3203; Inachukua muda.
Rafiki yangu mpendwa,
Sehemu kubwa ya mambo tunayojifunza kwenye maisha siyo mapya.
Bali tunakuwa tunarudia mambo yale yale kwa namna tofauti tofauti.
Na hiyo ni kwa sababu sisi binadamu huwa tunazoea na kusahau mambo haraka sana.
Tunakuwa tunajua kabisa, lakini kwa mazoea na usahaulifu, tunapotezea na mwishowe tunapata madhara.
Kitu ambacho tunahitaji kujikumbusha mara kwa mara ni kitu chochote kipya huwa kinachukua muda mpaka kiweze kuwa vizuri kama ambavyo mtu unataka.
Na hili asili inatuonyesha kwa mifano halisi kila wakati.
Kiumbe yeyote anayebeba ujauzito, huwa ana muda wake wa ujauzito huo kukomaa. Siyo rahisi kuharakisha zoezi hilo.
Chombo chochote cha moto ambacho kimesimama, kitahitaji nguvu kubwa pale unapokiwasha kianzishe mwendo.
Unapopasha moto kitu ambacho ni baridi, kinahitaji nishati kubwa mwanzoni, na muda wa nishati hiyo kusambaa kwenye kitu hicho ndiyo kipate moto.
Na mtoto mdogo anapozaliwa, huwa anachukua muda kufikia kila hatua ya ukuaji.
Mtoto akizaliwa na siku hiyo hiyo akaanza kuongea na kutembea, litakuwa jambo la kushangaza sana na watu watakuwa na wasiwasi mkubwa.
Inachukua muda kwa vitu kuwa vile vinavyopaswa kuwa.
Na huna cha kufanya kwenye huo muda zaidi ya kuendelea kuweka juhudi na kusubiri.
Ni kama kupandisha maji kwenye kisima kwa kutumia pampu ya mkono.
Unahitaji kusukuma pampu hiyo kwa muda ndiyo maji yaweze kutoka.
Utaweka nguvu sana, hasa mwanzoni, lakini hutayaona maji mara moja.
Hilo halimaanishi kwamba nguvu unazoweka hazifanyi kazi.
Zinafanya kazi sana, sema tu ni muda haujafika.
Unachopaswa ni kuendelea kuweka nguvu hizo na maji yajikusanye mpaka kutoka.
Ukiacha tu kuweka nguvu, hata maji kidogo yaliyokuwa yameanza kupanda yanarudi chini yote.
Ukija kuanza tena, inakuchukua muda mrefu zaidi.
Jambo jingine muhimu la kujikumbusha kila mara ni rahisi kuwashauri wengine kuliko wewe mwenyewe kufanyia kazi ushauri huo huo.
Kwa mfano hili tuliloanza nalo hapo, inapokuwa kwa mtu mwingine ni rahisi kumwambia weka juhudi, kuwa mvumilivu, matokeo yatakuja.
Lakini inapokuja kwako mwenyewe ukiwa kwenye hali kama hiyo, unaanza kuhangaika ufanyeje ili upate matokeo ya haraka.
Unaona kama ushauri wa kuweka juhudi na kuwa na subira haukufai wewe kwa hali unayokuwa nayo.
Kwa sehemu kubwa kwenye maisha, ushauri tunaowapa wengine ndiyo ushauri tunaouhitaji sana sisi wenyewe.
Kiasi kwamba kama tungeamua tu kufanyia kazi ushauri wetu sisi wenyewe, tungepiga hatua kubwa sana.
Ushauri ambao tunakuwa tayari zaidi kuwapa wengine, ndiyo ushauri ambao sisi wenyewe tunauhitaji sana.
Hivyo mahali pazuri pa kuanzia kwenye maisha yako ni kwa kila ushauri unaowapa watu wengine, jiulize wewe mwenyewe unaufanyiaje kazi.
Majibu unayoyataka tayari yapo kwenye ushauri ambao umekuwa unakazana kuwapa watu wengine.
Upo mfano wa mama mmoja ambaye alikuwa na kijana mlevi na anayemsumbua kwenye maisha.
Mama huyo akaenda na kijana wake kwa mtu mmoja aliyekuwa na busara na kumweleza kuhusu changamoto za kijana wake. Kisha akamwomba mtu amshauri kijana wake kuacha pombe.
Mwenye busara yule alisikiliza kwa makini kisha akamwambia mama na kijana wake warudi kwake baada ya wiki mbili.
Mama na kija waliondoka na wakawa wanasubiri kwa shauku kubwa watakachokuja kusikia baada ya hizo wiki mbili.
Wiki mbili zikapita na wakarudi kwa mwenye hekima.
Walipofika mtu yule hakuwa na maneno mengi, alisema tu; :Kijana, acha pombe.”
Mama alishangazwa na kumuuliza mtu yule mwenye busara ilimshinda nini kusema hilo walipokuja kwake wiki mbili zilizopita.
Mwenye busara akamjibu; “Wiki mbili zilizopita hata mimi mwenyewe nilikuwa natumia pombe, hivyo ilinibidi niache kwanza pombe kabla sijamshauri mtu mwingine kufanya hivyo.”
Kuna mengi sana ya kujifunza kwenye mfano huo, lakini mawili ya kuondoka nayo kwa uhakika ni haya;
La kwanza na ambalo nimekuwa nalisema sana na inabidi nilirudie kwa sababu tunasahau ni kama hulipwi kwa kuwashauri watu, usipoteze muda wako kufanya hivyo. Badala yake kazana kufanyia kazi ushauri ambao unakuwa na kihere here cha kuwapa watu wengine, maana huo ndiyo ushauri ambao wewe mwenyewe unauhitaji sana.
La pili ni kama unalipwa kuwashauri watu, washauri yale ambayo wewe mwenyewe umeyafanya na hivyo una uzoefu halisi kwenye kuyafanya.
Hilo likufanya uwe halisi badala ya kuonekana unaigiza au kudanganya.
Na pale unapomshauri mtu na akakukatalia ushauri wako, unacheka kabisa ndani yako kwa sababu unajua shida anayoitafuta mtu huyo.
Unapokuwa unashauri mambo ambayo huna uzoefu nayo, watu watakubabaisha na kila wakati utakuwa unayumba yumba sana. Kwa sababu wewe mwenyewe unakuwa hujiamini.
Nimalizie kwa msisitizo kwamba kila kitu kinachukua muda.
Sikuambii hivyo kwa sababu nimesoma mahali.
Kwa sababu ndiyo uhalisia wa safari ya maisha yangu.
Kwa kila jambo nililofanikisha, imenichukua muda mrefu sana, tena zaidi ya nilivyozoea.
Ninapowaona watu ambao wanaanza sasa kule ambapo nilipita muda mrefu ila wanataka kwa haraka zaidi, huwa nacheka ndani yangu. Kwa sababu najua wanazidisha tu ugumu wa safari yao.
Sawa, nimalize na mfano mwingine, ambao nimeshaushirikisha hapa zaidi ya mara moja. Lakini kuna mtu atafurahia kujifunza kupitia mfano huo kama vile ni kitu kipya kabisa. Sina tatizo na hilo, maana najua asilimia 90 ya kazi yangu ni kurudia mambo yale yale bila kuchoka.
Kijana mmoja alikuwa anataka kuwa mtawa, hivyo akaenda kwa mtawa ambaye ni mzoefu na mbobezi. Akamuuliza mtawa yule; “nataka kuwa mtawa mbobezi kama wewe, itanichukua muda gani?”
Mtawa akamjibu; “miaka 10.”
Kijana akamuuliza tena; “nipo tayari kufanya kazi usiku na mchana, itanichukua muda gani?”
Mtawa akamjibu; “miaka 20.”
Somo la kujifunza hapo?
Tayari unalo, lifanyie kazi.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe
Kweli inachukua muda
LikeLike
Ndiyo
LikeLike
Hakika kila kitu kinahitaji muda kuleta matokeo na ukilazimisha kufupisha badala ya muda huo kuwa mfupi ndiyo unazidisha zaidi ya mara mbili. Hivyo muhimu ni kuipa kila kitu muda. Asante
LikeLike
Ndiyo
LikeLike
Niufanyie kazi ushauri ninaotaka kuwapa watu kwanza kabla ya kuufanyia kazo nione matokeo na kama unafanya kazi ndkwangu ndiyo naweza kumshauri mtu na pia kwa kua ushauri haulipwi siyo lazima kushauri tupunguze kiherehere cha kushauri watu hata bila kuombwa na tukifanyia kazi wataona wenyewe
LikeLike
Tuwe bize na mambo yetu.
LikeLike
Asante sana kocha kwa somo nzuri hapa nimejifunza mengi hasa kwa upande wangu nilete mfano kuna Wasaidizi wangu yaani wale wa mama ambao huwa wanafanya kazi kwenye kiwanda kazi yakuchagua mbegu za mawesa tukimaliza kazi yaani tumeuza bidha yote na nimeagiza mzigo mwingine huwa wanakuja kwangu nakuniambia kwamba wao huwa hawataki kukaa hivyo bila kazi kwanini boss usifanye kama viwanda wengine yaani wao huwa wanafanya kazi kila Siku? Huwa nawajibu kwamba huwezi ukamzaa mtoto ukapenda aseme Siku hiyo hiyo aliyo zaliwa na atembee pia viwanda hivyo nivya zamani sisi ndiyo tunaanza kazi ni step by step 🪜 na hapa pia kumenikumbusha hiyo dhana ya kutaka njia za mkato ni ndefu sana kama mtawa alivyo mjibu Kijana Asante kocha
LikeLike
Hatua kwa hatua.
LikeLike
Siyo rahisi kupingana na asili hata kwa kutumia uzoefu wa watu waliokutangulia au menta na kocha
LikeLike
Hakika
LikeLike
Ahsante Doctor kwa somo zuri saana lenye kufikirika,mimi kikubwa ambacho nimejifunza hapa, nikwamba ninapaswa kumshauri mtu kwenye ushauri ambao tayari ninauzoefu nao kwenye utendaji kazi pale pale endapo atakuwa na uhitaji kutoka kwangu,na siyo kujitia kihere khere kwenye kushauri vitu ambavyo sijaombwa kufanya hivyo na vile vile kila safari yenye mafanikio makubwa na ya ukwel inahitaji uwekaji wa muda mrefu na kukaa kwenye mchakato sahihi.
LikeLike
Tuhangaike na mambo yetu.
LikeLike
Asante kocha,kwenye safari ya maisha lazima nitumie ushauri ninaotaka kuwapa wengine je mimi nimeufanyia kazi ? Lazima nijipe mda kwa kila jambo sio kuyumbishwa yumbishwa na kuwa na kihere here.
LikeLike
Kila la kheri.
LikeLike
Asante kocha kwa somo linatufundisha kuweka kazi zaidi na matokeo bora ni suala la muda, tunapaswa kupambana zaidi na ushauri tunaotoa kwa wengine nasi unatuhusu
LikeLike
Karibu.
LikeLike
Kila kitu kwenye maisha yetu kinahitaji muda na hiyo ndio asilli inavyofanya kazi …..ni ajali pekee ndio inayotokea Kwa haraka
Asante sana
LikeLike
Hakika, ajali inatokea kwa haraka, lakini pia inakuwa imejengewa mazingira ya kutokea muda mrefu.
LikeLike
Asante Kocha,
Mfano wa mtawa umenifundisha/ umenikumbusha jambo muhimu sana: njia ya “mkato” ina “makato” mengi.
LikeLike
Ukikimbilia njia za mkato unaishia kubaki na mikato.
LikeLike
ASANTE sana
LikeLike
Karibu.
LikeLike
Kadiri unavyokitaka kitu kwa haraka ndivyo itakavyokuchukua muda mwingi zaidi kukipata kitu hicho
LikeLike
Hakika
LikeLike
Kila kitu kinahitaji muda kwenye maisha yetu.
Huwezi kwenda kinyume na asili hata siku moja.
Asante sana Kocha Dr. Makirita Amani
LikeLike
Kabisa
LikeLike
Asante sana kocha, hakika so vizuri kumshauri mtu jambo ambalo hufanyi,nimependa sana mfano wa mwenye Hekima tena kwa maneno machache
LikeLike
Ndiyo
LikeLike
Inachukukwa muda kwa vitu kuwa vile vinavyotakiwa kuwa. Wala huna cha kufanya zaidi Ya kuweka juhudi na kusubiri. Na subira huvuta heri.
Asante
LikeLike
Kabisa.
LikeLike
Kila ushauri ninaotaka kuwapa watu napaswa kwanza kuufanyia kazi mimi.Na muhimu ni kwamba napaswa kujua kiwa inachujua muda!
LikeLike
Hakika
LikeLike
Asante sana Kocha. Muda na KAZI bila kuacha = matokeo
LikeLike
Tukae humo.
LikeLike