3206; Raha ya ukuaji.

Rafiki yangu mpendwa,
Viumbe wote hai huwa wana sifa ya ukuaji.
Na sisi sote huwa tunafurahia sana ukuaji kwenye viumbe wote hai wanaotuzunguka.

Ukiwa na wanyama unaowafuga au mimea uliyopanda, ukuaji ndiyo kitu ambacho unakifuatilia sana.
Unakuwa unajua kila hatua ambapo kitu kipo na hatua gani inayofuata kwenye ukuaji.

Inapokuja kwenye watu muhimu kama watoto wetu, ufuatiliaji wetu kwenye ukuaji unakuwa ni wa karibu zaidi.
Wazazi ambao ndiyo kwa mara ya kwanza wanapata mtoto, huwa wanakuwa na shauku kubwa kwenye kila hatua ambayo mtoto anapiga.
Wakati mwingine wanahesabu kitu kuwa ukuaji wakati bado muda wake haujafika.
Kwa mfano mtoto ambaye bado ni mchanga kabisa, anapotoa sauti za ba ba ba.
Kwa matamanio makubwa ya ukuaji anbayo mzazi anakuwa nayo, anaweza kusema mtoto katamka baba.
Hata kama mtoto bado hajafikia kuongea, mzazi atafurahia hilo, japo siyo sahihi.

Nguvu hiyo ya ukuaji ipo kwenye kila eneo na kila kitu kwenye maisha yetu.
Inapokuja kwenye biashara tunazofanya, nazo zina nguvu ya ukuaji ndani yake.
Biashara zinazaliwa, kukua kisha kuzeeka na kufa.
Ili kuvuka kuzeeka na kufa, biashara inapaswa kubaki kwenye hatua ya ukuaji wa kasi mara zote.
Hapo ndipo raha ya ukuaji ilipo; unajua kabisa nini kinapaswa kutokea na una uwezo wa kusababisha matokeo hayo.

Wajibu wetu mkubwa kwenye biashara tulizonazo ni kuhakikisha mara zote zinakuwa kwenye ukuaji wa kasi.
Ni ukuaji huo wa kasi ndiyo unaiepusha biashara na changamoto mbalimbali zinazoweza kuiua.

Ukuaji wenyewe una hatari ya kuiua biashara, lakini hatari ni kubwa zaidi kama kusipokuwepo na ukuaji kabisa.
Hivyo una wajibu mkubwa wa kuhakikisha unaendelea kusukuma ukuaji kwenye biashara yako, kwa sababu ndipo nguvu ya kupona kwa biashara yako ilipo.

Ni raha iliyoje kuona kitu kinatoka hatua moja kwenda hatua nyingine, ambayo ni imara zaidi.
Hii ni raha ambayo una uwezo wa kuipata kila mara kupitia kuikuza biashara yako.
Una nafasi ya kuendelea kupata ushindi kupitia ukuaji endelevu wa biashara yako.

Chukua wajibu wako wa kuhakikisha biashara yako inaendelea kukua na upate raha kwa uendelevu.
Usiridhike na hatua yoyote ambayo biashara yako imefikia.
Bali jua kuna fursa ya kupiga hatua zaidi na zaidi.
Ni kupitia kuiwezesha biashara kupiga hatua hizo kwa msimamo ndiyo penye nguvu ya ukuaji endelevu wa biashara.

Kwenye biashara, unapoacha tu kukua, ndiyo unakuwa umeanza kuzeeka na kufa.
Zuia hatari hizo kwa kuiweka biashara yako kwenye mchakato wa ukuaji mara zote.
Mchakato huo utaiimarisha biashara na wewe mwenyewe pia.
Ufanyie kazi mara zote.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe