3194; Sehemu ngumu zaidi kwenye mipango.

Rafiki yangu mpendwa,
Watu wengi huwa hawapati mafanikio makubwa kwenye maisha yao.
Na siyo kwa sababu hawataki kufanikiwa, wanakuwa wanataka sana.
Pia siyo kwa sababu hawaweki mipango ya kufanikiwa, wanaiweka sana tu.
Na pia siyo kwamba hawaanzi kufanyia kazi mipango yao, huwa wanaanza wakiwa na shauku kubwa.
Lakini sasa, huwa wanashindwa kuvuka sehemu ngumu zaidi ya mipango yao ya mafanikio.
Sehemu hiyo siyo kupanga wala kuanza, bali kuendelea na mpango bila kujali matokeo gani yanayopatikana.

Wakati watu wanaweka mipango, huwa wanaiona njia ikiwa imenyooka kabisa ya kuwafikisha pale wanapotaka.
Wanapanga kuanza biashara, ambayo itawafikia watu wengi na kutengeneza faida kubwa.

Urahisi wa mpango wao unawapa hamasa kubwa ya kuanza na wanaanza kwa matumaini makubwa.
Msukumo wa mwanzo unawafanya wafanye makubwa mwanzoni na waanze kupata matokeo fulani hivi mazuri.

Halafu sasa maisha yanaingilia katikati, wanakutana na ugumu ambao hawakuutegemea na hivyo mpango haukuelezea jinsi ya kuvuka ugumu huo.
Hapo ndipo majaribu makubwa yalipo, ndipo wanaofanikiwa na wanaoshindwa wanapotengana.
Wote wenye mipango ya kufanya makubwa huwa wanapitia kipindi fulani kigumu na chenye anguko kubwa.
Huku wakiangalia kwa nje wanaona kuna fursa nyingine rahisi zaidi ambazo wengine wanaonekana kunufaika zaidi.

Wanaoshindwa wanaamua kuachana na mpango wao wa awali kutokana na ugumu wanaokuwa wamepitia.
Wanakimbilia kwenye fursa mpya zinazoonekana kuwa rahisi.
Halafu unajua nini, mchezo unajirudia tena na kule. Mwanzo unakuwa rahisi kwa sababu ya hamasa kubwa, ni mpaka wanapokutana na ugumu ndipo hamasa inaisha na wanajikuta wakiacha tena.
Hivyo ndivyo mtu anavyojikuta akiwa amefanyia kazi fursa nyingi ndani ya muda mfupi na hakuna mafanikio makubwa anayokuwa ameyapata.

Wanaofanikiwa huwa wanaendelea kukomaa na mpango walioweka licha ya kukutana na magumu kwenye utekelezaji wake.
Wanapopitia magumu wanaangalia ni jinsi gani ya kufanya kwa ubora zaidi ili kupata kile wanachotaka.
Wanajua mafanikio yapo kwenye kitu chochote kile ambacho kinafanyiwa kazi kwa muda mrefu bila kuachwa.
Pia wanajua mambo huwa magumu kabla hayajawa marahisi.
Wanapoona wengine wakiwa na urahisi kwenye fursa zao, wanajua ni kwa sababu wamezifanyia kazi kwa muda mrefu.

Mtu yeyote yule, anayeweza kufanya kitu chochote kile kwa usahihi na kwa muda mrefu bila kukata tamaa na kuishia njiani, ni lazima atafanikiwa.
Wengi hawafanikiwi kwa sababu wanakata tamaa na kuishia njiani mapema.

Hili tunakumbushana, kwa sababu wote tumeshakubali kwamba tumejipata na hatutahangaika tena.
Lakini siyo rahisi kukumbuka ahadi hizo pale mambo yanapokuwa magumu na dunia kuonekana kama imekuelemea.
Kwa kujikumbusha hili kila siku, linakupa nguvu ya kuendelea licha ya magumu unayoweza kuwa unayapitia kwenye mipango uliyonayo.

Unapokutana na ugumu wowote, unapaswa kufurahi, kwa sababu wengi watakwamishwa na ugumu wa aina hiyo, ila wewe utaendelea kusonga mbele bila kusimama.
Ugumu upo kwa ajili ya kuwaondoa wale ambao hawajajitoa hasa kupata kile wanachotaka.
Usikubali kuwa mmoja wa ambao wanajaribu, ifanye asili ijue kwamba unajua unachotaka na hakuna namna utaacha kukipata.

Weka mipango yako ya kukufikisha kule unakotaka kufika, kisha fanyia kazi mipango hiyo kwa mwendelezo bila kuacha.
Hata pale unapokutana na magumu na kuona wengine wanaofanya kama wewe wakikata tamaa, wewe endelea kufanyia kazi mipango yako.
Hivyo ndivyo mafanikio makubwa yanavyojengwa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe