3201; Madhara ya kutokusikiliza.

Rafiki yangu mpendwa,
Mtu mmoja amewahi kuandika kwamba unapochagua menta au kocha kwenye maisha yako, unatakiwa umsikilize kile anachokuambia.

Hiyo ni kwa sababu lengo la kuwa na menta au kocha ni kupunguza urefu wa safari, kwa kuepuka kurudia makosa ambayo yeye amewahi kufanya au alishajifunza.

Lakini huwa kuna hali fulani ya kibinadamu ya kutaka sana kufanya kile unachotaka kufanya, hata kama ni kinyume na unavyoambiwa na menta au kocha wako.
Unakuwa unaona kama kile anachokushauri kwako ni tofauti na kuna namna unaweza kukifanya kwa tofauti kuliko yeye.

Na kweli unafanya, kinyume na vile menta au kocha amekushauri na matokeo wote tunayajua, unaishia kupata kile ambacho menta au kocha alikuambia utapata lakini hukusikia.

Hilo ni kosa ambalo mimi binafsi nimekuwa nalirudia rudia sana kwenye huduma ninazotoa na linanigharimu kwenye upotevu wa nguvu na muda kwenye mambo ambayo mwisho wake matokeo yake yanakuwa siyo mazuri.

Mara nyingi nimekuwa najiambia wacha nifanye hili kama jaribio ili nione matokeo yake.
Na matokeo yamekuwa yanakuja vile vile kama yalivyoelekezwa kuja.
Sasa hapo hakuna kipya nakuwa nimegundua, zaidi ya kupoteza muda na nguvu, huku nikijizuia kupata fedha zaidi kwa kufanya yaliyo sahihi.

Nina mamenta mbalimbali kwenye maeneo mbalimbali ya maisha yangu.
Ambao nimechagua kujifunza kwao kupitia kusoma maandiko yao mengi na kuboresha safari yangu ya maisha kupitia yale ninayojifunza kwao.

Mmoja wa mamenta hao ni Charlie Munger ambaye nimechagua kuwa menta kwenye eneo la kujifunza, kufikiri, kufanya maamuzi bora na kuishi miaka mingi huku nikifanya kazi bila kustaafu.
Munger ana miaka 99 na bado anaendelea na kazi zake kama kawaida.

Kupitia kujifunza kwa Munger kuna mengi sana ambayo nimekuwa naondoka nayo na kuyafanyia kazi na yanakuwa na matokeo mazuri.
Lakini kuna maeneo matano ambayo amekuwa anayasisitiza sana, lakini mimi nimekuwa naamua kuyapuuza nikidhani naweza kupata matokeo ya tofauti.
Lakini mara zote matokeo yamekuwa ni kama alivyoeleza.

Eneo la kwanza ni kuhusu kutoa ushauri.
Munger anasema kwa zaidi ya miaka 60 ambayo amekuwa anafanya uwekezaji, amegundua haina maana kumpa mtu yeyote ushauri.
Watu watafanya kile wanachotaka kufanya hata kama utawashauri kwa namna gani.
Na wengine wanakuomba ushauri au unawashauri wakiwa wameshafanya maamuzi au hata kuanza kufanya.
Kwa upande wangu hilo limekuwa hivyo mara zote, nawashauri sana watu, lakini wanaishia kufanya kile wanachotaka kufanya.

Eneo la pili ni ukosoaji.
Munger anasema kwenye maisha yake yote hajawahi kukutana na mtu anayependa kukosolewa.
Anasisitiza ni sifuri kabisa, kila mtu anachukia ndani yake pale anapokosolewa.
Na mimi nimekuwa nadhani naweza kuwakosoa watu kwa namna ya kuwajenga, lakini mwisho wa siku wanachukizwa na hilo.
Hata uwe na nia njema kiasi gani, bado ukosoaji unawaumiza watu.

Swali ni utawezaje kwenda na watu kama hawataki ushauri wala kukosolewa?
Na hapo ndipo eneo la tatu na la nne ambayo Munger amekuwa anasisitiza.

Eneo la tatu ni kujihusisha na watu wanaoaminika.
Kwenye sheria zake sita za maisha marefu na ya mafanikio anasema ameweza kuishi maisha marefu kwa sababu anajihusisha na watu wanaoaminika na kutegemewa.
Hapa napo nimekuwa nakosea sana, nawachelewesha sana watu ambao wamekuwa hawaaminiki.
Watu ambao wanatoa ahadi na hawatekelezi, wanapanga mambo na hawatekelezi.
Nimekuwa nadhani labda wana nafasi ya kubadilika, lakini haijawahi kutokea.
Watu wapo vile walivyo na wataendelea hivyo, chochote watakachokuambia au kukuahidi tofauti ni matamanio tu wanayokuwa nayo, lakini asili yao itabaki vile walivyo.

Eneo la nne ni usibishane na watu.

Munger amekuwa anaulizwa iwapo wamekuwa wanapitia hali ya kutokuelewana na mshirika wake mkubwa na wa muda mrefu (kwa zaidi ya miaka 60) kwenye biashara na uwekezaji, Warren Buffet.
Munger anajibu kuna nyakati huwa wanatofautiana, lakini hawajawaji kubishana au kutokuelewana.
Anasema kwa kipindi ambacho wamekuwa pamoja, ni kama mara 4 hivi wamekuwa wanatofautiana, na hawajakosana wala kubishana.
Mshirika wake Warren amekuwa anashirikisha kwamba wanapotofautiana, Munger huwa anamwambia; “Warren, fikiria zaidi kuhusu hilo. Una akili na niko sahihi.”
Hapo kuna funzo jingine kubwa la umuhimu wa kujihusisha na watu wanaoaminika na kuwaacha kwenye maamuzi wanayofanya hata kama hukubaliani nayo au siyo sahihi.
Nimekuwa nafanya kosa la kubishana na watu pale ninapoona wanachofanya siyo sahihi, lakini imekuwa haina matunda.

Eneo la tano ni imani na sheria.
Munger na Warren wanasema katika kuchagua kampuni ambazo wanawekeza au kununua, huwa wanazingatia vitu hivyo viwili; imani waliyonayo kwa anayeendesha biashara na uzingatiaji wa sheria.
Wanasema wanaweza kuvumilia makosa mengi ya kibiashara, kwa sababu mambo huwa hayatabiriki.
Lakini hawana uvumilivu wowote kwa mtu ambaye anafanya makosa ya kuvunja imani au sheria ambazo zipo.
Ni kitu rahisi kabisa kueleweka hicho, lakini napo nimekuwa nafanya makosa, napoteza muda mwingi na watu ambao siyo waamifu na wanavunja sheria nyingi.
Na hakuna matokeo mazuri ambayo nimekuwa napata kwa watu wa aina hiyo.

Rafiki, huenda na wewe umejifunza vitu hapo, vifanyie kazi ili upunguze muda na nguvu unazopoteza kuhangaika na mambo ambayo hakuna namna yatakupa matokeo unayoyataka.
Usirudie makosa ambayo wengine wameshayafanya au wameshayafundisha.
Muda wetu ni mfupi, tuutumie kufanya yale ambayo ni sahihi na yanatupa matokeo tunayoyataka.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe