3196; Kugundua upya tairi.
Rafiki yangu mpendwa,
Huwa kuna ngazi tatu kwenye kujifunza vitu vipya.
Ngazi ya kwanza ni ya upumbavu.
Kwenye ngazi hii mtu hajifunzi kabisa kwa kujiona tayari anajua kila kitu.
Hii huwa ni ngazi hatari kwa sababu mtu anakuwa hajui kama hajui.
Ngazi ya pili ni ya ujinga.
Hii ni ngazi ambayo mtu anajifunza kutokana na makosa yake mwenyewe. Anafanya kitu na kukosea, kisha kujifunza na kutokurudia tena.
Hii huwa ni ngazi nzuri ya kujifunza kwa sababu mtu anajua kile ambacho hajui.
Ngazi ya tatu ni werevu.
Kwenye ngazi hii mtu anajifunza kutokana na makosa ya watu wengine na hivyo kutokuyarudia kabisa.
Hapa mtu anaangalia nini wengine wamefanya wakakosea kisha yeye anafanya tofauti.
Hii ndiyo njia bora kabisa ya kujifunza, kwa sababu huongii gharama kubwa ya kufanya makosa wewe mwenyewe.
Ngazi ya upumbavu ni hatari kwa sababu mtu anakuwa hajui kwamba hajui. Na hilo linapelekea afanye makosa mengi, lakini bado pia hajifunzi, hivyo anaendelea kuyarudia na kuzidi kuumia.
Na ubaya wa upumbavu hata kuumia mpumbavu huwa haumii, bali wale wa karibu yake ndiyo huwa wanaumia.
Jitahidi sana usiwe mpumbavu, kwa sababu utawaumiza sana wengine.
Ngazi ya ujinga ni ngumu na inayochelewesha mtu kupata matokeo anayotaka. Hiyo ni kwa sababu makosa ya kufanya ni mengi, hivyo mpaka mtu amalize kufanya makosa yote peke yake, muda unakuwa umeenda sana.
Na kwa kuwa maisha yetu hapa duniani ni mafupi, ujinga ni njia ya kujichelewesha.
Kinachowaweka watu kwenye ngazi ya ujinga ni uvivu na kiburi.
Wanakuwa na uvivu wa kujifunza, kwa kuona bora wafanye kuliko kujifunza kwanza. Wanaweza kuona kama wanaokoa muda, ila wanaishia kuupoteza zaidi.
Kiburi wanachokuwa nacho wajinga ni cha kudhani kwamba wao ni tofauti. Wanaona wale walioshindwa kwenye kitu fulani hawakuwa wanajua, hivyo wao wanajua zaidi.
Wanafanya kwa kuona wao ni tofauti na hivyo watapata matokeo ya tofauti, lakini mwisho wa siku wanajikuta wameangukia kule kule walikoangukia wengine.
Kwa kifupi walio kwenye ngazi ya ujinga ni kama wanajaribu kugundua upya tairi.
Huenda kweli kuna muundo wa tofauti wa tairi kuliko tulivyozoea sasa, lakini hizo rasilimali utakazopoteza kwenye huo mchakato wa ugunduzi, zingefanya mengine makubwa kama ungetumia tu tairi ambazo tayari zipo.
Ni kweli unaweza kuwa tofauti na wengine na unaweza kuwa unapenda kufanya kwa namna yako zaidi kuliko kujifunza, lakini kumbuka maisha ni mafupi na ushindi siyo mateso uliyopitia, bali matokeo uliyopata.
Ngazi ya werevu ni bora sana kwa mtu yeyote anayetaka kupiga hatua kubwa bila kutumia vibaya rasilimali zake. Kwenye ngazi hii mtu anaweza kuwa na ufanisi mkubwa kwa kufanya yale tu ambayo tayari yameshaonyesha matokeo mazuri kwa wengine huku akiepuka yale ambayo hayakufanya vizuri kwa wengine.
Pamoja na ubora wa njia hii, bado wengi hawaitumii kwa sababu ya uvivu na kiburi tulivyoona kwenye ngazi ya ujinga.
Lakini pia watu huwa wana mtazamo tofauti kuhusu mafanikio. Wengi hupenda waonekane wameteseka sana kufanikiwa, wakati mwisho wa siku watu hawajali sana umepita njia gani kupata ulichonacho, hapo ni hata kama watajali kuhusu ulichopata.
Huwa hakuna njia ya mkato ya mafanikio, lakini kujifunza kutokana na makosa ya wengine kunakupunguzia mahangaiko mengi na kukuokolea muda wako.
Kama ungekuwa unaishi milele, ungeweza kutumia njia ya ujinga ili ufanye majaribio yote peke yako na huenda ukaweza kuja na kitu cha tofauti na dunia ikajifunza.
Lakini kwa ufupi wa maisha yako hapa duniani na hatua kubwa unazopaswa kupiga, kuwa tu mwerevu.
Acha uvivu na kiburi, jifunze kutoka kwa wengine na kamwe usirudie makosa ambayo tayari wameshayafanya na yakawagharimu.
Hata kama unajishawishi wewe uko tofauti kiasi gani, jikamate haraka kwenye hicho kiburi, inapokuja kwenye kukosea, haupo tofauti kama unavyodhani.
Huwa kuna kauli maarufu inayosema mafanikio huwa yanaacha vidokezo (Success leaves clues).
Kwa mafanikio makubwa unayoyataka, usipoteze rasilimali zako kwa majaribio ya aina yoyote yale.
Wewe fanya yale ambayo waliofanikiwa wameyafanya na wakapata matokeo mazuri.
Iga kwanza hayo kwa uhakika mpaka upate matokeo mazuri ndiyo unaweza kubadili vile unavyotaka.
Lakini unapokuwa unaanzia chini kabisa, acha uvivu, acha kiburi.
Chagua njia sahihi ya mafanikio na ifuate hiyo kwa msimamo mpaka ufanikiwe.
Usihangaike na majaribio, maisha yako ni mafupi sana kuhangaika na mengine yoyote yasiyokupeleka kwenye mafanikio unayoyataka.
Usiwe mpumbavu kwa kuona tayari unajua kila kitu.
Usiwe mjinga wa kujifunza kila kitu kwa kukosea wewe mwenyewe.
Kuwa mwerevu kwa kujifunza kwa wengine na kufanya yale yaliyo sahihi pekee.
Huhitaji kugundua upya tairi, tumia zilizopo tayari kufika kule unakotaka kufika.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe
Asante sana Kocha ntavuka Daraja hili kwa hakika kwasababu naamini kila jambo linaweza kufanikiwa kama tutachukua hatua kubwa
LikeLike
Vizuri sana.
LikeLike
Ni vema kuwa mwerevu mimi kufikia mwisho kabla ya kuingia kwenye bm nilikua kwenye hatua ya mjinga ila sasa nimehama niko kwenye upande wa waerevu nimeacha kiburi na ujinga najifunza kwa wengine na kufanya kwa kuboresha ili kupata matokeo makubwa
LikeLike
Vizuri sana.
LikeLike
Asante kocha,Siitaji kufanya mambo mapya bali inabidi niweke nguvu kubwa kwa ninachokifanya kwa sasa ili niweze kufika ninakopataka.
LikeLike
Safi, kaa humo.
LikeLike
Huhitaji kugungua upya tairi, tumia zilizopo tayari kufika kule unakotaka kufika
LikeLike
Hakika
LikeLike
Asante kocha hatua ninayokwenda kuchukua ni naendelea kujifunza kupitia wale waliofanikiwa na kuyafanyia kazi ili kupata matokeo bora
LikeLike
Kila la kheri.
LikeLike
Huhitaji kugundua upya tairi, tumia zilizopo tayari kufika kule unakotaka kufika.
LikeLike
Ndiyo
LikeLike
Asante Kocha,
Nimejifunza sihitaji kugundua upya tairi, nitatumia ambazo tayari zipo kufika kule ninakotaka kufika.
LikeLike
Vizuri
LikeLike
Nitajifunza Kama Mwerevu na sio kujifunza Kama Mpumbavu. Nitaitumia makosa ya wengine kujifunza na kupata matokeo.
LikeLike
Kila la kheri.
LikeLike
Tuwe welevu tujifunze Kwa wengine ili tupate matokeo makubwa kwenye kipindi hiki kifupi Cha maisha yet
Asante sana
LikeLike
Hakika
LikeLike
Ni kweli kuwa ujinga ni sawa na kugundua tairi jipya. Ni kupoteza muda na rasilimali.
Sitakuwa mpumbavu kwa kus Hania najua Kumbe sijui
Sitakuwa Mjinga kwa kujifunza kutokana na makosa yangu mwenyewe
Nitakuwa mwerevu kwa kujifunza kutoka na na makosa ya wengine ili mimi nisiyarudie.
Asante
LikeLike
Vizuri sana.
LikeLike