ukiwa na tabia njema na unazoendelea kuziboresha, lazima utapata chochote kile unachotaka kwenye maisha yako.
Unachohitaji wewe ni kujenga ujuzi, kujenga tabia na kujipa muda wa kutosha wa kuendelea kufanya bila kuishia njiani.

Hiyo ndiyo njia tuliyochagua hapa;
Unaanza na kujenga ujuzi mkubwa kwenye mauzo kama bado kipato chako kiko chini, kikishakua unaenda kwenye ujuzi wa kujenga biashara kubwa.
Unakuwa na tabia ya kukaa kwenye mchakato na kuzingatia misingi inayotuongoza hapa bila ya kuacha.
Halafu unajipa muda mrefu, wa miaka kumi na kuendelea wa kupambana kwa kila namna kwenye huo ujuzi na tabia kuhakikisha unapata unachotaka.
Kama utakaa hapa na kuzingatia hayo, ninachoweza kukuhakikishia ni ushindi mkubwa, bila kujali unaanzia wapi.

Ujuzi utakufikisha kwenye ngazi ya utajiri ya LAKIONEA (Dola laki 1 na kuendelea)
Tabia zitakufikisha kwenye UMILIONEA.
Na muda utakufikisha kwenye UBILIONEA.
Hiyo ni kanuni na ngazi za uhakika, ni wewe tu uziamini na kuzifuata.

Maswali ni je umechagus kukaa kwa maisha yako yote?
Je utajenga ujuzi kwa uendelevu ili kuendelea kukuza kipato chako?
Je utakaa kwenye mchakato bila kuyumba na kufuata misingi inayotuongoza bila kuivunja?
Je umejitoa kweli ili kupata unachotaka? Upo tayari kuvumilia na kung’ang’ania mpaka upate unachotaka?

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe