3198; Siyo kilema.

Rafiki yangu mpendwa,
Ni mara ngapi umewahi kuwaambia watu kwamba lengo lako ni kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yako, halafu watu hao wakaanza kukuonyesha lengo lako siyo sahihi?
Wanakuambia kuweka lengo la utajiri ni tamaa na hata hivyo pesa huwa hazileti furaha!

Sasa hebu niambie kitu kimoja, hao watu wanaokuambia hayo, hali yao kifedha wanakuwaje?
Ukweli ni kwamba, watu hao wanaojipa wajibu wa kukushauri kuhusu fedha kwa kukuonyesha fedha siyo nzuri kwako, nao wenyewe hawana fedha.

Mara zote ni watu wasio na fedha ndiyo watakupa ushauri wa kukukatisha tamaa pale unapopanga kupata fedha zaidi.
Ni masikini ndiyo utawasikia wakisema fedha haiwezi kununua furaha.

Na hiyo ni sababu kwa nini hupaswi kuwasikiliza, kwa sababu wanachokushauri siyo sahihi.
Kuchukua ushauri wa jambo lolote lile kwa mtu ambaye hana hicho anachoshauri ni kujipoteza.

Lakini labda tuseme ushauri unaopewa kwamba utajiri siyo mzuri kama unavyodhani.
Kwa nini ukubali kwa kuambiwa?
Kwa nini usiupate ili uweze kujionea wewe mwenyewe?

Kwa sababu utajiri siyo kilema kwamba ukishakipata basi umekipata na huwezi kuondokana nacho.
Kwa nini usiamue kupambana kuupata utajiri huo mkubwa kabisa na ujionee wewe mwenyewe kama utakukosesha furaha kama wengi wanavyosema.

Na kama baada ya kupambana kujenga utajiri mkubwa utagundua fedha siyo muhimu kama ulivyodhani basi unaweza ukazigawa kama misaada kwa wale wenye uhitaji.
Unaweza kugawa mpaka ubaki na kile kiasi unachoona kinakupa utulivu.

Hapo unakuwa umepata faida zaidi ya moja, kwanza unakuwa umetumia uwezo wako mkubwa kuzalisha matokeo makubwa, pili unakuwa umejijengea uzoefu binafsi kwenye aneo hilo na tatu unakuwa umeyafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi.

Kama utaweza kujenga utajiri mkubwa na ukagundua siyo muhimu kwako kama ulivyofikiri, nakuhakikishia kuna watu wenye uhitaji mkubwa sana wa fedha kwenye maisha yao, ambao ukiweza kuwapatia fedha utakuwa umeleta tofauti kubwa sana kwao.

Na kwa kuwa kujenga utajiri siyo kilema, pambana kuujenga na kama hutaufurahia kama ulivyotegemea, ugawe kwa wale wenye uhitaji.
Kwa kufanya hivyo utaweza kurudi kwenye ngazi yoyote uliyochagua huku pia ukiwanufaisha wengine.

Baada ya kusema hayo, turudi kwenye vipaumbele vyako kwenye maisha.
Pitia ratiba zako za siku, siyo zile unazopanga, bali yale hasa unayofanya.
Jiulize kwa jinsi umekuwa unaziendesha siku zako, ni matokeo gani ambayo ni rahisi zaidi kuyapata?

Unaweza kujiwekea vipaumbele vingi kwa mipango na maelezo, lakini matokeo yako yatatokana na yale hasa unayofanya na siyo unayopanga kufanya.

Kutengeneza utajiri mkubwa kwako kinapaswa kuwa kipaumbele namba moja kwako.
Na hilo halipaswi tu kuwa kwa maneno na mipango, bali kwa uhalisia wa yale unayofanya.

Kwenye muda wako wa kufanya kazi/biashara, angalia kila ambacho umekuwa unafanya na jiulize kina mchango kiasi gani kwako kufikia utajiri mkubwa unaoutaka?
Kama unatumia muda wako wa thamani kufanya mambo ambayo hayana mchango kwenye lengo lako la utajiri ulilonalo, unakuwa umechagua kupoteza muda huo.

Chochote ambacho unataka kupata na umekiweka kama kipaumbele cha kwanza kwako, lazima kijidhihirishe kwa matumizi yako halisi ya muda.
Kwa muda wa kazi usiopungua masaa 10 kwenye siku yako jambo hilo la kipaumbele cha kwanza ndiyo linapaswa kuchukua muda huo mwingi.

Unaweza kuwa na malengo mengi, lakini lengo lako namba moja linapaswa kuwa ni kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yako.
Kwa sababu ni lengo ambalo ukilifikia linarahisisha malengo mengine yote uliyonayo.
Weka kila ulichonacho kwenye hilo lengo lako kuu na utaweza kulifikia haraka kuliko ukitawanya rasilimali zako kwenye mambo mengi.

Nikukumbushe hii ndiyo maana tupo kwenye lengo la UBILIONEA na hatua ya kwanza ni kufikia ULAKIONEA.
Kabla ya kufikia ulakionea, mengine yote tunapaswa kuyasimamisha na kila rasilimali tuliyonayo kupelekwa kwenye kulifikia hilo lengo.
Tunalifanya lengo hilo kuwa ndiyo kipaumbele pekee kwenye maisha yetu na muda wetu.
Na tunalipambania hasa bila ya kujizuia kwa namna yoyote ile.

Matokeo tutakayoyapata kwenye kufanyia kazi lengo la LAKIONEA yatatupa mwanga wa namna gani tupambanie malengo ya juu zaidi ya UMILIONEA na UBILIONEA.
Lakini kabla ya hayo ya juu, wajibu mkuu ni kufikia kwa uhakika lengo la chini kwanza.

Itakuwa ni jambo la ajabu sana kulikataa lengo kubwa na la juu kwamba halikufai, wakati hata lengo la chini yake umelishindwa kabisa.

Tumia muda wako wa siku nzima na kila siku kwa namna ambayo huwezi kushindwa kufikia lengo la kifedha ulilonalo.
Kwa sababu ushindi kwenye maisha huwa unayokana zaidi na kutokuacha kufanya.

Nikirudi kwenye dhumuni la ukurasa huu, utajiri siyo kilema kwamba ukishaupata unakubadili moja kwa moja.
Hivyo pambana kujenga utajiri mkubwa kadiri uwezavyo.
Na kama utagundua hilo halikuwa sahihi kwako, baada ya kuwa umeshaujenga utajiri huo, una fursa ya kuugawa kwa wale wenye uhitaji.
Kama hilo la kugawa utajiri kwa wale wenye uhitaji nalo halitakupa furaha, basi tatizo siyo fedha kama ulivyodhani, bali tatizo ni wewe binafsi.

Yote kwa yote, hata kama una matatizo binafsi yanayokuzuia usifurahie chochote, bado kuwa na fedha nyingi na za kutosha kunayafanya maisha yako kuwa bora zaidi.

Usiwasikilize masikini pale wanapokukatisha tamaa kwenye lengo lako la kifedha maana hawajui wanachoongea.
Pata fedha na ujionee wewe mwenyewe na hapo utaamua hatua sahihi kwako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe