3192; Maarifa, Maadili na Ujuzi.

Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye ukurasa uliopita wa 3191 tumejifunza kuhusu Ujuzi, Tabia Na Muda.
Kwenye ukurasa huu tunakwenda kupata toleo la watoto la vitu vitatu muhimu kuwajengea ili kuwaandaa kwa maisha ya mafanikio.

Lakini kabla ya kuingia kwenye ukurasa huu, nianze kwa kuambiana ukweli sisi kama wazazi.
Wengi wetu hapa tuna watoto katika ngazi mbalimbali za umri.
Na pia wote tumekuwa na matatizo makubwa mawili inapokuja kwenye malezi ya watoto.

Tatizo la kwanza ni unafiki.
Wote tunakubali ya kwamba mfumo wa elimu kwa namna ulivyo sasa hauna manufaa kwa watoto.
Lakini bado tunahangaika kuwapeleka watoto kwenye shule za gharama kubwa.
Tunaweza kukubali kwamba tunafanya hivyo kwa sababu hatuna namna nyingine, maana hatuwezi kuubadili mfumo huo wa elimu sisi wenyewe.

Lakini tatizo la pili hatuwezi kulikwepa, ambalo ni uvivu kwenye malezi ya hao watoto wetu.
Kwa sababu tumeshawapeleka shule za gharama, tunaona tumemaliza kazi yetu kama wazazi na kinachobaki ni wajibu wa walimu kuwajenga hao watoto.
Matokeo yake wanakaririshwa mambo mengi, wanafaulu vizuri mitihani, lakini wanapokuja kwenye maisha, yanawapiga chenga sana.
Yote hayo ni kwa sababu sisi wazazi hatukufanya kazi yetu vizuri.

Hivi karibuni kumekuwa na video inayozunguka sana mtandaoni ikimwonyesha kamishna wa elimu akiongea kwenye mahafali ya shule.
Katika hotuba yame amesisitiza kama wazazi tuna wajibu mkubwa wa kuwajengea watoto vitu vitatu muhimu; maarifa (akishika kichwa), maadili (akishika kifua) na ujuzi (akishika mikono).
Alisisitiza kwamba kuwapeleka watoto shule nzuri na wakafaulu vizuri masomo yao hatujamaliza wajibu wetu kama wazazi.
Vitu hivyo vitatu alivyotaja ni wajibu wetu wazazi kuvijenga kwa watoto wetu ili kuwaandaa kwa maisha ya mafanikio makubwa.
Tunaweza kusema ni urithi wa uhakika unaoweza kuwaachia watoto wako, ambao utadumu nao milele, kuliko hata mali nyingi unazoweza kuwaachia.

Sote ni mashahidi wa jinsi baadhi ya wazazi waliopambana sana kujenga utajiri mkubwa na kuwaachia watoto wao walivyopoteza utajiri wote ndani ya muda mfupi baada ya kufariki kwa wazazi wao.
Yote hayo ni kwa sababu watoto hao hawakupewa Maarifa, Maadili na Ujuzi ambavyo vingewawezesha kuendeleza utajiri walioachiwa.
Na hata kama watoto hawataachiwa utajiri wa mali, wakijengewa vitu hivyo vitatu kwa uhakika, wataweza kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yao wenyewe.
Tuviangalie vitu hivyo vitatu kwa undani zaidi.

Kitu cha kwanza kuwajengea watoto ni kiu ya kupata MAARIFA kila wakati.
Wakati walimu shuleni wanawakazania kukariri masomo yatakayowapa ufaulu wa alama A na kuzipa sifa shule zao, sisi wazazi tunapaswa kuwakazania watoto kupenda kujifunza kwa kupata maarifa mbalimbali kupitia usomaji.
Tunapowajengea watoto kiu ya kujifunza kwa uendelevu, kwa kuwajengea tabia ya udadisi na kupenda kujua vitu vipya kila mara inawafungulia dunia kubwa sana ambayo kwa wengi imefungwa.
Ni kupitia maarifa ndiyo wanaweza kuwa na ndoto kubwa na hata kuzipambania ili kufanikiwa.
Sote tunajua jinsi kuchelewa kuyapata haya maarifa kumekuwa kikwazo kwetu kupiga hatua za mafanikio mapema kwenye maisha yetu.
Tusitake kurudia makosa hayo hayo kwa watoto wetu, tuwajengee msingi wa maarifa mapema.
Na wajibu wetu hapa ni kuwajengea watoto wetu tabia ya kujisomea vitabu kwa kusoma nao pamoja.
Hili linapaswa kuanza mapema ili iwe tabia ya kudumu kwa watoto hao, kwani ndiyo itawapa manufaa makubwa kwa maisha yao yote.

Kitu cha pili cha kuwajengea watoto ili wawe na maisha ya mafanikio ni MAADILI.
Maadili ni misingi muhimu wanayoisimamia kwenye kuendesha maisha yao kwa namna bora kwao na kwa wengine.
Sote tunaona jinsi ambavyo kumekuwa na mmomonyoko wa maadili kwenye jamii zetu.
Siyo tu kwa tabia mbaya ambazo zimekuwepo baina ya watu, bali hata kuwepo kwa wimbi kubwa la vijana ambao wanataka kupata fedha nyingi bila kufanya kazi na hivyo kuishia kwenye vitu visivyo na tija kama kucheza kamari na michezo ya kubahatisha.
Tunapaswa kuwajengea watoto wetu maadili ya msingi ambayo watapaswa kuyazingatia kwenye maisha yao bila ya kuyavunja kwa namna yoyote ile.
Na hilo linaanza na sisi wenyewe kuyaishi maadili hayo, kwa sababu watoto huwa hawasikilizi tunaongea nini, bali wanaangalia tunafanya nini kisha kuiga hicho tunachofanya.
Tunaweza kuwapigia kelele sana watoto ni jinsi gani wanapaswa kuwa, lakini wataishia kuiga vile tunavyoishi.
Uzuri ni tayari tunayo misingi mizuri ya maadili kwenye KISIMA CHA MAARIFA, wajibu wetu ni sisi kuiishi misingi hiyo na kuwaonyesha watoto wetu kwa vitendo huku tukiwafundisha mara kwa mara na kurudia rudia jinsi wanavyoweza kujijengea misingi hiyo ya maadili na kwa nini ni muhimu wao kufanya hivyo.
Tuyaishi maadili na kuyafundisha mara zote kwa watoto wetu.

Kitu cha tatu cha kuwajengea watoto ni UJUZI.
Kwenye ujuzi ndipo palipo muhimu sana kuwajengea watoto uwezo wa kuja kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha.
Ujuzi ndiyo unamtambulisha mtu kwa wengine na kumpa fursa nzuri za kuingiza kipato kikubwa kupitia yale anayoweza kuyafanya na yenye thamani kubwa kwa wengine.
Kumekuwa na mwenendo mbaya sana kwenye jamii zetu kwa sasa wa watu, hasa vijana kukimbilia kufanya vitu vinavyowaingizia fedha, lakini ambavyo siyo ujuzi ambao una fursa ya kuwapa ukuaji zaidi.
Utitiri wa michezo ya kubahatisha ni kielelezo cha jinsi ambavyo watu wanatafuta njia ya mkato ya mafanikio, wakati haijawahi kuwepo.
Mafanikio makubwa na ya kweli yanajengwa kwenye kazi.
Na kazi inayowalipa watu kwa viwango vikubwa ni ile inayotokana na ujuzi mahususi.
Ni wajibu wetu kama wazazi kuwajengea watoto wetu ujuzi mapema.
Kwanza tunapaswa kuwachochea kujaribu kufanya vitu vingi ili tuone ni vipi wanaweza kuvifanya vizuri zaidi na wanapenda kuvifanya pia.
Tukishajua vile wanavyopenda kufanya na wanavifanya vizuri zaidi, tunapaswa kuwasaidia kujenga ujuzi mkubwa kwenye maeneo hayo, ujuzi ambao utawatofautisha kabisa na watu wengine kwenye jamii.

Ujuzi mkuu kwa kila mzazi aliye kwenye KISIMA CHA MAARIFA kuwajengea watoto wake ni kuuza.
Kwa kila aina yoyote ya ujuzi ambayo watoto wetu wanakuwa nayo, watafanya vizuri zaidi kama wataweza kuwa wauzaji wazuri.
Hivyo tunawajibika kuanza kuwaandaa watoto wetu mapema kuwa wauzaji bora kuwahi kutokea.
Tuwafundishe kwa vitendo misingi yote muhimu ya mauzo ambayo tunaifanyia kazi kwenye maisha yetu.
Watoto wakiweza kuwa wauzaji bora mapema, kwa chochote watakachofanya, watapata matokeo bora zaidi.
Lakini pia sisi tunahangaika na kujenga biashara zetu ziweze kudumu miaka mingi, kama hatutawajengea watoto wetu ujuzi wa kuendesha biashara kwa mafanikio, ndoto zetu zitazimika siku tunapokufa.
Chochote tunachojenga, tuwajengee watoto wetu uwezo wa kukiendeleza pale tunapokuwa hatupo.

Nimekuwa nasema ni jambo la ajabu sana sisi wazazi kuhangaika kujenga biashara zetu, huku tukipambana kuwalipia watoto ada kubwa kwenye elimu ya darasani, halafu wakihitimu tunawasukuma wakatafute kazi za kuajiriwa na watu wengine, ambao watawalipa kiasi kidogo cha fedha na hata kuwanyanyasa.
Kwa nini wakati tunahangaika kuwalipia ada tusihangaike pia kuwajengea ujuzi ambao wakimaliza tu shule wanaendelea kufanya shughuli mbalimbali ambazo tumeshaanzisha?

Ni wajibu wetu sisi wanachama wa KISIMA CHA MAARIFA kuvunja hii laana iliyojengeka kwenye jamii zetu ya kila kizazi kuanzia sifuri kwenye kujenga mali na utajiri.
Tuanze kuwajengea mapema watoto wetu ujuzi wa kujenga na kutunza utajiri, kupitia kuwafanya kuwa wauzaji bora, waendeshaji bora wa biashara na pia wawekezaji wakubwa.
Mwekezaji mwenye mafanikio makubwa duniani, Warren Buffett ambaye kwa sasa ana miaka 94, alianza kufanya uwekezaji kwenye soko la hisa akiwa na miaka 11 na hajawahi kuacha kuwekeza tangu hapo.
Sasa hebu niambie mtu ambaye amefanya uwekezaji bila kuacha kwa miaka 83, atawezaje kushindwa? Tena akiwa mtu wa kupenda maarifa (Buffett anasema anatumia muda wake mwingi kusoma, angalau kurasa 500 kwa siku) na akiwa na misingi anayoisimamia (Buffett amekuwa na misingi ambayo imemwezesha kuepuka hasara ambazo zimewapoteza wengi).

Ni rahisi kwetu kulaumu mfumo wa elimu kutokuwa na tija kwa watoto.
Ni rahisi kwetu kulalamikia ada kubwa tunazowalipia watoto.
Lakini je tumekuwa tunajiwajibisha vya kutosha kwenye wajibu wetu wa kuwajenga watoto?
Kuwajengea maarifa, maadili na ujuzi ni jukumu namba moja kwetu.
Hakuna mtu mwingine yeyote atakayefanya hayo kwa watoto wetu.
Hata kama tutapambana kiasi gani kujenga mafanikio na utajiri, kama tutashindwa kuyajenga mapema mambo hayo matatu kwa watoto wetu, tutakuwa tumeshindwa maisha yetu yote.
Tubebe sasa huu wajibu na kuufanyia kazi kwa uhakika.
Na wala usione umechelewa, hata kama watoto wameshakuwa wakubwa na ulishakosea huko nyuma, una nafasi nyingine ya kufanya kitu sasa.
Anza kufanyia kazi hili mara moja na litaleta matokeo mazuri.

Tuwajengee maarifa kwa kuweka vichwa vyao sawa.
Tuwajengee maadili kwa kuiweka mioyo yao safi.
Na tuwajengee ujuzi kwa kuiweka mikono yao ‘bize’.
Nini kinashindikana hapo?
Tufanye wajibu wetu, hatuna wa kumlaumu kama hayo yatatushinda.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe