XXII; Kuhusu ubatili wa kuwa njia panda.
Rafiki yangu Mstoa,
Kufanya maamuzi na kuyasimamia kwenye utekelezaji ni kitu ambacho kimekuwa changamoto kwa watu wengi.
Kwa kutaka matokeo fulani, watu hufanya maamuzi sahihi.
Lakini inapokuja kwenye utekelezaji, huwa wanasita kuchukua hatua zinazopaswa kuchukuliwa kulingana na maamuzi waliyofanya.
Hapo watu wanakuwa njia panda, kwa sababu hawataki kuacha kile walichonacho ili kupata wanachotaka.
Hali hiyo imekuwepo tangu enzi na enzi na mwanafalsafa Seneca alimwandikia rafiki yake Lucilius kuhusu hilo kwenye barua yake ya 22 katika mfululizo wa barua zake za kifalsafa.
Hapa tunakwenda kujifunza jinsi kuwa njia panda kulivyo kubaya ili tuweze kufanya maamuzi na kuyatekeleza kwa uhakika.
1. Jinsi ya kutekeleza ushauri kunategemea wakati uliopo.
Seneca anaanza kwa kumwambia rafiki yake Lucilius kuhusu ushauri aliopata wa kuachana na mambo yasiyokuwa na tija kwake, lakini anauliza anawezaje kutekeleza hilo.
Anamwambia ushauri kuhusu jambo unaweza kutolewa, lakini jinsi ya kutekeleza ushauri huo inategemea wakati husika ambapo mtu anafanyia kazi.
Anatoa mfano kwamba daktari anaweza kushauri kuhusu afya, lakini inapokuja kwenye kumtibu mtu, ni lazima awe naye ndiyo aweze kumpa matibabu sahihi.
Anaeleza pia kwamba hata mpiganaji anayekuwa ulingoni, anaweza kuweka mkakati mzuri wa ushindi kwa kumwangalia mshindani wake ambaye yupo hapo.
Kitu kikubwa sana tunachoondoka nacho hapa ni kwa mipango yoyote tunayoweka, tutumie wakati uliopo na yote tuliyonayo katika kuitekeleza.
Tusisubiri mpaka hali iwe ya aina fulani, bali tutumie kile ambacho tayari tunacho katika kutekeleza yale tuliyopanga.
Kupanga halafu usifanye kwa sababu zozote zile ni kujiweka njia panda.
Panga na tumia yote uliyonayo sasa kufanya na kuna hatua utapiga.
Hatua ya kuchukua;
Ukishaweka mipango, tumia yote uliyonayo kwenye wakati uliopo kutekeleza mipango hiyo. Usiahirishe kwa kusubiri hali fulani ya tofauti, tumia vile ulivyonavyo sasa, vinatosha kuanza.
Nukuu;
“There are certain things which can be pointed out only by someone who is present.” – Seneca
“Kuna vitu ambavyo vinaweza tu kuonyeshwa na mtu aliyepo kwa wakati husika.” – Seneca
2. Nenda hatua kwa hatua na siyo ghafla.
Kwenye kufanya mabadiliko makubwa kwenye maisha, watu wengi huchukua hatua kubwa na za ghafla kwa kutaka mabadiliko ya haraka.
Lakini wanachoishia kupata kinakuwa kinyume kabisa na matarajio yao, kwani wanapata anguko na kurudi kwenye kile walichopanga kuachana nacho.
Seneca anamshauri rafiki yake Lucilius kuacha kuhangaika na shughuli nyingi ambazo hazina tija kwake. Lakini anamtahadharisha asiache ghafla, bali aache kidogo kidogo.
Anampa mfano ni kama kulegeza fundo la kamba badala ya kulikata.
Ni kama tu fundo litakuwa gumu ndiyo mtu anaweza kulikata.
Anaendelea kusisitiza kwamba mtu hapaswi kuacha maisha yake yakihangaika na mambo yasiyokuwa na tija kwake.
Kama hawezi kuachana na mambo hayo, ni bora kuachana na maisha yenyewe, kwa sababu yatakuwa yanakosa maana kwake.
Hatua ya kuchukua;
Kwa mabadiliko yoyote unayotaka kuleta kwenye maisha yako, yaendee hatua kwa hatua badala ya ghafla. Kwa njia hiyo utaweza kufikia mabadiliko unayotaka bila hatari ya kurudi nyuma.
Nukuu;
“But I likewise maintain that you should take a gentle path, that you may loosen rather than cut the knot which you have bungled so badly in tying,” – Seneca
“Lakini pia nasisitiza unapaswa kwenda kwa upole, kwa kulegeza fundo ulilosumbuka kulifunga badala ya kulikata.” – Seneca
3. Huwezi kutumia visingizio vya kulazimishwa na wengine.
Seneca anaeleza watu ambao huwa wanafanya vitu halafu wanajitetea kwamba hayakuwa maamuzi yao, bali walilazimishwa na wengine kufanya.
Anaeleza hiyo ni sababu isiyo ya kweli na njia pekee ya kupata matokeo ambayo mtu anayataka ni kuamua kuachana na sababu zozote anazoweza kuzitumia.
Anasema hakuna mtu anayelazimishwa kuhangaika na mambo yasiyokuwa na tija kwake.
Kwa sababu inamtaka mtu kuweka juhudi kwenye kuyafanyia kazi, hivyo kama ataacha kuweka hizo juhudi, moja kwa moja anakuwa ameachana nayo.
Hatua ya kuchukua;
Usitumie visingizio vya wengine kwamba wamekulazimisha kufanya kitu fulani, badala yake chagua kutokuweka juhudi kwenye kitu chochote ambacho hukitaki na utakuwa umeachana nacho bila ya kusumbuka.
Nukuu;
“But no one is compelled to pursue prosperity at top speed; it means something to call a halt, – even if one does not offer resistance, – instead of pressing eagerly after favouring fortune.” – Seneca
“Lakini hakuna anayelazimishwa kukimbizana na utajiri kwa kasi kubwa; mtu anaweza kuamua kuacha, hata kama siyo kwa kupinga, basi kwa kuamua kutokuendelea kuweka juhudi.” – Seneca
4. Utumwa haushikilii watu, bali watu ndiyo wanashikilia utumwa.
Seneca anasema ukiangalia vitu ambavyo watu wanavilalamikia, unaona dhahiri kwamba ni vitu ambavyo wao wenyewe wamechagua kuwa navyo.
Anasema watu wanapenda matunda ya ugumu wanaokuwa wanapitia, ila wanakuwa wanauchukia ugumu wenyewe.
Anaendelea kusema watu wanalalamikia matamanio yao kama wanavyolalamilia ‘michepuko’ yao, kitu ambacho wanakuwa wamejitakia wenyewe, lakini kinawasumbua.
Kikubwa ambacho Seneca anatuonyesha hapa ni kwamba, yale tunayoyalalamikia, ni sisi wenyewe tumeyapa nguvu.
Hivyo kama tunataka mabadiliko, tuache kuyapa mambo nguvu ambazo zinaishia kutusumbua sisi wenyewe.
Hatua ya kuchukua;
Usilalamikie kitu ambacho wewe mwenyewe ndiyo unakipa nguvu, chagua kuacha kukipa kitu uzito na kitakosa nguvu ya kukusumbua.
Chochote unacholalamikia, jiulize ni kwa jinsi gani wewe mwenyewe unakipa nguvu kisha acha kufanya hivyo na kitaacha kukusumbua.
Nukuu;
“It is so, my dear Lucilius; there are a few men whom slavery holds fast, but there are many more who hold fast to slavery.” – Seneca.
“Hivyo basi rafiki yangu Lucilius; kuna watu wachache ambao utumwa unawashikilia, lakini kuna wengi anbao wanaushikilia utumwa.” – Seneca
5. Unayaacha maisha ukiwa hovyo kuliko ulivyoyaanza.
Seneca anashirikisha nukuu ya Epicurus ambapo anasema watu wengi wanayaacha maisha kama walivyoyaanza, akiwa anamaanisha watu walizaliwa wakiwa hawana kitu na wanapokufa hawaondoki na kitu.
Lakini Seneca anasema kauli hiyo siyo kweli, kwani watu wengi wanayaacha maisha wakiwa hovyo kuliko walivyoyaanza.
Anasema hakuna mtu alizaliwa akiwa na tamaa au hofu, yote hayo watu wamejifunza kwenye maisha na wanateseka nayo maisha yao yote.
Watu wanajikuta wakiishi maisha ya mateso kwa sababu ya tamaa na hofu zinazowatawala, na hivyo kuyamaliza maisha wakiwa hovyo kuliko walivyoyaanza.
Hatua ya kuchukua;
Usikubali kitu chochote ambacho hukuzaliwa nacho kiyaharibu maisha hako. Epuka kutawaliwa na tamaa na hofu au imani nyingine zozote zinazokunyima uhuru wa kuyaishi maisha yako. Ulizaliwa ukiwa huru, hakikisha pia unakufa ukiwa huru.
Nukuu;
“Nature should scold us, saying: “What does this mean? I brought you into the world without desires or fears, free from superstition, treachery and the other curses. Go forth as you were when you entered!” – Seneca
“Asili inatukemea ikisema; ‘Hii ina maana gani? Nilikuleta hapa duniani ukiwa huna tamaa au hofu, ukiwa huru na imani za kishirikina na laana. Ondoka hapa duniani ukiwa kama ulivyoingia.” – Seneca
6. Unachohangaika nacho kuhusu maisha siyo sahihi.
Seneca anamalizi barua hii akionyesha jinsi ambavyo watu wanahangaika na vitu visivyo sahihi kwenye maisha yao.
Anasema watu wengi wanahangaika na kuishi maisha marefu badala ya kuhangaika na kuishi maisha mazuri.
Anaeleza kuishi maisha mazuri ipo ndani ya udhibiti wa mtu, lakini kuishi maisha marefu ipo nje ya udhibiti wake.
Hatua ya kuchukua;
Hangaika na kuishi maisha bora kwako, kitu ambacho unaweza kukidhibiti kuliko maisha marefu ambayo yapo nje ya uwezo wako, kwa kuwa hujui lini utakufa.
Ukiweza kuzidhibiti hisia zako na kufanya yaliyo sahihi mara zote, utakuwa na maisha mazuri.
Na uzuri ni ukiwa na maisha mazuri, kuna uwezekano mkubwa yakawa marefu pia.
Nukuu;
“Men do not care how nobly they live, but only how long, although it is within the reach of every man to live nobly, but within no man’s power to live long.” – Seneca
“Watu hawajali jinsi gani wataishi maisha mazuri, bali wanahangaika na kuishi maisha marefu; japo ipo ndani ya uwezo wa kila mtu kuishi maisha mazuri lakini hakuna mwenye nguvu ya kuamua aishi kwa urefu kiasi gani.” – Seneca
Rafiki yangu Mstoa, tumejifunza kupitia barua hii umuhimu wa kuamua na kutekeleza bila kusubiri wala kusingizia wengine. Pia tumeona jinsi tunavyoweza kuwa huru kama tutaachana na hisia za hofu na tamaa na imani za kishirikina.
Tuyafanyie kazi haya kwa kupambania kuwa na maisha mazuri kwetu ili tuondoke hapa duniani tukiwa bora kama tulivyokuja na siyo tukiwa hovyo zaidi.
Kutoka kwa Mstoa mwenzako,
Kocha Dr Makirita Amani.
Asante Kocha,
Nimejifunza kudhibiti hofu na tamaa, kuacha ushirikina na laana ili maisha yangu yawe mazuri badala ya kung’ang’ana kuishi maisha marefu ambayo sina uamuzi nayo. Nikiishi maisha mazuri, inaweza kuwa bahati nzuri kwangu yakawa maisha marefu.
LikeLike
Hakika, tupambanie maisha mazuri, na urefu utakuja wenyewe.
LikeLike
Asante Kocha, nitaondoka duniani kama nilivyokuja, bila hofu wala woga..sitaung’ang’ania umaskini huku nikiulalamikia Bali nitaachana nao.
Kuachana na kitu kibaya nitaacha kuweka juhudi kwa kitu hicho na hapo nitakuwa nimeachana nacho kwa hakika, nitaweka juhudi katika Yale ninayoyataka kwelikweli
LikeLike
Kila la kheri.
LikeLike
Asante Kwa barua hii naendelea kujifunza zaidi
Asante sana
LikeLike
Karibu
LikeLike