3207; Simu ziite sasa.

Rafiki yangu mpendwa,
Nimekuwa naona watu wakiweka picha za bidhaa mbalimbali wanazouza kwenye mtandao (wasap status) pamoja na bei zake.
Kisha wanaweka maelezo; simu ziite sasa.
Nimekuwa nachukulia kauli hiyo kama utani tu na kuona hakuna muuzaji aliye makini anayekuwa anategemea kweli kwamba simu zitaita.

Siku moja nilikuwa namfanyia usaili mtu wa mauzo na kwenye kujibu maswali ya awali alieleza amewahi kufanya kazi ya mauzo kwenye kampuni fulani.
Maswali yangu mengi yaliegemea kwenye hiyo kazi ya mauzo, nikitaka kujua alikuwa anaifanyaje na nini kilimfanya aiache.
Alinieleza jinsi alivyokuwa anafanya ni hivyo, kuposti picha za bidhaa na kusubiri simu ziite.

Nilipomuuliza kwa nini aliacha hiyo kazi, alijibu biashara haikuwa nzuri, maana alikuwa analipwa kwa kamisheni na hivyo hakuweza kuwa anafanya mauzo ya kutosha.
Nilimuuliza kama kuna kitu cha ziada alikuwa anafanya zaidi ya kuposti hizo bidhaa, akajibu hakuna.
Hapo ndipo niligundua kumbe ‘simu ziite sasa’ ni mkakati kamili ambao watu wanautegemea kwenye mauzo.

Nimekuwa pia nakutana na watu ambao mkakati wao mkuu wa mauzo ni kutuma jumbe kwa watu kwa njia mbalimbali. Wakiamini kwa kutuma jumbe nyingi wataweza kuuza kwa ukubwa.

Sikiliza rafiki, watu wanaweza kuzunguka kwa namna wanavyotaka, lakini mkakati sahihi wa mauzo ni ule unaohusisha kuzungumza na mtu kumshawishi anunue.
Na mazungumzo yanaweza kuwa ya ana kwa ana (ambayo yana ushawishi mkubwa ila huwezi kuyafanya kwa wingi) au kwa njia ya simu (ambayo yana ushawishi mdogo ila unaweza kuyafanya kwa wingi).

Vitu vingine vyote unavyofanya kwenye mauzo ni vya ziada tu, vyenye lengo la kuelekea kwenye mkakati wa mazungumzo.
Hivyo vitu vingine ni kama kurusha jiwe gizani, ukisikia mtu amelia kwamba jiwe limempata, unamwambia apite mbele, huyo ni wa kuuzia.
Kwa lugha nyingine ni hayo mengine unayokuwa unayafanya lengo lake ni kumtaka mtu anyooshe mkono kwamba na mimi nataka.
Na hapo sasa wewe ndiye wa kufanya naye mazungumzo kumshawishi anunue.

Sasa kwa sababu watu wengi wamevurugwa na mambo mengi waliyonayo ya kufanya huku muda wao ukiwa mchache, kuwasubiri wakupigie au kukutafuta ni kujipoteza mwenyewe.
Ni lazima wewe uwatafute, kuhakikisha wanajua unachouza na kuchukua hatua ili kupata hicho unachouza.

Hivyo unaweza kupost kila mahali unakotaka kupost, ukatuma ujumbe kila mahali unakotaka kutuma, lakini lazima uanzishe mazungumzo na watu, tena wengi na siyo wachache.
Ongea na watu kuwashawishi wanunue, hayo ndiyo mauzo. Vingine vyote ni vya ziada tu.

Ni kiburi cha hali ya juu sana kuweka bidhaa/huduma zako mtandaoni kisha kusema; simu ziite sasa na ukaona umeshakamilisha kazi.
Unakuwa unajikuta wewe ni nani au una nini hasa cha kuwafanya watu waache yote wanayofanya na kuanza kukutafuta?

Kuna wabishi watasema huwa tunapost na watu wananunua.
Wacha nikuambia, kila kitu kinachofanyika huwa kinafanya kazi, hata kama ni kwa kubahatisha.
Tunachozungumzia hapa ni jinsi ya kuufanya mchakato uwe wa uhakika kwako badala ya kubahatisha.

Turudi kwenye kanuni ya soko kubwa;
Ni asilimia 3 tu ya soko ndiyo wapo kwenye hitaji la kununua sasa.
Na asilimia hiyo 3 ndiyo inalengwa na watu wote wanaotangaza biashara zao kwa njia mbalimbali.
Hawa ndiyo mara moja moja watakutana na ulichopost na wakapiga simu kweli kupata unachouza.
Na wewe ukaona njia yako ya kupost na kusubiri inafanya kazi, hivyo kuendelea nayo.
Lakini haitakuchukua muda utasema biashara ni mbaya, kwa sababu simu haziiti.

Kuna asilimia 17 ya watu kwenye soko ambao wanakusanya taarifa kuhusu kitu wanachotaka kununua. Wanataka kununua, ila hawana haraka ya kufanya hivyo.
Hawa ndiyo watakutana na kitu ulichopost na wakajiambia wakiwa tayari watakutafuta.
Lakini unajua maisha huwa yanaingilia katikati hapo, anakuja kujikuta ameshanunua anachotaka na kusahau kabisa kuhusu wewe.

Sitaendelea na makundi ya chini hapo, kwa sababu nina imani picha umeipata.
Fanya kila unachoamini kitafanya kazi kwa upande wako wa mauzo, halafu jumlisha na mazungumzo ya kutosha na watu.
Post vile utakavyo, tuma jumbe nyingi uwezavyo, fanya chochote ambacho kinakupa amani.
Halafu sasa, wakati unasubiri simu ziite, na wewe unakuwa unazipiga kwa wingi.

Kwa zama tunazoishi sasa, kama mambo hayaendi unatakiwa uyalazimishe kwenda.
Wakati unasubiri simu ziite na wewe endelea kuzipiga.
Usiwe mvivu na mzembe.
Ongea na watu.
Wengi iwezekanavyo.
Hayo ndiyo mauzo.

Huenda unayajua yote haya, lakini bado kuchukua hatua zilizo sahihi inakuwa vigumu kwako.
Kwenye ukurasa utakaofuata tutaliangalia hilo kwa undani zaidi.
Lakini mpaka wakati huo, usisubiri simu ziite, bali ziitishe wewe.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe